Alikuwa analinda mazao yake yasiliwe na tembo na ndiyo kawaida yetu maana bila kulinda huwezi kuvuna chochote.
Na Adelinus Banenwa
Kijana mmoja aliyetambulika kwa jina la Kinyunyi Nyakile mkazi wa mtaa wa Ichamu kata ya Kunzugu Halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara amepteza maisha baada ya kushambuliwa na tembo wakati akilinda bustani yake ya nyanya.
Tukio hilo linatajwa kutokea usiku wa kuamkia Juni 8, 2025 ambapo inaelezwa kundi la tembo zaidi ya watano walifika karibu na mashamba ya wakulima hapo Kunzugu ndipo wakulima walianza kuwafukuza lakini tembo mmoja aligeuka na kuanza kuwakimbiza hadi alipomshika Kinyunyi na kumkanyaga vibaya hali iliyopelekea kupoteza maisha.
Mwenyekiti wa mtaa wa Ichamu James Magwayega Haruna ameiambia mazingira fm kuwa tukio hilo limewasikitisha kutokana na kupoteza nguvu kazi ya mtaa na imekuwa kawaida kwa wakazi wa mtaa wake ili wavune mazao yao ya shambani ni lazima kulinda.
Kwa upande wake Magambo Magambo ambaye ni baba mdogo wa marehemu Kinyunyi amesema kama familia wamepoteza mtu muhimu sana hasa ukizingatia alikuwa bado mdogo na alikuwa hajawa na familia Aidha ameiomba serikali kujenga uzio kuzuia wanyama hao ili kunusuru maisha ya wananchi na mazao.
Naye diwani wa kata ya Kunzugu Mhe Pasaka Samson amesema taarifa za mwananchi wake alizipata usiku ambapo alichukua hatua ya kwenda hadi eneo la tukio kisha aliwasiliana na mamlaka mbalimbali ikiwemo watu wa Kikosi dhidi ya ujangiri KDU, Jeshi la polisi pamoja na ofisi ya mkuu wa wilaya.
Mhe Pasaka amesisitiza kuwa serikali ione umuhimu wa kuongeza gari la doria kwa kuwa lililopo halitoshi kuanzia Balili hadi Tungirima ambao ni ukanda wote wa hifadhi ya taifa ya Serengeti.
No comments:
Post a Comment