Showing posts with label SIASA. Show all posts
Showing posts with label SIASA. Show all posts

Thursday, 27 February 2025

 

Baraza la madiwani Bunda TC wapitisha bajeti ya bilion 2.24 ya TARURA kwa 2025 na 2026

27 February 2025, 

Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Bunda Michael Kweka kulia akiwa na mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Bunda Juma Haji

Fedha hizo zikipitishwa kama zilivyopendekezwa zitakwenda kutelezeza hatua tofauti za ujenzi wa miundombinu ya barabara kama vile ujenzi wa barabara mpya, ujenzi wa mitaro, uwekaji wa taa za barabarani maeneo ya senta pamoja na ujenzi wa madaraja na karuvati.

Na Adelinus Banenwa

Baraza la madiwani la halmshauri ya mji wa Bunda limepitisha shilingi Bilion 2.24 kama makadirio ya bajeti ya TARURA kwa mwaka wa fedha 2025 na 2026 ili kutekeleza hatua mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa halmashauri ya mji wa Bunda.

Akiwasilisha mapendekezo hayo meneja wa wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA muhandisi Ahimidiwe Kiruswa mbele ya baraza hilo la madiwani amesema katika fedha hizo zikipitishwa kama zilivyopendekezwa zitakwenda kutelezeza hatua tofauti za ujenzi wa miundombinu ya barabara kama vile ujenzi wa barabara mpya, ujenzi wa mitaro, uwekaji wa taa za barabarani maeneo ya senta pamoja na ujenzi wa madaraja na karuvati.

Sauti ya meneja wa TARURA muhandisi Ahimidiwe Kiruswa
Baadhi ya Madiwani katika kikao cha bajeti ya Bunda

Katika ushauri wao baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo wamemtaka meneja huyo wa TARURA kuhakikisha anamaliza viporo vya barabara vilivyobaki katika mwaka wa fedha 2023 na 2024 pia kuamalizia mpango wa utekelezaji wa mwaka 2024 na 2025.
Aidha madiwani hao wamemtaka meneja huyo wa TARURA kuhakikisha anawasimamia wakandarasi wanaopewa kazi za ujenzi wa miundombinu ya barabara kutokana na wakandarasi hao kuwa na tabia ya kutelekeza kazi na kuacha changamoto kubwa kwa wananchi,

Sauti ya baadhi ya madiwani wa halmashauri ya Bunda mji
katibu tawala wilaya ya Bunda ndugu Salumu Mtelela

Naye katibu tawala wilaya ya Bunda ndugu Salumu Mtelela amempongeza meneja wa TARURA kwa kuendelea kusimamia uboreshaji wa miundombinu ya barabara mjini Bunda huku akimuelekeza kuendelea kusikiliza ushauri unaotoka kwa madiwani kwa kuwa hao ndiyo wanaoishi katika maeneo yao na changamoto kubwa za barabara wanafahamu zipo maeneo gani.

Sauti ya katibu tawala wilaya ya Bunda Salumu Mtelela

Thursday, 20 February 2025

 

Madiwani Bunda DC wakubali kupitisha bajeti ya Tsh, 36,5 bilion

20 February 2025, 

Makamu mwenyekiti wa halmashauriya Bunda DC Mhe Keremba Irobi

Baraza la Madiwani halmashauri ya wilaya ya Bunda limepitisha makadilio ya bajeti ya shilingi Bilion 36.5 kwa mwaka wa fedha 2025 na 2026

Na Adelinus Banenwa

Baraza la Madiwani halmashauri ya wilaya ya Bunda limepitisha makadilio ya bajeti ya shilingi Bilion 36.5 kwa mwaka wa fedha 2025 na 2026 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, mishahara ya watumishi, kulipa madeni, pamoja na matumizi mengine.

Bajeti hiyo imepitishwa leo tarehe 20 Feb 2025 katika baraza hilo liliketi kujadili ambapo pamoja na mambo mengine baraza hilo lilipitia mapendekezo ya kamati mbalimbali za halmashauri.

Kikao hicho kimeongozwa na makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo mhe Keremba Irobi.

