Mahindi ya Bei nafuu bado hayajatibu kilio cha chakula Nyatwali - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Thursday 27 July 2023

Mahindi ya Bei nafuu bado hayajatibu kilio cha chakula Nyatwali

 

Mahindi ya bei nafuu kutoka NFRA yakiwa katika ghala mtaa wa Nyatwali kata ya Nyatwali

Baada ya serikali kuitikia kilio cha wananchi wa Nyatwali kuhitaji kupata mahindi ya bei nafuu, mambo yamekwenda tofauti kilio kimebadilika.

Na Edward Lucas

Baada ya serikali kupeleka huduma ya mahindi ya bei nafuu kwa wananchi wa Nyatwali wilaya ya Bunda, mapya yaibuka ambapo ndani ya wiki mbili ni tani 2.5 tu ndizo zimechukuliwa kati ya tani 30 za mahindi zilizopelekwa katika eneo hilo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Radio Mazingira Fm wananchi hao wamesema kutokana na kusimamishwa shughuli za uzalishaji mali kwa muda mrefu kwasasa wanakosa fedha ya kununua mahitaji mbalimbali kujikimu kimaisha hivyo wanaiomba serikali iwape bure au iwakopeshe mahindi.

Tatu Nyamanda, mkazi wa mtaa wa Nyatwali akizungumza na Mazingira Fm. Picha na Edward Lucas
Sauti za wananchi wa Nyatwali kuhusu suala la mahindi

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Nyatwali, Ramadhani Misongoma amesema kwa kuwa serikali inaendelea na mpango wa kulitwaa eneo hilo na shughuli za maendeleo kwa wananchi zikiwa zimesimamishwa ingependeza wapewe mahindi ya bure ili wajikimu wakisubiri utaratibu wa serikali kuwahamisha.

Sauti ya Ramadhani Misongoma, Mwenyekiti mtaa wa Nyatwali kata ya Nyatwali

Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Tamau, Asafu Ernest Owiti amesema kuwa baada ya kupokea mahindi hayo yanayouzwa shilingi 920 kwa kilo moja na shilingi 3,680 kwa ‘amboni’ moja, kumekuwa na mapokeo tofauti kutoka kwa wananchi.

Amesema kwa wananchi wa mtaa wa Tamau wakipiga na gharama ya usafiri kwenda Nyatwali kilipo kituo cha kuuzia mahindi hayo itagharimu takribani shilingi 5000 kwa thamani ya amboni jambo ambalo wanalazimika kununua katika eneo lao ambapo mahindi ni kati ya shilingi 4000 kwa ambaoni moja.

Asafu Ernesti Owiti, Mwenyekiti mtaa wa Tamau kata ya Nyatwali
Asafu Ernesti Owiti, Mwenyekiti mtaa wa Tamau kata ya Nyatwali akizungumza na Radio Mazingira Fm

Awali akizungumzia hali ya uuzaji wa mahindi katika kituo hicho, Meneja  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA Kanda ya Shinyanga, Revocatus Bisama baada ya kutafutwa na Mazingira Fm kwa njia ya simu amesema baada ya kupokea ombi la mkuu wa Wilaya ya Bunda wamepeleka tani 30 ikiwa lengo ni kupeleka tani 60 lakini hadi kufikia tarehe 25 July 2023 walikuwa wameuza tani 2.5 tu ikiwa ni takribani wiki mbili tangu mahindi yafikishwe katika kituo hicho.

Meneja  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA Kanda ya Shinyanga, Revocatus Bisama

No comments:

Post a Comment