Friday, 26 January 2018

Hatua za haraka zaanza kuchukuliwa kuondoa adha ya ukosefu wa choo Shule ya Bunda




Wanafunzi,Waalimu pamoja na wakazi wanaofanya shughuli zao katika shule ya Msingi Bunda halmashauri ya mji wa Bunda Mkoani Mara wako hatarini kupatwa na Magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu kutokana na shule hiyo kukosa choo jambo linalowalazimu wanafunzi pamoja na walimu kujisaidia mlimani.

Taarifa zinaeleza kwamba wanafunzi wa darasa la awali yaani chekechea,la kwanza, la pili na hata madarasa mengine baadhi yao hulazimika kuchimba mchanga kwa mikono katika eneo la uwanja wa mpira wa miguu shuleni hapo kisha hujisaidia haja kubwa na baadae huyafunika.

Alipoulizwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji huo Janeth Mayanja amesema kuwa suala hilo la ukosefu analitambua na tayari wameanza kulishughulikia kwa kujenga choo cha dharura kwa wanafunzi hao ikiwa sambamba na ujenzi wa matundu 16 ya vyoo vya kudumu.

Taarifa kutoka katika shule hiyo zinadai kwamba leo wameanza uchimbaji wa matundu hayo ya vyoo.

Hata hivyo wananchi wameshukuru redio mazingira fm  pamoja na serikali ya mji wa bunda chini ya mkurugenzi wake Janeth Mayanja  kwa hatua alizozichukua katika kunusuru adha hiyo .

Thursday, 25 January 2018

Mkurungezi wa mamlaka ya Maji Bunda BUWASA asimamishwa kazi kupisha uchunguzi dhidi tuhuma zinazomkabili



Imeelezwa kuwa Mkurungezi wa Mamlaka ya maji Bunda BUWASA bwana Mansur Mandemula amesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kufuatia tuhumu zinazomkabili za kuwa na duka la vifaa vya huduma ya maji jambo ambalo ni kinyume.

Akizungumza na radio mazingira fm Kwanjia ya simu Mkuu wa Wilaya Ya Bunda Mwl.Lydia Bupilipili amethibitisha kusimamishwa kwa mkurungezi huyo na kwamba siku ya leo ndiyo amekabidhi ofisi ili kupisha uchunguzi.

Bipilipili amesema tayari bodi ya maji Imevunjwa kutokana na kuwepo kwa taarifa za kumtetea Mkurungezi huyo huku wakishindwa kutimiza wajibu wao kama bodi na badala yake wamesababisha hadi deni limefika milioni mia nne sabini na saba paka sasa hivi.

Aidha Bupilipili amesema kuwa awali aliwaeleza wajumbe wa bodi hiyo kuwa wao wapo kwajili ya wananchi na sio watu wengine na kwamba bodi ilionekana kutokuwa wabunifu katika kazi zao kwa wananchi.

Katika hatua nyingine Bupilipili amesema moja ya agizo la waziri mkuu ni kutuma wataalam kutoka Makao makuu TAMISEMI ili kuja kuchunguza miradi yote ya maji katika Wilaya ya Bunda ambapo tayari wataalam hao wameshafika na tayari wameshaanza kazi kama maagizo yalivyokuwa.

Wednesday, 24 January 2018

Mwanakwaya Afariki Kanisani Baada ya Kutoa Sadaka

Mwanakwaya wa kwaya ya Kanisa Katoliki la Mtakatifu Secilia, Kigango cha Muze Parokia ya Zimba Jimbo la Sumbawanga, Flora Nandi (25), ameanguka na kufariki dunia muda mfupi baada ya kutoa sadaka ya shukrani akiwa kanisani.

Tukio hilo la kifo cha mwanakwaya huyo wa kwaya ya Mtakatifu Secilia lilitokea Jumapili saa 4 asubuhi wakati wa idada ya kwanza.

Akisimulia tukio hilo Katekista wa kanisa aliyekuwa akiongoza ibada hiyo, Philipo Lupadasi, alisema kuwa wanakwaya wakiwa wanaimba na marehemu muda mfupi baada ya Lupadasi kutoka kutoa sadaka ya shukrani na kuendelea kuimba.

Alisema ghafla aliangua chini hali iliyozua mtafaruku na kusababisha ibada kusimama kwa muda mfupi, hali iliyowafanya wanakwaya wenzake kumnyanyua na kumtoa nje ya kanisa, ili pate hewa wakiamini kuwa amepoteza fahamu.

