Friday, 29 December 2017

Swahiba Amtandika Mshale Na Kumuua Rafiki Yake Kisa Deni la Sh, 4,000 wilayani Bunda







Mkazi wa Mtaa wa Kilimahewa katika Halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara, Paul Juma (38), ameuawa kwa kuchomwa mshale na rafiki yake, baada ya kutokea ugomvi kati yao.

Inadaiwa ugomvi huo ulitokana na kumdai amuongeze Shilingi 4,000 kutokana na kumuuzia mabati manne chakavu kwa jumla ya Sh. 20,000.

Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Kamishna Msaidizi wa Polisi Jafari Mohamed, jana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kumtaja mtuhumiwa kuwa ni Julius Mtoni (48) mkazi wa mjini Bunda na watu hao walikuwa ni marafiki.

Kamanda Mohamed alisema tukio hilo lilitokea Desema 26 majira ya mchana wakati watu hao walipokuwa wanakunywa pombe ya kienyeji kwa mwanamke ambaye ni jirani yao.

Polisi wilayani hapa walisema Desemba 25, marehemu alimuuzia mtuhumiwa mabati manne chakavu kwa makubaliano ya kila bati Sh. 7,000.

Walisema kuwa siku hiyo mtuhumiwa huyo alimpatia marehemu Sh. 20,000 taslimu na kukubaliana kuwa atalipwa kiasi kingine cha Shilingi 8,000 kilichobakia siku nyingine.

Walisema Desemba 26 wakiwa wanakunywa pombe, marehemu alimdai mtuhukiwa amlipe Sh. 8,000 zilizokuwa zimesalia, lakini alimpatia Sh. 4,000 ndipo wakaanza kuzozana huku marehemu akishinikiza alipwe deni lake lote la Sh. 8,000.

Aidha, ilielezwa kutokana na kutokuelewana, marehemu alianza kumkaba mtuhumiwa, kisha kukimbilia nyumbani kwake na kuchukua upinde na kumfyatulia mshale ambao ulimpata begani.

Polisi walisema kuwa baada ya marehemu kuchomwa mshale huo aliuvunja na kubakiza kipande cha mshale huo mwilini mwake na kukimbilia polisi, lakini  alipoteza maisha kutokana na kutokwa na damu nyingi.

“Baada ya kuchomwa mshale huo marehemu aliuvunja na kubakiza kipande kikiwa mwilini mwake na kuja hapa polisi kisha hospitalini, lakini taarifa ya hospitali inaeleza alikufa baada ya kutokwa na damu nyingi,” alisema ofisa mmoja wa polisi ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake kwa madai sio msemaji wa jeshi hilo.

Mayanja asema na Wanawake wa mji wa Bunda kuhusu kujiunga katika SACCOS



Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Bunda Janeth Mayanja amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa saccos ya wanawake itakayozinduliwa mnamo january 4 2018 katika viwanja vya halmashauri hiyo.

Akizungumza na redio mazingira fm, Mayanja amesema kuwa siku hiyo ya uzinduzi wataanza kwa maandamano yakayoanzi  benki ya NMB mpaka viwanja vya halmashauri ya mji wa bunda.

Aidha amesema halmashauri kwa kugundua kilio na uhitaji wa wanawake katika mji wa bunda waliamua kuunda saccos hiyo itakayowasaidia wanawake kuinuka kiuchumi.

Hata hivyo amewataka wanaume kuwaunga mkono wanawake ili kufanikisha uchumi wa pamoja.

Kibara sekondary waja na mikakati mipya yakufanikisha ndoto ya wanafunzi Wilayani Bunda



