Milioni thelathini za kuweka umeme shule ya sekondari Nansimo zimepigwa? –Wananchi Bunda Mara - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Thursday 22 February 2018

Milioni thelathini za kuweka umeme shule ya sekondari Nansimo zimepigwa? –Wananchi Bunda Mara



Jumla Shilingi  milioni  thelathini  zilizo  tolewa  na  serikali  katika  mwaka  wa  fedha 2015-2016  za  kuweka umeme  shule ya sekondari Nansimo iliyopo wilayani Bunda mkoa wa Mara  zinadaiwa kutumika katika matumizi yasiyo eleweka.

Kutokana  na hali  hiyo  wazazi  na  walezi  wenye  watoto  wanaosoma shuleni hapo wamechachamaa na kulazimika kuonana na uongozi wa shule hiyo shuleni hapo na kujadili matumizi ya fedha hizo.

Kikao hicho  kimeongozwa  na  mwenyekiti  wa  bodi  ya  shule  hiyo Constantini Mazani akisaidiwa na mkuu wa shule hiyo  Elias Supira  ambae  alikuwa  katibu wa kikao.

Katibu  wa   kikao  hicho  mwalimu  Supira   ameeleza kuwa  wakati ameanza kazi shuleni  hapo  fedha   hizo  zilikuwa  tayari zimeingizwa kwenye  akaunti  ya  kata na  wakati huo huo kiasi cha  shilingi milioni  kumi na  tano zilikuwa zimekwisha kutumika  kuweka  nyaya za umeme  kwenye  madarasa  matatu,jingo la utawala  pamoja  na nyumba saba za waaalimu.

Amesema kuwa fedha  nyingine  iliyobaki  hakuwanayo taarifa japo alijua kwamba  fedha ipo  lakini  kwenye akaunti ya kata  hivyo mwenye  majibu sahihi  ya ubadhilifu   wa fedha ni  mheshimiwa diwani  na mtendaji wa kata aliye kuwepo  kwa sababu wao ndio wahusika.

Akielezea muafaka  wa  kikao  walichokaa baada ya  mvutano mkali  mwalimu Supira ameeleza  kwamba  afisa tarafa alikubali kulichukua na kulifanyia kazi  na kuahidi kulifatilia ofisi ya kata  na kuzungumza  na diwani pamoja na mtendaji wa kata ili wajue nini kilichojiri wakati huo.

Amesema kuwa  kama  shule swala hilo  limewaathiri  kwani majengo mengi  ya shule hayana  umeme  kwani fedha hizo zingetumika ipasavyo  shule nzima  ingekuwa na umeme.

Naye  mwenyekiti  wa serikali  ya kijiji cha Nansimo  Justace  Masige amesema  wakati anaingia  madarakani  alikuta  mchanganuo wa shilingi  milioni  kumi na tano ambazo zilikuwa zimeletwa  Nansimo sekondari  kwa  ajili ya ujenzi  lakini  baada  ya  kikao   cha  maendeleo ya  Kata  fedha hizo  zikaombewa zibadilishwe matumizi  kutoka ununuzi wa transifoma  nakuingizwa kwenye  mfumo wa  kuingiza umeme shuleni hapo na  kuridhiwa  na wajumbe.

Amesema baada ya maridhiano hayo fedha hizo zilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya shule na kupelekwa kwenye akaunti ya kata,ambapo msimamizi mkuu alikuwa ni katibu wa maendeleo ya kata ambae ni mtendaji kata.

Masige amesema kuwa mtendaji wakata ndiye aliyekuwa akizisimamia na ndiye aliyekuwa muhimili mkubwa wa manununuzi na matumizi ya fedha hizo na kufunga mkataba na waingizaji wa umeme shuleni hapo.