Katekista huyo alisema baada ya kumpepea kwa muda wanakwaya wenzake waliona Flora hapati fahamu, hali iliyowalazimu kumkimbiza katika zahanati ya kijiji cha Muze kwa ajili ya matibabu.

Alisema baada ya kufikishwa katika zahanati hiyo alipokewa na wahudumu wa afya na baada ya kufanyiwa uchunguzi ilibainika kuwa walimpeleka katika zahanati akiwa ameshafariki dunia.

Baada ya kupewa taarifa ya kifo hicho wanakwaya hao waliangua vilio hali iliyosababisha washindwe kurudi kanisani kuimba katika ibada ya pili, hivyo kuuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka nyumbani kwake.

Katekista huyo alifafanua kuwa Flora wakati anafariki dunia alikuwa na ujauzito wa miezi mitano.

Kwa upande wake mwalimu wa kwaya ya Mtakatifu Cecilia, Aloyce Mwandanje, alisema kuwa kifo cha mwanakwaya mwenzao kimewaachia majonzi makubwa, ingawa ni mapenzi ya Mungu.

Alisema mwili wa marehemu ulizikwa Jumatatu katika makaburi ya Kijiji cha Muze.

Monday, 22 January 2018

Majaliwa ahitimisha ziara ya mkoa wa mara.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akikata utepe kuzindua mabweni mawili ya Magufuli na Majaliwa katika Shule ya Sekondari ya Bumagi wilayani Butiama Januari 20, 2018.  Watatu kulia ni mkewe Mary. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiaagana na viongozi wa mkoa wa Mara kwenye uwanja wa ndege wa Musoma baada ya kukamilisha ziara ya siku saba mkoani humo Januari 21, 2017. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Butiama, Nimrod Mkono (katikati) na mkewe Marylouise   Januari 202018,kabla ya kumkabidhi mbunge huyo cheti cha shukurani kilichotolewa na wilaya ya Butiama ili kuthami mchango wake mkubwa wa kujenga na kuchangia maendeleo ya elimu wilayani humo. Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye Chuo Kikuu cha Julius Kambarage Nyerere ambacho kilichojengwa na mbunge huyo kikiwa ni sekondari na kutokana na ubora wake kilibadilishwa kuwa Chuo Kikuu.   (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri mkuu afungua makucha butiama.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Takukuru imkamate na kumhoji meneja wa mkoa wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Peter Salim baada ya kushindwa kutekeleza ujenzi wa mradi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.


Taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Waziri Mkuu imesema mtendaji huyo mkuu wa Serikali alisema licha ya Serikali kutoa Sh600 milioni Aprili mwaka jana kwa ajili ya kuanza ujenzi wa ofisi hizo, hadi sasa hakuna kilichofanyika.


Hata hivyo, meneja huyo katika alisema maelezo yake alieleza kuwa hadi kukamilika ujenzi wa ofisi hiyo utagharimu Sh3 bilioni na kwamba kati ya fedha zilizotolewa na Serikali, Sh400 milioni zimetumika kujengea msingi, kauli ambayo ilipingwa na mkuu wa wilaya hiyo, Anna-Rose Nyamubi.


“Waziri Mkuu si kweli kwamba kuna kazi inayoendelea, bali kilichopo pale ni mashimo ambayo hayajulikani ni ya nini. Pia, kuna jengo moja lilijengwa kwa mabati kama stoo hakuna mafundi wanaoendelea na kazi,” alisema Nyamubi.


Majaliwa alisema Serikali ipo katika mchakato wa kuboresha mazingira ya wafanyakazi, ikiwamo ujenzi wa ofisi za watumishi na kwamba haitamvumilia mtu yeyote atayekwamisha juhudi hizo.


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza kaimu katibu tawala wa Mara, Raphael Nyanda kutuma timu ya wakaguzi kufanya ukaguzi maalumu katika ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.


Alisema halmashauri hiyo imekuwa na tabia ya kutumia fedha za miradi ya maendeleo kwa shughuli nyingine.


Alikuwa akizungumza na watumishi na madiwani wa Butiama katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere.


Pia, Waziri Mkuu aliagiza kuchunguzwa kwa Solomon Ngiliule, ambaye ni mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Masanja Sabuni (mweka hazina) na Robert Makendo (ofisa ununuzi).