KIKAO cha wazazi katika shule ya sekondari Kibara, iliyoko wilayani Bunda, mkoani Mara, kimepitisha maazimio kadhaa, ili shule hiyo iendelee kutoa elimu bora kwa wanafunzi na kufanya vizuri kitaaluma mara kwa mara.
Katika taarifa ya kikao hicho iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na mkurugenzi wa shule hiyo Mtamwega Mgaywa amesema kuwa kikao cha wazazi wa wanafuzi wanaosoma katika shule hiyo kimeketi desema 22 mwaka huu.
Amesema kuwa katika kikao hicho wazazi wamezungumzia changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo, ili kuzirekebisha na kuleta ufanisi zaidi, ili wanafunzi waendelee kupata elimu iliyo bora zaidi.
Mgaywa ameyataja baadhi ya maazimio ya wazazi hao kuwa ni pamoja na mtu yeyote kutokuifunga shule hiyo, bila kushirikisha wazazi wenye watoto na bodi ya shule na kwamba pia shule hiyo isiingiliwe na mtu yeyote, wanasiasa wala maslahi ya kisiasa, na badala yake ibaki na masuala ya elimu tu.
Ameyataja maazimio mengine kuwa ni migogoro yoyote ipelekwe kwenye bodi ya shule na ikishindikana ipelekwe kwenye vyombo vya sheria, ambapo jingine ni kama kuna madai yoyote yafuate utaratibu wa kazi na siyo vinginevyo.
Katika kikao hicho pia wazazi wameazimia mkuu wa shule hiyo afanye marekebisho ya ajira na azingatie mwenye sifa ya taaluma ya elimu, ikiwa ni pamoja na kuboresha uongozi wa shule na kwamba pia kitafanyika kikao cha wazazi na bodi hapo Januari 3, mwakani, ili kuweka mikakati mingine ya kimaendeleo zaidi.

Kijana mwenye umri wa miaka 24 amehukumiwa miaka 30 kwenda jela kwa kosa la kubaka Wilayani Bunda



Mahakama ya wilaya ya Bunda MkoaniMara , Desemba 27  2017 imemuhukumu kifungo cha miaka 30 jela Baraka saimon 24 mkazi wa kijiji cha Muranda kata ya Namuhura kwa kosa la kubaka  na kumpa mimba mwanafunzi  mwenye umri wa miaka 16 . 

Akisoma shtaka mbele ya hakimu mkaazi wa mahakama ya wilaya ya bunda Jacklin J. Rugemalira , mwendesha mashtaka upande wa jamhuri inspecta Masoud ameeleza mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo mnamo tarehe 19.oktoba.2017 saa za jioni.

Aidha amesema kuwa majira hayo mtuhumiwa alimbaka msachana huyo mwenye miaka 16 anaesoma katika shule moja ya sekondari.

Hata hivyo alipoulizwa kuhusu makosa hayo mshtakiwa amekiri kutenda kosa hilo na ndipo mheshimiwa hakimu amemhukumu kifungo hicho cha miaka 30 jela.

Sunday, 24 December 2017

Wafugaji wa Kata ya Bunda stoo wako vizuri katika kutekeleza maagizo ya serikali

Jumla ya ng’ombe 7485 katika kata ya bunda stoo katika halmashauri ya mji wa bunda  imesajiliwa ikiwa ni sambamba na uwekaji  chapa zoezi lililochukua siku 10 kukamilika.

Zoezi hilo la uwekaji chapa kwa mifugo lilianzia katika kijiji cha butakale.

Akisoma taarifa fupi ya mifugo mbela ya mkuu wa wilaya ya Bunda, mtendaji wa kata hiyo bwana  Raymond Bukombe amesema kuwa kata hiyo inajumla ya mifugo 27485 na yote imesajiliwa.


Hata hivyo mkuu wa wilaya ya bunda Mwalimu Lydia Bupilipili amewapongeza wafugaji wa kata ya bunda stoo kwa kuhamasika kepeleka mifugo yao kuwekewa chapa na kusajiliwa kwa kuwa zoezi hilo ni la kitaifa na ni muhimu kwani inapunguza baadhi ya changamoto ikiwemo wizi wa mifugo

Wazazi Wilayani Bunda watakiwa kula sahani moja na watoto wao waliohitimu kidato cha nne hadi matokeo yatoke

Baada ya wanafunzi wa kidato cha nne kote  nchini  kumaliza mtihani wao mnamo mwezi wa 11   mwaka huu, wazazi na walezi wa watoto hao wametakiwa kuendelea na ushirikiano ule ule wa kuwalea watoto hao katika maadili mema.

Hayo yamesemwa na  baadhi ya wakazi wa kata ya kabarimu  halmashauri ya mji wa bunda kwa nyakati tofauti ambapo wamesema kuwa wapo baadhi ya wazazi hujisahau kuwapa malezi mazuri watoto hao na kuwaacha wakifanya mambo yasiyo yakimaadili kama kujihusisha na vitendo vya ngono.


Mmoja wa wakazi hao bwana Thomas Ezekil amesema kuwa wazazi wanapaswa kutambua kwamba watoto hao bado ni wanafunzi na wanasubiri matokeo yao ili waendelee na masoma yao.

Vijana wilayani Bunda waaswa kuchapa kazi

Vijana katika Halmashauri ya Mji wa Bunda Mkoani Mara wameombwa kutambua kuwa wao ni nguvu kazi ya taifa siku zote, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa bidii bila kubagua kazi, ili kuweza kuleta maendeleo katika jamii na taifa kwa ujumla.

Ushauri huo umetolewa baadhi ya vijana wa mtaa wa wa bank wakati wakizungumza na redio mazingira hii leo.

James Juma pamoja na Naomi Kulwa Wamesema vijana wasipojituma kufanya kazi kwa bidii kauli ya kusema  vijana ni nguvu kazi ya taifa itabaki midomoni mwa watu bila vitendo vyovyote, hivyo ni wakati wakujituma ili kauli hiyo iwe kwa vitendo.


Katika hatua nyingine vijana hao wameiomba halmashauri ya mji wa Bunda, kuwajali vijana katika upande wa asilimia iliyotengwa na serikali ili kuweza kusaidia katika majukumu yao ya kujituma.   

Mgambo wapongezwa na mkuu wa wilaya ya Bunda kwa kujitokeza kwao kwenye mafunzo

Mkuu wa wilaya ya Bunda Mkoani Mara mwl.Lydia Bupilipili amewapongeza wale wote waliojitokeza miaka ya nyuma kushiriki mafunzo ya mgambo, kwani wamekuwa msaada mkubwa ndani ya jamii katika utekelezaji wa majukumu ya ujenzi wa taifa.

Bulipili ametoa Pongezi hizo siku chache baada ya wanamgambo 166 kuchukuliwa na Suma jkt, kwajili ya kwenda kulinda katika makampuni  mbalimbali hapa nchini.

Aidha Bulipili amesema kuwa, vijana waendelee kujitokeza kwa wingi kushiriki mgambo kwani serikali ya wilayani Bunda imedhamilia kumaliza kero mbalimbali likiwemo suala la ajira. 

Hata hivyo Bupilipili  amesema mngambo ni kitu muhimu sana na sio cha kubezwa hata mara moja hivyo vijana wasione aibu kushiriki kwa asilimia mia moja.




Saturday, 23 December 2017

Jeshi la Polisi Wilayani Bunda limetolea ufafanuzi tukio la ajali ya moto iliyotokea hivi karibuni

Imeelezwa kuwa ajali ya moto iliyotokea hivi karibuni katika Mtaa wa Sabasaba Kata ya Bunda Mjini Halmashauri ya mji wa Bunda Mkoani Mara na kusababisha kuungua kwa maduka mawili inasadikika kuwa chanzo cha ajali hiyo ni shoti ya umeme.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari kuhusu tukio hilo Mkuu wa kituo cha polisi wilaya ya Bunda OCD Jeremiah Shila amesema kuwa kwa uchungzi wa awali wakishirikiana na Tanesco wameweza kubaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni shoti ya umeme iliyojitokeza katika moja ya maduka yaliyoungua.

Shila amesema bado wanaendelea kufanya uchunguzi zaidi ili waweze kubaini kisa kamili cha ajali hiyo.

Aidha Shila amesema kwa ushirikiano mzuri wa wananchi pamoja na Jeshi la polisi waliweza kuuzima moto huo licha ya kuwepo kwa changamoto ya gari la zima moto katika Wilaya Bunda.

Hata hivyo Shila ametoa wito kwa Wananchi wa wilaya ya Bunda kuwa wangalifu na umeme ikiwa ni pamoja na kuacha kupikia kwenye vibanda.


Ajali ya moto ilitokea mnamo tarehe 18.12.2017 majira ya saa tatu usiku katika mtaa wa sabasaba maeneo ya maduka ya wauza mitumba karibu na mlango wa kuingia soko kuu la mjini Bunda.

Wazazi katika mji wa Bunda washauriwa kuwekeza kwa Vijana wao kupitia ufundi

Wazazi na walezi katika halmashauri ya mji wa Bunda Mkoa wa Mara,wameaswa kuwafundisha vijana wao kazi za mikono za kujiajiri ili waweze kujikimu pindi wakati ukifika wa kujitengemea wasipate shida.

Hayo yamesemwa na Bwile Chisumu mkazi wa kata ya kabarimu mjini hapa wakati akizungumza na radio Mazingira fm  ambaye anajishughurisha na useremala na kueleza kuwa endapo wazazi wakianza kuwafundisha vijana wao kazi za ufundi itawasaidia pindi wakijitegemea na kuacha kutegemea kusubili ajira kutoka serikalini.