Sauti ya makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo mhe Keremba Irobi
Viongozi wa halmashauri wakiongozwa na mwenyekiti wa halmashauri hiyo Mhe Magafu Manumbu katikati, mkurugenzi wa halmashauri stanley Mbilinyi kulia na makamu mwenyekiti wa halmashauri Mhe Keremba Irobi

Katika ushauri wao madiwani hao wameshauri mkurugenzi pamoja na wataalamu kuzingatia maoni ya kamati katka utekelezaji wa miradi ikiwa ni pamoja na kupeleka huduma mahala ambapo hazipo kama katika  sekta za  Elimu na Afya.

Sauti za maoni ya baadhi ya madiwani kuhusu bajeti
Katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela

Kwa upande wake katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela ameipongeza halmashauri hiyo kwa ukusanyaji mzuri wa mapato ambapo amesema kwa mwaka wa fedha 2023 na 2024 halmashauri hiyo ilikusanya zaidi ya malengo.

Mtelela amewahimiza watumishi wa halmashauri hiyo wakiongozwa na mkurugenzi kuendelea kukusanya mapato pia kumaliza miradi ambayo inaendelea kutekelezwa katika halmashauri hiyo.

Sauti ya katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela
Baadhi ya madiwani katika baraza la Bunda DC

Wakati huo huo baraza hilo la madiwani halmashauri ya wilaya ya Bunda limepitisha mapendekezo ya Bajeti ya Wakala wa  barabara za mijini na vijijini TARURA ya shilingi bilion 7.6 ikijumuisha fedha za upanuzi wa barabara milioni 800 fedha za mfuko wa jimbo bilion 1 na Fedha za tozo ya mafuta bilion 2.

Sauti ya makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo mhe Keremba Irobi

Akizungumza katika baraza hilo kaimu meneja TARURA Bunda  Muhandisi Hamad Munisi amesema endapo  fedha hizo zikipitishwa  zinakwenda kutekeleza hatua mbalimbali ikiwemo ujenzi wa makarvati, ufunguaji wa barabara mpya, ujenzi wa barabara za lami na ujenzi wa mitaro.

kaimu meneja TARURA Bunda  Muhandisi Hamad Munisi

Tuesday, 13 February 2018

Ester Bulaya Atangaza Vita "Vita ni Vita Mura"



Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA na Mbunge wa Bunda, Mhe. Ester Bulaya ametangaza vita katika Jimbo la Kinondoni huku akiapia kwa Mungu wake kuwa atalinda kura za mgombea wao na lazima atangazwe mshindi kwa madai wamejipanga vilivyo.

Bulaya ametoa kauli hiyo zikiwa zimebakia takribani siku nne pekee kuelekea marudio ya uchaguzi mdogo katika majimbo ya Siha na Kinondoni ili wananchi wa maeneo hayo kupiga kura kwa mtu anayemuhitaji kuwa muwakilishi wake katika jimbo.

"Haki ya Mungu, Baba wa Taifa angekuwa hai angetoka CCM kwa sababu CCM ile sio hii ya sasa ambayo haifuati utaratibu, poleni wanaccm wenzangu wa zamani mmedharauliwa kwa kutoshiriki kura za maoni kumpata Maulid Mtulia. Baba wa Taifa alikuwa haendekezi vitu kama hivyo, lakini anafanya hivyo akiamini kabisa wanakinondoni mtachagua mgombea mnaemtaka halafu watatumia nguvu", amesema Bulaya.

Pamoja na hayo, Bulaya ameendelea kwa kusema "haki ya Mungu ngojeeni niwaambie hii ni 'game' ni sawa na 'Escape from Sobibor' yaani tunapiga kura, tunalinda kura na lazima mtu atangazwe. Sisi kule kwetu tunasema vita ni vita mura na nipo hapa lazima mtu atangazwe, polisi wananisikia yaani mara mia wao wahamishe kituo chao lakini sisi mtu wetu lazima ashinde.  Tumerudi kwa kujipanga".

Kwa upande mwingine, Bulaya amewataka wananchi wa jimbo hilo kutorudia kosa kwa kumchagua mtu ambae atawarudisha tena kwenye sakata la uchaguzi kama ilivyokuwa sasa.

Sunday, 11 February 2018

Chadema, CUF wadai kuna njama zinafanyika Kinondoni



Wakati wagombea ubunge wa Siha na Kinondoni wakiendelea kujinadi, vyama vya Chadema na CUF vimedai kuna njama zinafanyika Kinondoni baada ya mawakala wao kulazimishwa kula kiapo bila kukabidhiwa viapo vyao.