Sunday, 21 January 2018

Mwalimu wa Shule ya Msingi Bigutu adakwa na wananchi baada ya kukutwa akiiba vifaa vya ujenzi shuleni Mjini Bunda


 
Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Bigutu katika kata ya Bunda stoo hamashauri ya mji wa Bunda aliyejulikana kwa majina ya Said  MNEMA amekamatwa na wananchi kwa tuhuma za kukutwa Akiiba vifaa vya ujenzi wa shule hiyo vilivyochangwa kwa fedha za Wananchi.


Pendo Maguya ni mwananchi wa kata hiyo aliyeshuhudia mwalimu huyo akiiba sementi hatiamye kutoa taarifa kwa aliyekuwa mwenyekiti wa kitongoji hicho.

Amesema yeye pamoja na mwenzake Anastazia malagira walihisi kuwepo kwa uwizi katika vifaa hivyo vya ujenzi baada ya kuona mtu mmoja ambaye hawakumtaja jina mwenye toroli akisomba saruji kupeleka kwa mwalimu huyo.

Aidha Anastazi Malagira amesema ameshuhudia wizi wa sementi mifuko minne,Nondo na misumari,ambapo ameongeza kuwa walikuwa wanatoka kufata maji ndipo wakaona pikipiki na mtu mwenyetoroli akisimama katika mlango wa ofisi ya mwalimu mkuu na wakaamua kusubiri kuona kinachotoka ndani ya ofisi hiyo na kushuhudaia watu hao wakitoa vifa hivyo.

Naye kwa upande wake Makam mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo ameeleza kwamba amepata taarifa za wizi huo na kufika shuleni hapo ambapo alimkuta aliyekuwa mwenyekiti wa mtaa huo akiwa na mwalimu mkuu na alipomhoji mtuhumiwa huyoa alimweleza kuwa wakae wayamalize.
Hata hivyo Kaimu Afisa elimu wa shule ya msingi halmashauri ya mji huo Hundi Tanga Amesema kuwa amepata taarifa za tukio hilo na kuchukua hatua za kutoa taarifa polisi.

Diwani wa kata hiyo Chiruma Daud Subi ameeleza kwa amepata taarifa hizo na kufika katika eneo la tukio ambapo ameongeza kwamba baada ya ufuatiliaji wameshuudia matofari zaidi ya 300 pia zimehamishwa shuleni hapo na kupelekwa eneo analojenga mwalimu huyo anaetuhumiwa kwa wizi huo.

Hata hivyo Mkurugenzi wa mji wa Bunda Janeth Mayanja amelaani vikali tabia hiyo aliyoionyesha mwalimu huyo na kusema kuwa kwa upande wake atamchukulia hatua za kinidham kwani kitendo alichikifanya kinadidimiza jitihada za wananchi kuunga mkono serikali katika shughuli za kimaendeleo.

Saturday, 20 January 2018

Mkurugenzi Muwasa aingia matatizoni....Ni Baada ya Waziri Mkuu Kumtupa TAKUKURU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameamuru Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mara kumkamata na kumuhoji Mkurugenzi Mtendani wa Mamlaka ya Maji Musoma (Muwasa) Gantala Said kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za mradi wa maji Bunda.

Mbali na mkurugenzi huyo pia ameiagiza Takukuru imuhoji mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Nyakirang'anyi, Mahuza Mumay ambaye ndiye mkandarasi anajenga mradi huo unaotoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenye eneo la Nyabehu hadi Bunda mjini.

Waziri Mkuu amefikia uamuzi huo jana Ijumaa jioni baada ya mkurugenzi huyo kushindwa kueleza kitu kilichosababisha mradi wa maji Bunda kutokamilika  pamoja na Serikali kutoa fedha nyingi.

Akizungumza katika kikao maalumu cha kujadili changamoto za utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Mara, alichokiitisha mjini Bunda, Waziri Mkuu alisema alimua kuitisha kikao hicho baada ya kutoridhishwa na utekelezwaji wa miradi hiyo hususan inayosimamiwa na Muwasa.

Alisema kwa sasa Serikali inatekeleza kampeni ya Rais John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani. Kampeni hiyo  inayolenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, hivyo itawachukulia hatua wote watakaokwamisha miradi ya maji.

Waziri Mkuu alisema malengo ya kampeni hiyo ni kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

Pia Majaliwa aliagiza kupitiwa upya kwa mradi huo   kwa sababu hafurahishwi na ujenzi wake.

“Kama mkurugenzi wa Muwasa anasema mradi umekamilika kwa asilimia 98 sasa kwa nini wananchi walalamikie kukosa huduma hiyo.”