Chisumu ameongeza kuwa imefika wakati sasa kwa kila mwananchi kutambua kuwa kufanya kazi ni muhimu kwa kila mtu  na kutochagua wala kuidharau kazi kwa misingi fulangi kwani kazi nzuri ni yeyote inayokupatia kipato halali. 

Wananchi wa mji wa Bunda wamempongeza Mkuu wa Wilaya kwa Hatua anazo zichukuwa.

Siku chache baada ya mkuu wa wilaya ya Bunda Mwl.Lydia Bupilipili kumuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Bunda Janeth Mayanja kuhakikisha ana wasimamia wahusika wote wa mipango miji ili waweze kuboresha na kusitisha uwanzishwaji wa masoko kila sehemu bila utaratibu,wananchi wa mji wa bunda wampogeza mkuu wa wilaya kwa hatua hiyo huku wakisema ofisi ya mipango miji imejisahau katika utekelezaji wa majuku yao.

Wakizungumza na mazingira fm kwa nyakati tofauti  baadhi ya wananchi hao wamesema kuwa wamefikia hatua ya kuanzisha masoko kiholela pasipo mpangilio kwa sababu hawaoni watu wakuwaelekeza juu ya upangiliaji wa mji hivyo kupelekea kukosesha mapato ndani halmashauri na serikali kiujumla kwa sababu ya watu wachache.


Hata hivyo wananchi hao wamesema kuwa pindi wataalam hao wataanza kuchukua hatua juu ya suala hilo wasiyafute masoko hao bali watoe utaatibu ili kama kuanza kutoa ushuru watu wapo tayari kufanya hivyo lakini siyo kuyafuta kabisa.

Barabara bado ni changamoto katika kijiji cha Ruamkoma Wilayani Butiama


Wananchi wa kijiji cha  Ruamkoma kata ya Butiama Wilaya ya Butiama  mkoani  Mara wameiomba serikali kuwaboreshea miundombinu ya barabara katika kijiji hicho kwani wamekuwa wakishidwa kufanya shughuli za kimaendeleo katika kijiji hicho.

Hayo yamesemwa na wananchi wa kijiji wa ruamkoma wakati wakizungumza na mazingira fm kwa nyakati tofauti.

Mwikwabe Marwa ambae ni miongoni mwa wananchi hoa amesema kuwa wamekuwa wakipata shida kubwa ya kusafirisha bidhaa zao za biashara kutokana na ubovu wa barabara zilizopo katika kata hiyo na kuwalazimu kutumia gharama kubwa wakati wanapokuwa wanasafirisha bidhaa zao.


Aidha wamesema changamoto zingine wanazokumbana nazo ni pamoja na maji, umeme, na upungufu wa vyumba vya madarasa ya shule ya msingi na kuomba serikali kuwapelekea huduma hizo.

Mabwana Afya wanahitajika katika kijiji cha Sarama A wilaya ya Bunda

Wakazi wa kitongoji cha Mumwaro kijiji cha Sarama A wilaya ya Bunda Mkoani  Mara wameiomba serikali kuwapelekea mabwana afya katika kitongoji hicho ili waweze kuondokana na uchafunzi wa mazingira kwa kujisaidia ovyo aja kubwa na ndogo katika vichaka.

Kauli hiyo imetolewa na wananchi wa kitongoji hicho walipokuwa wakizungumza na mazingira fm.

Wambura kigunya ambaye ni miongoni mwa wakazi wa kitongoji hicho amesema kuwa wakazi wa kitongoji hicho walio wengi hawana vyoo kitendo kinacho wapelekea kujisaidia vichakani bila kujua ni hatari kwa afya ya zao.

Amesema kuwa ni vizuri kama serikali ya kitongoji ita kuwa na utaratibu wa kupita kila mji na kukagua kama kunachoo ili kuweza kunusuru afya za wakazi wa kitongoji hicho pia kuepuka magojwa ya mlipuko kama vile kipindupindu na kuhara.

Hata hivyo  wameomba uongozi wa kitongoji hicho kuwachukulia hatua  za kisheria wale wote watakao bainika hawana choo katika miji yao ili iwe fundisho kwa wengine.


