Afariki baada ya kukanyagwa na Tembo - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Tuesday 13 February 2018

Afariki baada ya kukanyagwa na Tembo



MKAZI wa kijijii cha Ilambila wilayani Kalambo, Maria Sekaye (60),   amefariki dunia baada ya kukanyagwa na tembo waliokuwa njiani wakitokea katika pori la akiba la Lwafu, kwenda katika nchi jirani ya Zambia.

Diwani wa Kata ya Mkowe, Alfred Mpandasharo, alisema tukio hilo lilitokea juzi  saa 4:00 asubuhi wakati mwanamke huyo akiwa ametoka kutembelea shamba lake lililokuwa limevamiwa na mazao kuliwa na tembo hao.

Alisema Maria akiwa njiani kurejea kijijini, ghafla alikutana na kundi kubwa la tembo waliokuwa na hasira wakiwa wamechokozwa na vijana wa kijiji hicho kutokana na kuwafukuza kwa kelele ili waondoke kijijini hapo waache kula mazao katika mashamba yao.

Diwani huyo alisema baada ya tembo hao kumkuta mwanamke huyo, walimvamia na kumwangusha kisha wakamkanyaga na kufa papo hapo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura, aliwaonya wananchi wanaowafukuza ovyo tembo hao, waache tabia hiyo kwa kuwa ni hatari kwa usalama wao badala yake wasubiri watendaji wa maliasili ambao watafika kwa ajili ya kuwafukuza.

Binyura alisema  kwa kawaida katika vijiji vya  Sundu, Mkowe, Ilambila na Katete huwa mapito ya tembo na mara kwa mara wamekuwa wakipita kwenda Zambia na baadaye kurejea tena nchini katika pori la akiba la Lwafu.

Alisema ni vizuri wananchi wakaacha kufanya kilimo na kujenga makazi katika mapito ya tembo kwa kuwa kawaida huwa hawaachi kupita hata kama itachukua miaka mingi lakini kuna siku watarejea na kupita tena, hivyo ni hatari kwao.

No comments:

Post a Comment