Wanafunzi zaidi ya 600 katika shule ya sekondari Nansimo wanatumia choo ya matundu manne. - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Sunday 25 February 2018

Wanafunzi zaidi ya 600 katika shule ya sekondari Nansimo wanatumia choo ya matundu manne.



Zaidi ya wanafunzi 600 katika shule ya sekondari Nansimo iliyoko katika halmashauri ya wilaya ya Bunda Mkoani Mara wanatumia matundu manne ya choo.

Hali hiyo imepelekea wanafunzi wa shuleni hapo kuiomba serikali kusikia kilio chao na kuwajengea choo kitakachokidhi idadi ya wanafunzi waliopo kwa kuwa hivi sasa wanapata usumbufu mkubwa  wakati wa kujisaidia kwani wanapanga foleni kusubira huduma hiyo.

Aganda Alex Daudi pamoja na Doto Manyama ni wanafunzi shuleni hapo wameeleza kwamba wanakumbwa na usumbufu mkubwa kwa upungufu wa matundu ya vyoo kwakuwa mara nyingi wanafunzi wamekuwa wakipanga foleni kusubiri wenzao wamalize kujisaidia ndipo na wao wapate huduma hiyo.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Elias Supira amekiri kuwepo kwa upungufu huo wa matundu ya vyoo na kueleza kwamba mwaka jana walikuwa na matundu sita vyoo vilivyokuwa vikitumiwa kwa wasichana na matundu manne kwa wavulana, ambapo baadae ya wasichana yalibomoka hivyo yakabaki ya wavulana pekee.

Amesema changamoto hiyo wameshalitolea taarifa kupitia kamati ya maendeleo ya kata lakini mpaka sasa halijafanyiwa kazi licha ya kwamba suala hilo linaweza kupelekea shule hiyo kufungwa kwa tahadhari ya usalama wa afya ya wanafunzi na jamii inayoishi katika eneo hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya kata ya Nansimo ambae pia ni diwani wa kata hiyo bwana Sabato Mafwimbo amesema changamoto hiyo ni hatari na inaweza kusababisha shule kufungwa huku hasara kubwa ikiwa ni kwa wazazi na wanafunzi wanaosoma shuleni hapo, hivyo amewaomba wazazi watakapoombwa kuchangia maendeleo ya ujenzi wa choo shuleni hapo watowe ushirikiano.

Hata hivyo kwa upande wa wananchi wa kata hiyo, wamesema kuwa watakuwa tayari kushirikiana na serikali kumaliza changamoto hiyo.

Aidha changamoto ya ukosefu wa matundu ya vyoo katika shule mbalimbali halmashauri ya mji na wilaya ya bunda bado ni tatizo kubwa kwani hivi karibuni mjini hapo shule moja ya msingi ilifungwa kwa siku 14 kwa kukosa choo.

No comments:

Post a Comment