Thursday, 21 December 2017

Hizi ni salamu tosha kwa wahalifu wilayani Bunda katika musimu huu wa sikukuu

Jeshi la polisi wilayani Bunda Mkoani Mara limewahakikishia wananchi kuwa watasherekea sikukuu kwa amani na utulivu kwani wamejipanga kikamilrifu kukabiliana na wahalifu watakao taka kuchafua hali ya hewa katika musimu huu wa sikukuu.
Akizungumza kupitia kipindi cha Asubuhi leo kinachorushwa na kituo hiki Mkuu wa polisi Bunda kamanda Jeremiah Shila amesema wao kazi yao ni kuhakikisha wanalinda raia na mali zake hivyo katika musimu huu wa sikukuu wako makini sana katika suala la ulinzi kaika maeneo yote ya Wilaya ya Bunda lengo ni wananchi kuwa salama wakati wote.
OCD Shila amewatumia salama waharifu wote wanaopanga kuja kufanya uhalifu katika wilaya ya Bunda kuwa hata wasipoteze muda maana wao wamejiandaa kikamilifu.

OCD Shila pia amezungumzia suala la ulinzi na usalama Wilaya ya Bunda kufuati matukio mbalimbali kutokea hivi karibuni ikiwemo ya ukatili wa kijinsia yaliyojitokeza katika maeneo tofauti ndani ya wilaya ya Bunda na kusema kuwa wanayafanyia kazi matukio yote yaliojitokeza na kuomba wananchi kutochoka pindi polisi wanapotaka ushirikiano kutoka kwao.

Zao la Pamba Wilayani Bunda la wekewa mpango kazi wa kueleweka

Zao la pamba limesisitizwa sana na serikali kuhakikisha katika mikoa inayolima zao hilo linaongeza uzalishaji kwa kiwango kikubwa.

Katika Wilaya ya Bunda Mkoani Mara kupitia Mkuu wake wa Wilaya mwl. Lydia Bupilipili aliagiza kila mwananchi alime hekar mbili huku akiagiza shule zote msingi na sekondari kuwa na shamba la pamba, mbali na hivyo aliagiza Halmashauri zote Wilaya na Mji ziwe na shamba darasa .

Katika kutaka kujuwa zaidi hatua zilizofikiwa kupitia agizo la Mkuu wa Wilaya tumemtafuta Mkaguzi na Mratibu wa zao la Pamba wilaya ya bunda bwana liberatus soka amesema kuwa

Hatua iliyofikiwa ni nzuri kwa sababu asilimia kubwa walegwa wametekeleza agizo la Mkuu wetu wa wilaya kwahiyo tunatarajia mambo mazuri katika musimu huu wa kilimo hasa kilimo cha zao la Pamba’alisema Soka

Suala la Pembejeo feki wilayani Bunda kupatiwa majawabu.

Taasisi za serikali pamoja na taasisi Binafsi katika Wilaya ya Bunda Mkoani Mara wametakiwa kusimamia ipasavyo suala la pembejeo zinazotakiwa kuwafikia wa wakulima ili kuwawezesha kulima kilimo bora na sio bora kilimo.

Agizo hilo limetolewa Jana na Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mwalimu Lydia Bupilipili wakati akifungua wa mdahalo kuhusu Pembejeo feki Wilayani Bunda ulioandaliwa na Baraza la kilimo na mifugo Tanzania |Agricultural Council of Tanzania ] katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji wa Bunda.

Bupilipili amesema Taasisi zinazohusika na usimamizi wa pembejeo wasipokuwa makini siku zote wataendelea kutiwa doa na wale wasiowatakia meme katika kazi yao hivyo amewataka kuamka nakuona sasa si muda wakufumbia macho masuala kama hayo.

Bupilipili amesema Wilaya ya Bunda inaongoza kwa pembejeo feki hivyo kuna kila sababu ya kuwa makini na watu wasio takia mema taifa lao kupitia kusambaza pembejeo feki kwa wakulima.


Bwana Khalid Ngassa kutoka Baraza La kilimo na mifugo Tanzania kwa upande wake amesema kuwa wakulima wanapata hasara kubwa na wanaumia sana kupitia pembejeo feki wanazopokea kutoka kwa wasambazaji hali ambayop inapelekea wakulima kukata tamaa na kilimo hivyo ameshauri wakulima nao wawe makini na pembejeo hizo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa mapema kama wakigundua kunadosari popote.

Kwa upande wao wakulima wa Wilaya Bunda wamekubalia kwa kauli moja ya kufuata ushauri waliopewa ikiwa ni pamoja na kusema pale ambapo kuna kasoro ili wawahi kusaidiwa tatizo hilo.