Polisi yafunguka sakata la kupiga mtu risasi maandamano ya Chadema - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Saturday 17 February 2018

Polisi yafunguka sakata la kupiga mtu risasi maandamano ya Chadema



Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amekiri mtu mmoja kupigwa risasi na polisi wakati wakiwatawanya wafuasi wa Chadema walioandama jana Februari 16, 2018.

Wafuasi hao wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe waliandamana kuelekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kinondoni, Aron Kagurumjuli kudai viapo vya mawakala wa chama hicho.

Maandamano hayo yalianzia viwanja vya Buibui Mwananyamala ulikokuwa ukifanyika mkutano wa kampeni wa Chadema na yalipofika eneo la Mkwajuni wafuasi hao walitawanywa na polisi, huku mtu mmoja aliyekuwa kwenye basi la daladala akidaiwa kupigwa risasi na kufariki dunia.

Akizungumza na MCL Digital, Februari 17 leo Jumamosi, Mambosasa amesema “Walizuia mwendo kasi, wakaanza kupiga mawe kwa hiyo kati ya risasi za hewani zilizopigwa kuwatawanya kuna iliyompata (mtu).”

Ufafanuzi huo wa Mambosasa licha ya kutoweka wazi kama mtu huyo amefariki dunia ama la, umekuja huku ikidaiwa kuwa aliyepigwa risasi na kupoteza maisha ni mwanafunzi wa elimu ya juu.

Soma: Mawakala waendelea kuzuiwa, msimamizi afafanua

Taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo zilianza kusambaa tangu Ijumaa jioni katika mitandao ya kijamii sambamba na kuwekwa picha yake huku ikieleza kuwa amepigwa risasi wakati akiteremka katika basi.

Mambosasa alipoulizwa kama mtu huyo ni mwanafunzi wa elimu ya juu amesema, “Haijathibitishwa hiyo, nipo kwenye pilika za uchaguzi, nadhani nitajibu hilo nitakaporejea ofisini na kupata taarifa.”

Uchaguzi wa majimbo ya Kinondoni na Siha unaendelea leo Jumamosi na Mwananchi litakuwa linakuletea kila kinachoendelea.

No comments:

Post a Comment