MRATIBU wa shughuli za UKIMWI katika halmashauri ya wilaya ya Bunda mkoani Mara, Vitus Gwanko amedai serikali kwa sasa haina bajeti ya kuwahudumia wananchi wa kawaida wanaoishi na virusi vya UKIMWI badala yake shughuli hiyo imeachiwa mashirika yasiyo ya kiserikali(NGO’s).
Akijibu hoja za madiwani waliotaka kujua sababu za halmashauri hiyo kutokuwa na bajeti ya kuwahudumia watu wa kawaida wanaoishi na VVU, Gwanko alidai kwa mwongozo waliyo nayo sasa halmashauri imeweka bajeti ya kuwahudumia watumishi wa umma pekee wanaoishi na VVU ndani ya halmashauri husika na sio watu wa kawaida.
Kwa mujibu wa Gwanko, halmashauri ya wilaya ya Bunda kwa sasa haina bajeti ya kuwahudumia waviu, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya UKIMWI, upatikanaji wa madawa ya ARV’s na huduma zingine.
Alidai awali halmashauri zilikuwa na bajeti hiyo kutoka tume ya kudhibiti Ukimwi nchini(TACAIDS) ambayo ilikuwa ikipata fedha toka kwa wafadhili na kwamba tangu wafadhili wasitishe mradi huo, huduma ya kutoa madawa ya kufumbaza virusi(ARV’s) na huduma zingine kwa WAVIU imebaki kwa mashirika na asasi za kiraia na sio serikali.
Naye ofisa utumishi katika halmashauri hiyo, Bakarani Oriwo alieleza kuwa bajeti iliyopo katika halmashauri yake inahusu WAVIU ambao ni watumishi wa umma na kwamba hiyo inatokana na agizo la serikali la kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanaoishi na VVU wanapewa huduma stahiki katika vituo vyao vya kazi na sio wananchi wa kawaida.
“Mwananchi wa kawaida anapata huduma hizi bure kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanafanyakazi hii kwa mujibu wa sheria nchini kote, lakini sisi katika bajeti yetu haijatuelekeza kuwahudumia WAVIU ambao sio watumishi wa umma” alisisitiza Oriwo.
Hata hivyo baadhi ya madiwani waliitaka serikali kuweka mpango wa kutenga bajeti kwa ajili ya wananchi wanaoishi na VVU huku wakitoa tahadhari kuwa siku mashirika na asasi za kiraia zitakapositisha shughuli zao za kuwahudumia WAVIU kutatokea shida kubwa nchini.
Madiwani hao walisema hivi sasa WAVIU wengi wanakosa huduma ya ushauri nasaha, pamoja na kutumia muda mwingi katika kufuatialia huduma hizo ikiwa ni pamoja na ARV’s).
Walisema si vyema serikali kuonesha upendeleo wa kutenga bajeti kwa ajili ya kuwahudumia WAVIU ambao ni watumishi wa umma pekee huku wananchi wenyewe wakitegemea hisani toka kwa wafadhili.
Mjadala huo ulikuja baada ya Mwenyekiti wa kamati ya UKIMWI katika halmashauri hiyo, Simba Mramba kulilieleza baraza la madiwani kuwa halmashauri hiyo imetenga jumla ya shilingi milioni 4 tu kwa ajili ya kuwahudumia wafanyakazi wanaoishi na VVU katika mwaka wa fedha 2018/2019.
No comments:
Post a Comment