Amedai kuwa katika kikao walichokaa hivi karibuni wazazi walihoji matumizi ya fedha hizo na kugundulika kuwa zimetumika kuingiza umeme katika baadhi ya nyumba tu za walimu na kuacha baadhi ya majengo jambo ambalo halikuwa makubaliano hivyo wazazi wakaamu iundwe tume ya kuchunguza fedha hizo.

Aidha baada ya ufuatiliaji katika ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya  imebainika kuwa  hakuna idhini iliyotolewa kubadilisha matumizi ya fedha hizo.

Kufuatia hatua hiyo wazazi wameagiza viongozi hao walete mikataba inayoonyesha makubaliano na namna fedha hizo zilivyotumika katika miradi hiyo.
Kwa upande wake Diwani wa viti maalum Nyamtondo Oliver Deus amesema kuwa tume iliyoundwa kufuatilia fedha hiyo iligundua kwamba shilingi milioni 15 zilitumika kujenga maabara, milioni mbili zilitumika kukopesha, na milioni kumi na tatu ilitumika kukopesha ofisi ya mkurugenzi na kufanya kazi nyingine kwa maelezo kwamba itakapoitajika itarejeshwa.

Amesema kwamba katika kikao hicho Diwani wa kata hiyo Sabato Mafwimbo alijaribu kueleza kwamba hiyo fedha ilikopwa na ofisi ya mkurugenzi lakini wazazi hawakuridhika na kuamua kuunda kamati ndogo kufuatilia kwa mkurugenzi ambapo mkurugenzi aliwaeleza kwamba hakuna nyaraka zozote zinazoonyesha kwamba fedha hiyo ilikopwa na ofisi yake.

Hata hivyo alipoulizwa Diwani wa kata hiyo ambaye pia ni Makam Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Bunda  Bwana  Sabato Mafwimbo  amekiri kufahamu jambo hilo na kueleza  kuwa fedha hiyo imeingizwa kwanye ofisi ya kata mwaka  2013/14, ambapo ilitolewa shilingi milioni 90,kwa shule tatu za wilaya Bunda ambazo ni Guta milioni 30, Bulamba milioni 30, na Nansimo milioni 30.

Akizungumzia shilingi milioni 30  za kata yake amedai mkandarasi wa kuweka umeme katika shule hiyo alitafutwa na mwenyekiti wa Halmashauri na mkurugenzi lakini fedha ilitumwa kwenye mfuko wa maendeleo ya kata kama wasimamizi wa maendeleo ya kata, ambapo alipotumwa mkandarasi kuanza kazi wao walimkataa kwa madai ya kutomtambua na kumuagiza alete mkataba.

Aidha baada ya kuleta mkataba wake aliendelea na kazi na malipo yalikuwa yakifanywa na ofisi ya kata,kwa masharti kwamba atakuwa akilipwa fedha kulingana na kazi atakayokuwa amefanya ambapo alilipwa na kubakia fedha nyingine ambayo amedai kuwa hakumbuki vizuri lakini anakadiria kuwa ilikuwa kama shilingi milioni kumi na kitu.

Ambapo fedha hiyo iliyobaki ilikuwa ni kwa ajili ya kununulia Transfoma ,na baadae wakamuelekeza Mkurugenzi kwamba pesa hiyo haitoshi hivyo iongezwe nyingine kwa ajili ya ununuzi wa transifoma.

Ameeleza kwamba wakati wakiendelea na mchakato huo likajitokeza zoezi la ujenzi wa maabara, ambapo walikaa kamati ya maendeleo ya kata , wakamshirikisha afisa Tarafa na kiongozi aliyekuwa ameteuliwa wilayani kusimamia ujenzi wa maabara kwenye kata hiyo ambaye alisema amemsahau wakaamua kubadilisha matumizi  ya fedha hiyo.

Hata hivyo alipoulizwa kuhusu kuundwa kwa kamati ya kuchunguza suala hilo amedai kuwa kamati hiyo iundwe tu watapata maelezo ya kujitosheleza.








No comments:

Post a Comment