Mhe. Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda akiwa katika mkutano kijiji cha Sarakwa kujadili mikakati ya kukabiliana na wanamapori waharibifu |
Mbunge wa Jimbo la Bunda Mhe. Boniphace Mwita Getere leo amefanikisha ahadi yake ya kuwakutanisha wananchi wa vijiji vinavyopakana na mbuga ya Serengeti, taasisi za uhifadhi na viongozi wa serikali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda ili kujadili na kuweka mikakati ya kusaidia kilio cha wananchi dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Katika mkutano huo uliofanyika katika viwanja vya Shule ya msingi Stephen Wasira kijiji cha Sarakwa kata ya Hunyari ulitoa nafasi kwa wananchi kueleza changamoto mbalimbali, mapendekezo na ushauri huku viongozi wakitumia nafasi hiyo kufafanua baadhi ya hoja na kuelezea mikakati ya kukabiriana na changamoto hizo.
Wananchi wa kijiji cha Sarakwa wakiwasilisha hoja zao kuhusu changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu |
Miongoni mwa hoja za wananchi kuhusu adha ni tembo kuingia katika mashamba na kuharibu mazao yao jambo linalopelekea kukosa uhakika wa chakula na kuwasababishia njaa huku wengine wakipoteza mifugo yao kutokana na uvamizi wa simba, chui na fisi na kubainisha kuwa fedha ya kifuta jasho au machozi haifiki kwa wakati na haitoshi ikilinganishwa na hasara inayosababishwa.
Katika mkutano huo wananchi wameomba kuwekewa kituo karibu cha kukabiliana na wanyama, kuwekewa uzio ili kutenga maeneo ya wananchi na hifadhi huku wakilia na mpango wa kuona gari moja tu ndilo likihudumu katika maeneo mengi ya wilaya ya Bunda jambo linalopelekea kutofika kwa wakati katika matukio.
David Mwakipesile, Meneja wa Idara ya Mawasiliano Grumeti Fund |
"Ni kweli kituo cha Hunyari gari ni moja na ndilo tulilonalo kwa sasa...haya mengine nitayaacha kwa mbunge pamoja na watu wa serikali waangalie kama kutakuwa na uwezekano wa kuongeza gari waongeze lakini sisi kwa uwezo wetu tunalo hilo gari moja ambalo tunamudu kuliendesha" Mwakipesile
Kamishna Msaidizi kutoka TAWA, Said Kabanda |
Akizungumzia mkakati huo, Kamishna Msaidizi TAWA, Said Kabanda amesema jambo la kukabiliana na wanyama waharibifu linahitaji ushirikiano wa wadau wote wakiwemo wananchi na taasisi zingine ili kufanikisha zoezi
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dr Vicent Naano Anney |
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dr Vicent Naano Anney amesema kuhusu changamoto ya upungufu wa gari inaichukua kwenda kuifanyia kazi kwa kuwashirikisha viongozi na wadau wengine ili kuhakikisha yanapatikana magari mengine mawili ili kuondoa kilio hicho kwa wananchi.
Aidha amewatahadharisha wananchi dhidi ya vitendo mbalimbali vinavyoweza kuhatarisha usalama wao hususani vitendo vya kuingia ndani ya hifadhi pasipo utaratibu maalumu.
No comments:
Post a Comment