Jana kwa nyakati tofauti, mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kinondoni, Waziri Muhuzi na mkurugenzi wa habari, uenezi na uhusiano wa umma wa CUF, Abdul Kambaya walisema endapo viapo havitatolewa katika muda muafaka mawakala wao wanaweza kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kusimamia kura za ubunge na udiwani.

Muhuzi alisema katika kata ya Hananasif, mawakala 50 wa Chadema kati ya 611 wa jimbo hilo walilazimisha kupewa viapo hivyo, huku Kambaya akibainisha kuwa mawakala wote wa CUF wamekubali kula kiapo bila kupewa viapo vyao, kwamba watawasilisha malalamiko yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Muhunzi alisema kitendo cha kuapa kimefanyika kinyume na kanuni za uchaguzi zinazoagiza wakala kuapa na kuondoka na kiapo chake.


Mvutano huo umeibuka ikiwa imepita siku mbili tangu NEC kuvitaka vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo mdogo unaofanyika Februari 17, kuwasilisha majina ya mawakala wao.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima alisema ili wakala akamilike, lazima awe na barua kutoka kwenye chama chake, ale kiapo na awe na barua ya utambulisho kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi kwenda kwa msimamizi wa kituo.

Alipotafutwa jana kueleza kuhusu mawakala hao kunyimwa viapo, Kailima alisema vyama hivyo vina haki ya kuwasilisha madai hayo.
“Mawakala wa vituo ni 611 , vyama vipo 12 na jumla ni mawakala 7,332 sasa unawezaje kusaini viapo vyao leo (jana) kwa mkupuo? Wakati huo chama kimoja kimeleta majina jana mchana ambayo ilikuwa siku ya mwisho,” alisema.

Alibainisha kuwa mawakala kupata kiapo si hatua ya mwisho inayowatambulisha kuwa mawakala rasmi.

“Kuna hatua tatu, kwanza kula kiapo lakini bado anatakiwa kuwa na barua ya utambulisho wa chama na barua nyingine ya msimamizi wa uchaguzi kwenda kwa msimamizi wa kituo cha uchaguzi. Sasa barua hizo asaini mtu huyo mmoja kwa siku moja!” alihoji.

Kailima alitoa wito kwa vyama kubadilika huku akiahidi mawakala hao kupatiwa viapo hivyo leo.

“Viapo watapewa tu hata kesho (leo), lakini tubadilike. Busara tu ilitakiwa kuwasilisha mapema majina hayo bila kusubiri siku ya mwisho,” alisema.

Katika maelezo yake, Muhuzi alisema kumekuwa na changamoto katika kata zote 10 za Kinondoni na mgogoro zaidi ulijitokeza katika kata za Kijitonyama, Makumbusho na Mwananyamala.

“Wanataka viapo vichelewe kutoka hadi siku ya uchaguzi ili kuleta usumbufu kwa mawakala kutotambulika, na wizi wa kura ufanyike. Hali hii imejitokeza kwa mawakala wetu kata zote 10 za jimbo hili,” alisema.

Hata hivyo, alifafanua kuwa kutokana na wingi wa mawakala, haikuwa rahisi kwa wasimamizi wa uchaguzi kusaini viapo vyao vyote kwa wakati mmoja.

Mwandishi wetu alishuhudia vurugu zilizodumu kwa zaidi ya saa mbili, kuanzia saa sita mchana katika ofisi za Kata ya Hananasif kabla ya mawakala kukubali kula kiapo, huku baadhi ya wafuasi wa Chadema wakizunguka eneo hilo wakiimba, “Tunataka viapo vyetu.”

Mgogoro uliibuka baada ya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi katika kata hiyo kudai kuwa hakuna wakala atakayekabidhiwa hati yake leo kutokana na maelekezo ya msimamizi wa uchaguzi, Aron Kagurumjuli.

Katibu wa Chadema Kata ya Hananasif, Daniel John alisema maelekezo ya NEC yanataka wakala kula kiapo kisha kuondoka na hati.

Alisema kutokabidhiwa hati hizo za viapo kunaweza kuwa ni mpango kukataliwa kwa mawakala wao katika uchaguzi huo.

Kambaya kwa upande wake alisema, “Mawakala 611 wa CUF wamekubali kuapishwa bila kupewa viapo ila tumewasilisha barua ya malalamiko ofisi ya NEC.

