Wananchi wa Kyanyari Butiama walazimika kulala mapema baada ya tukio la mauaji ya watu wanne - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Thursday 1 June 2023

Wananchi wa Kyanyari Butiama walazimika kulala mapema baada ya tukio la mauaji ya watu wanne

 

Wananchi wakiwa katika mkutano wa hadhara na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi

Kufuatia tukio la mauaji ya watu wanne katika kijiji cha Nyakiswa kata ya Kyanyari Wilaya ya Butiama wananchi wa maeneo hayo wameanza kuishi na hofu kwa kulala mapema na kuingia na makopo ndani kwa ajili ya kujisaidia.

Hayo yamebainishwa jana tarehe 31 May 2023 kupitia mkutano wao na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh Jumanne Sagini katika viwanja vya Mwibagi Stooni alipofika kufanya kuzungumza kuhusu hali ya ulinzi na usalama kufuatia tukio hilo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupewa nafasi kupitia mkutano huo baadhi wameendelea kuonesha wasiwasi wao kuhusu hali ya ulinzi na usalama huku wakibainisha kuwa kwa sasa wanalazimika kulala mapema wakihofia usalama wao.

"Sisi watu wa mkoa wa Mara kuingia ndani na kopo kwa ajili ya kujisaidia ni mwiko kwetu lakini kwa hili la juzi nina kuhakikishia kabisa kuna wanaume tunaingia na makopo tunajisaidia ndani...Ukifika hapa saa moja utakuta hamna bodaboda hata mmoja, kama hali ni shwari hao boda wanaogopa kwanini...' mkazi wa Kyanyari Butiama


Aidha wameiomba serikali kupitia jeshi la polisi kuimarisha doria katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na kujengewe kituo cha polisi na kuongeza jitihada za kuwasaka wote waliohusika na mauaji hayo.
Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizoibuliwa kupitia mkutano huo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara Kamishina Msaidizi ACP Salum Ramadhani Morcase  amesema polisi imeendelea kuimarisha doria ikiwa ni pamoja na kuwasaka wale wote waliohusika na tukio hilo huku akiwasihi wananchi kufuata sheria na kuimarisha ulinzi katika maeneo yao kwa kushirikiana na jeshi la polisi.

Kamishina Msaidizi wa Polisi ACP Salum Ramadhani Morcase, RPC Mkoa wa Mara.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo la Butiama, Mh Jumanne Sagini amewaondoa hofu wananchi hao huku akieleza mikakati mbalimbali iliyowekwa na serikali katika kuimarisha usalama huku akitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kutokomeza vitendo hivyo.

Mh Jumanne Sagini akizungumza katika mkutano na wananchi wa kata ya Kyanyari ButiamaNo comments:

Post a Comment