Asimulia maneno ya mwisho ya mumewe masaa machache kabla ya kuuawa na mwili wake kutelekezwa porini. - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Friday 2 June 2023

Asimulia maneno ya mwisho ya mumewe masaa machache kabla ya kuuawa na mwili wake kutelekezwa porini.

 

Namjungu Aloyce, mke wa Kalebu Dinda 'Otike' bodaboda aliyeuawa katika kijiji cha Nyakiswa kata ya Kyanyari Wilaya ya Butiama akisimulia hali ilivyokuwa

Namjungu Aloyce ni mwanamke aliyepoteza mumewe katika tukio la mauaji ya watu wanne lililotokea tarehe 27 May 2023 Usiku katika kijiji Cha Nyakiswa kata ya Kyanyari Wilaya ya Butiama Mkoani Mara.


Ndoto ya maisha marefu na mumewe iliishia usiku huo wa tarehe 27 wakiwa wameishi kwa takribani miaka 11 na kifanikiwa kupata watoto jumla ya watoto 5 wa kiume wanne na wakike mmoja wa kwanza akiwa na miaka sita.


Ni kwa kazi hiyo hiyo ya bodaboda ndio ilikuwa tegemeo la familia lakini katika usiku wa siku hiyo ndoto za familia zinapotea baada ya kupigiwa simu kuwa walichoweza kukiona ni ndala peke yake zikiwa zimetelekezwa kando ya barabara kabla ya masaa machache kutaarifiwa kuwa "Kalebu Dinda" amepatikana akiwa ameuawa.


"Nikiwa nimelala kama saa tano hivi alikuja mke wa shemeji yangu akanigongea mlango nilipofungua akaniuliza mumeo yuko wapi..nikamjibu sijui alipoondoka hapa ameniacha nimebandika 'fugo' (sufuria ya kupikia ugali) hadi sasa hivi sijamuona"


"Nilianza kumpigia simu ikawa inaita lakini hapokei nikahisi huenda yuko kwenye pikipiki hawezi kupokea kama ilivyo kawaida yake anapokuwa anaendesha...hadi baadaye alipotaarifiwa kuwa amepatikana akiwa ameuawa na mwili wake kutelekezwa kwenye shamba la mahindi"


Hii imeibua msiba mkubwa katika familia kwa baba ambaye hakupata hata sekunde ya kusema neno la mwisho kwa familia yake isipokuwa yale waliozungumza naye jioni kabla ya kuuawa.


Namjungu anasema mumewe alikwenda nyumbani kuwajulia hali ambapo mwanaye mkubwa alimweleza kuwa anaumwa ndipo 'Otike' akatoa maelekezo kwa mama yao ili kumnunulia dawa kutoka kwenye chenji iliyokuwa imebaki lakini alijibiwa kuwa imetumika kwenye mambo mengine.


Akiwa anatafakari namna ya kupata dawa kwa wakati kutokana na uhaba wa maduka ya dawa katika maeneo hayo aliondoka katika ishara ya kuendelea na kazi ya kutafuta mkate wa kila siku huku akiacha neno la matumaini kwa familia yake kuwa anapambania mahitaji yao.


"Akasema huko ninakokwenda hamna dawa laakini mtoto akamkandamizia kuwa baba kaninunulie dawa...alivyomwambia hivyo akaondoka akapandisha juu..." anasimulia Namjungu


Hiyo ndio ilikuwa mara yake ya mwisho kuongea na familia yake na kama Mungu angewafunulia kile ambacho kitafuata baada ya hapo huende wangemwambia maneno mazito yale yanayochemsha mioyo yao kwa sasa.  


Akizungumza na Mazingira Fm anasema majira ya saa 5 usiku aligongewa mlango na ndugu zake wakimuuliza iwapo ana taarifa zozote kuhusu mumewe ndipo walipomwambia kuna taarifa za bodaboda kuvamiwa barabarani lakini mpaka wakati huo walikuwa wamefanikiwa kupata pikipiki ikiwa imetelekezwa barabarani na ndala nyeusi ambazo alithibitisha kuwa ni za mumewe.


Katika tukio hili vyombo vya dola vinaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwasaka waliohusika na mauaji hayo lakini kwa upande wa Namjungu anafikiria zaidi kuhusu hatima ya watoto wake ikiwa hakuwa na shughuli yoyote mbali na kilimo kwa ajili ya kujikimu kwa chakula.


Hivyo anatamani kuona sambamba na juhudi za kuimarisha ulinzi zinazofanywa na vyombo vya dola anatamani pia kuona ni kwa namna gani suala la malezi ya watoto linaangaliwa.


"Ninaomba mnisaidie kuwatafuta yaani hata kama ni kunyongwa na wenyewe kwasababu na wenyewe wameniumiza sana....ameniachia watoto wadogo..." anasimulia Namjungu kisha anahitimisha kwa kilio cha uchungu. 


Katika tukio hilo watu watatu waliouawa akiwemo mume wa Namjungu (Kalebu Dinda au Otike) walikuwa ni waendesha bodaboda ambao tayari mazishi yao yamefanyika na pikipiki zao zilipatikana katika maeneo ya tukio huku mtu wa nne akiwa bado hajatambulika na mwili wake umehifadhiwa Hospitali ya Butiama.

No comments:

Post a Comment