Maduka 139 yatiwa kufuli na TRA -Musoma - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Thursday 1 March 2018

Maduka 139 yatiwa kufuli na TRA -Musoma



Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mara, imeyafungia maduka 139 yasiyotumia mashine za stakabadhi za kielektroniki (EFDs).

Katika operesheni hiyo iliyoanza tangu Februari Mosi, TRA imefanikiwa kuwasajili zaidi ya wafanyabiashara 108 katika mfumo huo wa stakabadhi kwa njia ya kielektroniki. 
Meneja wa TRA Mkoa wa Mara, Edson Issanya amesema kuwa wafanyabiashara 159 tayari wametuma maombi na wamekidhi vegezo vya kufungiwa mashine hizo zitakazowezesha Serikali kufuatilia na kukusanya kodi zote stahiki bila udanganyifu.

“Tumeanza mchakato utakaowezesha wafanyabiashara wote waliotimiza masharti kufungiwa mashine hizo, kwa mujibu wa sheria,” alisema Issanya.

Hadi sasa, zaidi ya wafanyabiashara 857 kwa mujibu wa Issanya wamejiunga na mfumo wa utoaji wa stakabadhi kwa njia ya EFDs.

“TRA imefanikiwa kupatia ufumbuzi changamoto iliyokuwa ikiwakabili wafanyabiashara mkoani hapa ya kulazimika kufuata mashine hizo jijini Mwanza baada ya kuwasajili mawakala na wasambazaji watatu, wafanyabiashara hawana tena kisingizio kwa nini wasifunge mashine?” Alihoji meneja huyo.

Mmoja wa wafanyabiashara wa mjini Musoma, Juma Sondobhi alipongeza hatua ya TRA kusogeza upatikanaji wa mashine hizo mjini Musoma na kwamba, umewarahisishia upatikanaji wa huduma hiyo. “Ilikuwa gharama kubwa kusafiri hadi jijini Mwanza kutafuta mashine kwa sababu wakati mwingine tulilazimika kukaa huko kwa siku tatu kusubiri huduma, hivi sasa tunalipia na kuzipata hapahapa mjini,” alisema.

No comments:

Post a Comment