Alisema mkurugenzi huyo amekuwa akimlipa mkandarasi fedha kabla ya kufanya kazi ambapo hadi sasa tayari mkandarasi anayenga mradi huo ameshalipwa zaidi ya Sh 7 bilioni na mradi haujakamilika na wananchi wanaendelea kutumia maji ambayo siyo salama.

Waziri Mkuu alisema viongozi hao wahojiwe na wakibainika kuhusika na ubadhilifuu wa fedha za mradi huo, wachukuliwe hatua kali za kisheria.

“Serikali imedhamiria kuimarisha huduma za maji, hivyo hatuhitaji mtu atakayeenda kinyume na mpango huo.”

Mradi wa kupeleka maji kwenye mji wa Bunda maji kutoka Ziwa Victoria katika eneo la Nyabeho ulisanifiwa mwaka 2006 na ulikuwa unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha za maendeleo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima aliagiza kufungwa na ofisi za Muwasa na kuwataka wafanyakazi wa mamlaka hiyo kutoruhusiwa kuingia ofisini hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamalaka ya Maji Musoma, Mhandisi Said Gantala (kushoto) akitoka kwenye ukumbi wa Balili Rock Resort  mjini Bunda baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuamuru kuwa akamatwe na ahojiwe na TAKUKURU Januari 19, 2018.Kulia ni Kamanda wa TAKUKURU  wa mkoa wa Mara, Alex Kuhanda.

Watumishi na madiwani shirikianeni-majaliwa



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa Halmashauri na Mji wa Bunda pamoja na Madiwani washirikiane katika utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maendeleo.

Pia amewaagiza watumishi wa umma katika halmashauri ya wilaya na mji wa Bunda wafanye kazi kwa bidii na wawahudumie wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana (Ijumaa, Januari 19, 2018) wakati akizungumza na watumishi na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya na wa Halmashauri Mji wa Bunda, katika ukumbi wa Halmashauri ya Bunda.

“Watumishi wa umma  acheni kukaa sana maofisini tengeni muda wa kuwatembelea wananchi katika maeneo yao na shirikianneni nao katika kutatua kero zinazowakabili. Madiwani na watumishi lazima mshirikiane ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Alisema watumishi na madiwani wakishirikiana katika usimamizi wa utekelezaji wa miradi mbalimbali  ya maendeleo, wilaya itafanikiwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Pia Waziri Mkuu aliwasisitiza watumishi hao kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi  na wajiepushe na vitendo vya rushwa, wizi , ufisadi na uzembe kwa sababu vinarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

 Awali, Waziri Mkuu alikagua mradi wa maji wa Bunda na baadae alizindua kikundi cha Ushirika cha Igembe Sabo na kukagua skimu ya umwagiliaji wa zao la mpunga ya Nyatwali wilayani Bunda.

Waziri Mkuu alihitimisha ziara yake wilayani Bunda kwa kuhutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Sabasaba katika mji wa Bunda.

Serikali Yakataza Kulima Pamba kwa Mkataba Wilayani Bunda









WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imekataza kilimo cha pamba cha mkataba kwa sababu kinawanyonya wakulima.

Ameyasema hayo jana (Ijumaa, Januari 19, 2018) wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua zahanati ya Hunyari wilayani Bunda, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mara.

“Ni marufuku kwa wanunuzi wa pamba kulima pamoja na wakulima kwa sababu wakulima wanakosa uamuzi wa kupanga bei. Kuanzia sasa zao hilo litauzwa kwa njia ya mnada.”

Alisema Serikali imeweka mkakati wa kuimarisha mazao makuu ya biashara ambayo uzalishaji wake umeanza kupungua likiwemo na zao la pamba.

Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa kilimo cha zao la pamba kuanzia hatua za maandalizi ya shamba, pembejeo hadi masoko.

Pia Waziri Mkuu amewaagiza Maofisa Kilimo katika wilaya hiyo wawafuate wakulima vijijini kwa ajili ya kutoa elimu itakayowawezesha wakulima kulima kwa kufuata njia bora za kisasa.Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wafugaji kuhakikisha wanakuwa na idadi ya mifugo kulingana na uwezo wa eneo lao.“Marufuku kulisha mifugo katika mashamba ya watu.”

Amesema Serikali itachukua hatua kali za kisheria kwa mfugaji yeyote atakayelisha mifugo yake katika mashamba ya wakulima kwani tabia hiyo huchangia migogo baina yao.