Prof. mbarawa aahidi kukamilika kwa ujenzi wa daraja la mto mara - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Saturday 17 February 2018

Prof. mbarawa aahidi kukamilika kwa ujenzi wa daraja la mto maraSerikali imesema ujenzi wa daraja la mto Mara lenye urefu wa mita 94 lililopo katika barabara ya Tarime-Mugumu-Nata litakamilika mwanzoni mwa mwezi wa nne mwaka huu.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, wakati akikagua ujenzi wa daraja hilo ambalo linaunganisha wilaya ya Tarime na Serengeti na kuwatoa hofu wananchi wa wilaya hizo kuwa endapo daraja hilo likikamilika litaondosha adha waliyokuwa wanaipata ya kuvuka hasa vipindi vya masika.

Kwa upande wake Mkandarasi wa kampuni ya M/S Gemen Engineering & Mayanga, Mhandisi Andrew Nyamtori, amesema kuwa mradi umekamilika kwa sehemu kubwa hivyo kazi zilizobakia ni kutandika vyuma juu ya daraja ili likamilike na kuanza kutumika na hivyo kuiomba Serikali kuendelea kuwaamini wakandarasi wazawa kwa kuwapa miradi mingine mikubwa.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Mara Mhandisi Mlima Ngaile, amesema watahakikisha wanamsimamia vizuri mkandarasi ili aweze kutekeleza mradi huo kwa viwango vyote na kwa wakati. 

Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa, amekagua kiwanja cha ndege cha Musoma na kueleza kuwa Serikali tayari imeshatangaza zabuni ya upanuzi wa kiwanja hicho na kuwa wakati wowote zabuni zitafunguliwa ili mzabuni kuweza kupatikana.

No comments:

Post a Comment