“Hii iliwahi kutokea Kata ya Saranga, mawakala walinyimwa viapo na hawakupata hadi siku ya uchaguzi wakiwa wamechelewa kuingia kwenye vituo ila mawakala wa CCM walikuwa wamepewa, hii haikubaliki. Kiapo ni mali ya wakala na anatakiwa kupewa siku hiyohiyo kwa mujibu wa kanuni.”

Akizungumzia suala hilo, mgombea wa Chadema jimbo la Kinondoni, Salum Mwalimu alisema CCM imebanwa kila kona Jinondoni, ndio sababu ya kuanza mvutano huo wa mawakala.

“Huwezi kuwaapisha mawakala leo halafu ukamwambia utawapa barua zao za kiapo. Hivi utaratibu wa kumpigia simu wakala aje kuchukua barua ya kiapo umeanza lini na utawapigia wangapi,” alihoji Mwalimu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar).


Walivyojinadi

Wakati NEC ikitoa ufafanuzi huo, jana CUF na CCM ziliendelea na kampeni huku Chadema kikiahirisha kampeni za Mwalimu kutokana na kushiriki mazishi ya kada wa chama hicho, Tambwe Hiza aliyefariki dunia siku tatu zilizopita.

Akijinadi katika mkutano wa kampeni kwenye Uwanja wa Jaba, Kigogo Mbuyuni, mgombea wa CUF, Rajab Salim alisema akichaguliwa atahakikisha anaishauri Serikali kufuta ada za kuhifadhi maiti kwa maelezo kuwa wakati wa kuuguza, ndugu hutumia fedha nyingi.

Alisema mbali na hilo, pia atahakikisha analimulika suala la bima kwa wazee na wanawake kwa kutumia mfuko wa jimbo lengo likiwa ni makundi hayo kupata huduma ya afya bila usumbufu.

“Pia nitahakikisha nasimamia mifereji inayotiririsha majitaka. Nitahakikisha mitaa ya Kigogo taa za barabarani zinawaka ili kuondoa uhalifu. Kero zote nazifahamu, naomba tuache demokrasia ifanye kazi yake mkinichagua nitaanza na kero za watu wanaoishi mabondeni kama nyie mliopo Kigogo,” alisema.

Akijinadi katika Viwanja vya Tandale shule ya msingi, mgombea wa CCM, Maulid Mtulia alianza kwa kuwajibu wanaoponda uamuzi wake wa kujiuzulu ubunge wa Kinondoni kwa tiketi ya CUF na kuhamia CCM alikopitishwa tena kuwania nafasi hiyo, kwamba alifanya hivyo kwa nia njema.

“Nilikuwa eneo lisilo sahihi na hatukuwa tukizungumza lugha moja hivyo ingekuwa ngumu mimi kuwaletea maendeleo na kutatua kero zenu,” alisema Mtulia,

“Mnaona wenye Serikali yao wote wapo hapa, hii inaonyesha ushirikiano walio nao na kwa mtindo huu itakuwa rahisi kwangu kutatua kero zenu.”

Huku akimtolea mfano Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako aliyekuwa katika mkutano huo, Mtulia alisema, “Ndalichako yule pale naweza kumuomba anifanyie ukarabati shule hii ya Tandale ambayo mimi nilisoma. Naomba mjitokeze kwa wingi kunichagua tuijenge Kinondoni mpya pamoja,” alisema.

Katika Jimbo la Siha, mgombea wa CCM, Dk Godwin Mollel alisema akichaguliwa kuwa mbunge atahakikisha wananchi wa Kata ya Ngarenairobi wanapata maeneo kwa ajili ya kujenga nyumba za makazi.

Dk Mollel ambaye pia alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema kabla ya kuhamia CCM Desemba mwaka jana na kupitishwa tena kuwania nafasi hiyo, alisema wapo wananchi wanaotaabika kwa kukosa makazi kutokana na kukosa maeneo.

“Naombeni mnitume nikawatumikie, ninawaahidi kuwatafutia maeneo ya makazi, pia nitahakikisha mnapata tangi la maji ambalo litatumiwa kusambaza maji katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo,” alisema.

Aliwataka wananchi kuepuka siasa za chuki na uadui na kuhakikisha wanafanya kampeni za kistaarabu.