Mbarawa atoa miezi 9 kwa mkandarasi nyaza roads works-Bunda Mara - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Monday 19 February 2018

Mbarawa atoa miezi 9 kwa mkandarasi nyaza roads works-Bunda Mara





Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na wakazi wa kijiji cha Kisorya, wilaya ya Bunda alipokutana nao baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Bulamba-Kisorya yenye urefu wa KM 51 inayojengwa kwa kiwango cha lami, wilayani humo, mkoani Mara.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka mkandarasi Nyanza Road Works kukamilisha ujenzi wa barabara ya Bulamba-Kisorya yenye urefu wa KM 51 kwa kiwango cha lami ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.

Prof. Mbarawa ametoa kauli hiyo wakati akikagua ujenzi wa barabara hiyo na kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Kisorya na kusema kuwa usanifu wa barabara na madaraja katika barabara hiyo umewasilishwa sasa ni jukumu la mkandarasi kuendelea na ujenzi kwa kasi na kwa viwango vya ubora.

“Serikali ina nia njema kwa wananchi wa wilaya ya Bunda na mkoa wa Mara sasa tunaijenga barabara hii na mwishon mwa mwaka mtaanza kunufaika nayo”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo utarahisisha mawasiliano na kupunguza gharama za shughuli za usafirishaji wa samaki, mazao na abiria, uboreshaji makazi na kukuza uchumi kwa maeneo yaliyo kando ya barabara.

Kuhusu suala la fidia, Prof. Mbarawa amefafanua kuwa Serikali italipa fidia kwa mwananchi ambaye barabara imemfuata kama anavyostahili.

“Serikali haina nia ya kumuonea mtu yeyote bali inachofanya inalipa kulingana na sheria inavyoelekeza”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Makutano-Sanzale KM 50 na kumwagiza mkandarasi wa M/S Mbutu JV Contractor (T) kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kabla ya mwezi Julai mwaka huu.

“Mradi huu ni wa muda mrefu sana na wananchi wameusubiri kwa muda kama hamtamaliza mradi huu mpaka mwezi juni, hii itakuwa kazi yenu ya mwisho, maana ninategemea nyinyi kama wazawa mngekuwa wa mfano” amesisitiza Prof. Mbarawa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amesema kwa sasa mkoa umeamua kupata taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa miradi ya barabara kila baada ya miezi mitatu ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Mara, Mhandisi Mlima Ngaile amesema Wakala utasimamia mradi wa ujenzi wa barabara hizo na kuhakikisha mradi unazingatia viwango kulingana na mkataba.

Waziri Prof. Mbarawa yuko mkoani Mara kwa ziara ya siku mbili akiwa na lengo la kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya sekta ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment