Monday, 31 July 2023

Utafutaji watu 13 waliozama ziwa Victoria umeendelea leo bila mafanikio

 

Baadhi ya wananchi waliokusanyika kando ya ziwa Victoria eneo la Mchigondo kwa ajili ya zoezi la utafutaji wanaohofiwa kufa maji. Picha na Adelinus Banenwa

Hakuna hata mmoja aliyepatikana hadi kufikia jioni ya leo 31 July 2023 kati ya 13 wanaohofiwa kufa maji eneo la Mchigondo Wilaya ya Bunda baada ya mitumbwi miwili kuzama Ziwa Victoria jana 30 July 2023 majira ya saa 12:30 jioni

Na Adelinus Banenwa na Edward Lucas

Zoezi la utafutaji watu 13 wanaoshukiwa kufa maji Ziwa Victoria katika kijiji cha Mchigondo limeendelea tena leo pasipo mafanikio.
Katika zoezi hilo lililoanza tangu jana 30 July 2023 majira ya saa 12:30 lilipotokea tukio hilo, limeendelea tena leo kwa ushirikiano wa wananchi na kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mara ambapo hadi jioni ya leo 31 July 2023 hakuna hata mtu mmoja aliyepatikana.
Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mara, Augosto Magere ameeleza changamoto wanazokutana nazo katika zoezi hilo ni pamoja na hali ya hewa, kiza kinene na wingi wa tope.

Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mara, Augosto Magere

Tukio hilo la watu kuzama kwenye maji limetokea katika kijiji cha Mchigondo kata ya Igundu Halmashauri ya Wilaya wa Bunda wakati waumini wa Kanisa Takatifu la Mungu la Kiroho KTMK wapatao 28 walilopanda kwenye mitumbwi miwili tofauti kisha kuzama huku watu 14 kunusurika, mtoto mmoja akifariki dunia na wengine 13 hawajulikani walipo.

Walionusurika ajali ya mitumbwi kuzama Bunda wasimulia hali ilivyokuwa

 

Pichani ni Baraka Jumbula wa kwanza kushoto na Joseph Kundi wa pili kulia ambao ni manusura wa ajali ya mitumbwi. Picha na Adelinus Banenwa

Vijana walionusurika kwenye ajali ya mitumbwi eneo la Mchigondo Bunda wasimulia hali ilivyokuwa baada ya mitumbwi kuzama na wao walivyonusurika huku wakiokoa watoto watatu.

Na Adelinus Banenwa na Edward Lucas

Joseph Kundi mkazi wa Bulomba alikuwa ni miongoni mwa wasafiri katika mitumbwi iliyozama ziwa Victoria eneo la Mchigondo Bunda ambaye katika tukio la kuzama anasimulia juhudi alizozifanya za kuogelea na kujaribu kuwaokoa watu waliokuwa wamezama katika mtumbwi wa kwanza kabla ya dakika chache mtumbwi wao pia kuzama.

Anasema wakiwa nyuma waliona mtumbwi wa mbele unazama na watu waliokuwa ndani yake walianza kupiga kelele kuomba msaada ambapo walifanya jitihadi za kuwahi ili kuokoa na waliposogea karibu alijitosa ndani ya maji ili kusaidia hasa watoto waliokuwa wakielea ndani ya maji.

Akiwa katika jitihada hizo kwa kushirikiana na mmoja kati ya vijana waliokuwa wamezama katika mtumbwi huo alifanikiwa kuwaokoa baadhi ya watu na kuwahamishia katika mtumbwi wao lakini dakika chache baadaye mtumbwi wa pili pia ulizidiwa na idadi ya watu na purukushani za watu wengine kujiokoa jambo lililopelekea mtumbwi huo kuzama.

Baada ya mitumbwi yote miwili kuzama Joseph anasimulia zaidi nini kilifanyika ili kujiokoa na kubahatika kuwaokoa watoto wengine watatu kwa kushirikiana na Baraka Jumbula aliyekuwa katika mtumbwi wa kwanza.

Sauti ya Joseph Kundi na Barka Jumbula manusura ajali ya mitumbwi kuzama wakisimulia tukio

Bunda: Watu 13 wahofiwa kufariki dunia Ziwa Victoria

 

Wananchi wakifuatilia zoezi la utafutaji watu 13 ambao wanahofiwa kuzama majini. Picha na Adelinus Banenwa.

Watu 13 wanahofiwa kufariki dunia huku wengine 14 wakinusurika baada ya mitumbwi miwili kuzama Ziwa Victoria wakiwa wanatoka kanisani eneo la Mchigondo kata ya Igundu Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.

Na Adelinus Banenwa na Edward Lucas

Watu 13 wanahofiwa kupoteza maisha na wengine 14 wakinusurika kifo baada ya kuzama ziwa Victoria eneo la Mchigondo kata ya Igundu Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoa wa Mara.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Kijiji cha Igundu, Sumila Nyamkinda Kafumu amesema tukio hilo limetokea jana tarehe 30 July 2023 majira ya saa 12:00 jioni wakati waumini wa Kanisa Takatifu la Mungu la Kiroho (KTMK) wakiwa wanarejea nyumbani baada ya shughuli za kanisa kitongoji cha Mchigondo.

Akizungumza na Mazingira Fm, Kafumu amesema inasadikiwa walikuwa jumla ya watu 28 ambao walipanda mitumbwi miwili tofauti lakini wakiwa safarini mtumbwi wa nyuma ulipata ajali na kuanza kuzama ndipo mtumbwi uliokuwa umetangulia ulirudi ili kutoa msaada lakini ulielemewa baada ya watu wengi kuuvuta kwa nyuma jambo lililopelekea mtumbwi huo pia kuzama.

Sauti ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Igundu, Sumila Nyamkinda Kafumu
Mitumbwi inayotajwa kutumiwa na watu hao wakati wa safari ikiwa imetolewa na kusogezwa ufukweni katika kijiji cha Mchigondo. Picha na Adelinus Banenwa

Baadhi ya viongozi wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dr Vicent Naano leo asubuhi wamefika katika eneo hilo na kuandelea na juhudi za utafutaji ambapo hadi kufikia mida ya mchana zoezi la utafutaji limesitishwa kutokana na hali ya hewa huku wakiweka mipango ya kuendelea na zoezi hilo hapo baadaye kwa ushirikiano wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mara na wanatarajia kupata msaada zaidi kwa kikosi cha Wanamaji kutoka Mwanza ili kuongeza nguvu.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dr Vicent Naano akizungumza kuhusu zoezi la utafutaji

Kwa upande wake mkuu wa polisi kikosi Cha zimamoto na uokoaji Mkoa wa Mara, Augostino Magere amesema tangu walipofika eneo la tukio jitihada za kuwatafuta watu 13 wanaohofiwa kufa maji zimefanyika ambapo hadi saa Saba walikuwa hawajafanikiwa kupata mtu lakini changamoto kubwa katika eneo la uokozi ni kuwa tope jingi

Wachimbaji wadogo wa madini Bunda wafunguka kinachowarudisha nyuma

 

Mchimbaji mdogo wa madini eneo la Nyasana Bunda akiwa katika zoezi la kukamatisha dhahabu kwa kutumia kalai, maji na zebaki (mercury). Picha na Edward Lucas

Na Edward Lucas

Utaratibu wa viongozi, wadau na mamlaka zingine za serikali kujitokeza madini yanapopatikana ikiwa hakuna ushiriki wao katika zoezi la utafutaji na uchimbaji wa madini ni moja kati ya mambo yanayowakwamisha wachimbaji wadogo wa madini.

Hayo yamebainishwa na wachimbaji wadogo wa madini katika eneo la Kazaroho lililopo mtaa wa Nyasana kata ya Kabasa Halmashauri ya Mji wa Bunda wakati wakizungumza na Radio Mazingira Fm katika kipindi cha Duarani.

Mgambi Kebacho Mwita ni mchimbaji na mmiliki wa duara katika eneo hilo amesema alitumia takribani mwaka mmoja kuchimba hadi kuufikia mwamba wa dhahabu kwa kutumia vifaa duni huku akisaidiwa na vijana aliokuwa anawalipa kwa huduma ya chakula kutoka nyumbani

Vijana wakiwa wanatumia njia ya kamba kuvuta mchanga na mawe ya dhahabu kutoka katika duara katika machimbo ya Kazaroho kata ya Kabasa Wilaya ya Bunda. Picha na Edward Lucas
Mgambi Kebacho Mwita akisimulia hali inavyokuwa

Naye Samsoni au maarufu kama Mzee Madevu amesema wengine wanatelekeza maduara kutokana na kukosa uwezo wa kifedha na vifaa duni katika kutambua eneo sahihi la kuchimba hivyo ameiomba serikali kuhakikish inawatembelea wachimbaji wadogo ili kubaini changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi

Samsoni au maarufu kama Mzee Madevu akieleza kuhusu shughuli za uchimbaji katika eneo hilo

Thursday, 27 July 2023

RC Mara: walimu zingatieni sheria sasa hivi dunia ni ya utandawazi

Mkuu wa mkoa wa Mara Said Mohamed Mtanda katika ziara wilayani Bunda, Picha na Thomas Masalu

Walimu zingatieni sheria kwa sasa dunia niyautandawazi watu wanarekodi kila kitu na kutuma kwenye mitandao.

Na Thomas Masalu

Mkuu wa mkoa wa Mara, Mhe Said  Mohamed  Mtanda amewataka walimu kuzingatia Sheria katika utekelezaji wao wa majukumu ili kuondoa migongano na jamii inayowazunguka.

Mhe  Mtanda ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na walimu wa shule ya  Msingi Miembeni A mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na matundu ya vyoo katika shule hiyo, ujenzi huo unatekelezwa kupitia mradi wa BOOST.

Aidha Mhe Mtanda amesema siku hizi mambo mengi yamekuwa wazi na watu wana rekodi kila kitu na kurusha kwenye mitandao hivyo walimu wanajukumu ya kufanya kazi yao kwa weledi mkubwa.

Sauti ya Rc Mara Said Mohamed Mtanda
Mkuu wa mkoa wa Mara Said Mohamed Mtanda katika ziara wilayani Bunda, Picha na Thomas Masalu

Katika hatua nyingine  Mtanda, akiwa shule ya Msingi Mazoezi amewakumbusha wanafunzi kuacha mara moja tabia ya kupokea zawadi njiani maana siku hizi matukio ya ukatili yamekuwa mengi kwa watoto.

Ameongeza kuwa  wanafunzi wanapaswa kutoa taarifa kwa mwalimu mkuu pale wanapoona dalili ya kutaka kufanyiwa ukatili ili hatua zichukuliwe dhidi ya yule anayetaka kufanya tukio hilo.

Sauti ya Rc Mara Said Mohamed Mtanda

Mahindi ya Bei nafuu bado hayajatibu kilio cha chakula Nyatwali

 

Mahindi ya bei nafuu kutoka NFRA yakiwa katika ghala mtaa wa Nyatwali kata ya Nyatwali

Baada ya serikali kuitikia kilio cha wananchi wa Nyatwali kuhitaji kupata mahindi ya bei nafuu, mambo yamekwenda tofauti kilio kimebadilika.

Na Edward Lucas

Baada ya serikali kupeleka huduma ya mahindi ya bei nafuu kwa wananchi wa Nyatwali wilaya ya Bunda, mapya yaibuka ambapo ndani ya wiki mbili ni tani 2.5 tu ndizo zimechukuliwa kati ya tani 30 za mahindi zilizopelekwa katika eneo hilo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Radio Mazingira Fm wananchi hao wamesema kutokana na kusimamishwa shughuli za uzalishaji mali kwa muda mrefu kwasasa wanakosa fedha ya kununua mahitaji mbalimbali kujikimu kimaisha hivyo wanaiomba serikali iwape bure au iwakopeshe mahindi.

Tatu Nyamanda, mkazi wa mtaa wa Nyatwali akizungumza na Mazingira Fm. Picha na Edward Lucas
Sauti za wananchi wa Nyatwali kuhusu suala la mahindi

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Nyatwali, Ramadhani Misongoma amesema kwa kuwa serikali inaendelea na mpango wa kulitwaa eneo hilo na shughuli za maendeleo kwa wananchi zikiwa zimesimamishwa ingependeza wapewe mahindi ya bure ili wajikimu wakisubiri utaratibu wa serikali kuwahamisha.

Sauti ya Ramadhani Misongoma, Mwenyekiti mtaa wa Nyatwali kata ya Nyatwali

Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Tamau, Asafu Ernest Owiti amesema kuwa baada ya kupokea mahindi hayo yanayouzwa shilingi 920 kwa kilo moja na shilingi 3,680 kwa ‘amboni’ moja, kumekuwa na mapokeo tofauti kutoka kwa wananchi.

Amesema kwa wananchi wa mtaa wa Tamau wakipiga na gharama ya usafiri kwenda Nyatwali kilipo kituo cha kuuzia mahindi hayo itagharimu takribani shilingi 5000 kwa thamani ya amboni jambo ambalo wanalazimika kununua katika eneo lao ambapo mahindi ni kati ya shilingi 4000 kwa ambaoni moja.

Asafu Ernesti Owiti, Mwenyekiti mtaa wa Tamau kata ya Nyatwali
Asafu Ernesti Owiti, Mwenyekiti mtaa wa Tamau kata ya Nyatwali akizungumza na Radio Mazingira Fm

Awali akizungumzia hali ya uuzaji wa mahindi katika kituo hicho, Meneja  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA Kanda ya Shinyanga, Revocatus Bisama baada ya kutafutwa na Mazingira Fm kwa njia ya simu amesema baada ya kupokea ombi la mkuu wa Wilaya ya Bunda wamepeleka tani 30 ikiwa lengo ni kupeleka tani 60 lakini hadi kufikia tarehe 25 July 2023 walikuwa wameuza tani 2.5 tu ikiwa ni takribani wiki mbili tangu mahindi yafikishwe katika kituo hicho.

Meneja  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA Kanda ya Shinyanga, Revocatus Bisama

Sunday, 23 July 2023

Mazingira Fm yatoa mshindi tuzo za EJAT 2022


Catherine Msafiri Madabuke mtangazaji radio Mazingira na mshindi wa tuzo ya Umahiri katika kipengere cha utalii na uifadhi. Picha kutoka mtandaoni

Radio Mazingira Fm imefanikiwa kumtoa mshindi wa tuzo za EJAT zinazotolewa na baraza la habari Tanzania MCT ambaye ni Catherine Msafiri Mdabuke.

Na Adelinus Banenwa

Catherine Msafiri Madabuke mtangazaji kutoka radio Mazingira fm ameibuka mshindi wa umahiri wa uandishi wa habari katika kipengere cha utalii na uhifadhi tuzo za EJAT 2022.

Tuzo hizo zinazotolewa na baraza la habari Tanzania MCT kwa waandishi wa habari mahiri ambapo tuzo za mwaka 2022 zimetolewa usiku wa tarehe 22 july 2023 katika ukumbi wa mlimani city Dar es salaam.

Akitangazwa mshindi

Ikumbukwe kwamba ni kwa mara ya pili Radio mazingira fm inatoa mshindi wa umahiri wa buandishi wa habari katika tuzo hizi amabapo mwaka 2020 Thomas Masalu mtangazaji wa mazingira fm aliibuka mshindi wa tuzo hii ya umahiri wa uandishi wa habari katika kipengere cha utalii na uhifadhi

Kwa niaba ya uongozi wa radio Mazingira Fm inampongeza Catherine Msafiri Madabuke kuibuka mshindi katika tuzo hizo.

Gari lililobeba mashabiki wa yanga laua na kujeruhi Bunda

 

Mashabiki wa club ya yanga wamesherekea kilele cha siku ya mwananchi kwa masikitiko baada ya miongoni mwa gari lililokuwa limebeba mashabiki wa timu hiyo mjini Bunda kupata ajali iliyosababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi wengine 14.

Na Adelinus Banenwa

Watu wawili wamepoteza maisha na wengine 14 kujeruhiwa katika ajali ya gari la mashabiki wa Club ya Yanga wakati wakitoka kuwa karimu wagonjwa hospitali ya Manyamanyama katika siku ya mwananchi.

Tukio hilo limetokea 22 july 2023 hatua chache kutoka viunga vya hospitali ya Manyamanyama baada ya msafara huo wa mashabiki kumaliza kuwasalimia wagonjwa.

Dkt  Deus Nasoro mganga mfawidhi hospitali ya Manyamanyama ameiambia mazingira fm kuwa hospitali hiyo imepokea miili ya watoto wanaokadiriwa kuwa na kati ya miaka 9 hadi 10 na majeruhi 14 waliotokana na ajali hiyo.

Aidha dkt Deus amesema majeruhi hao 14 kati yao wana majeraha ya kawaida na wengine wanaendeleana matibabu.

Dkt  Deus Nasoro mganga mfawidhi hospitali ya Manyamanyama

Kwa upande wa mashuhuda wa tukio hilo wamesema chanzo cha ajali watu kuwa wengi kwenye hilo gari na kuegemea upande mmoja jambo lililopelekea dereva kushindwa kulimudu gario hilo.

Sauti ya shuhuda wa tukio hilo

Friday, 21 July 2023

Watumishi idara ya afya wanusurika kifo gari likiteketea kwa moto Bunda

Gari la idara ya afya lililoteketea kwa moto. Picha na Adelinus Banenwa

Watumishi wanne wa idara ya afya pamoja na dereva wao wamenusurika kifo baada ya gari lao kuwaka moto wakati wanatoka kutoa huduma ya uzazi wa mpango mtaa wa Kinyambwiga kata ya Guta Halmashauri ya Bunda Mjini

Na Adelinus Banenwa

Watumishi wanne wa idara ya afya kutoka Musoma na Bunda pamoja na dereva wao wamenusurika kifo baada ya gari lao kuwaka moto katika eneo la Manyamanyama Bunda barabara ya Mwanza Musoma.

Tukio hilo limetokea leo 21 july 2023 majira ya mchana  ambapo watumishi hao walikuwa wakitoka hospital ya Manyamanyama kwenda Bunda mjini.

Akizungumza na mazingira fm Paul Christopher  dereva wa gari hilo amesema wakati wanatoka hospitali ya manyamanyama aliona moshi ukitoka kwenye dashboard  ndipo aliposimamisha gari  ili kujua nini tatizo.

Christopher ameongeza kuwa baada ya kuona moshi umezidi walijitahidi kutumia kifaa cha kuzimia moto yaani fire extinguisher  pamoja na mchanga lakini hawakufanikiwa kuuzima moto.

Paul Christopher  dereva wa gari 
Gari la idara ya afya lililoteketea kwa moto. Picha na Adelinus Banenwa

Kwa upande wake Dkt Lucy kiongozi wa msafara huo ameiambia mazingira fm kuwa  moshi ndiyo umeanza kuonekana kwenye gari na harufu ya kitu kuungua ndipo alipomwambia dereva asimamishe  gari  na kushuka kisha kufungua bonet ya gari na kugundua tayarii moto umeshaanza kuwaka.

Aidha Dkt lucy amesema wanashukuru wametoka salama na vifaa vyao isipokuwa dereva ndo nyaraka zake zimeungua pia amewashukuru wananchi waliojitokeza kutoa msaada lakini gari lote limeteketea.

Dkt Lucy kiongozi wa msafara

Watumishi hao walikuwa wanatoka kata ya Guta mtaa wa Kinyambwiga  katika huduma ya  uzazi wa mpango .

Getere awakutanisha wananchi na taasisi za uhifadhi kilio cha wanyama waharibifu

 

Mhe. Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda akiwa katika mkutano kijiji cha Sarakwa kujadili mikakati ya kukabiliana na wanamapori waharibifu

Na Edward Lucas

Mbunge wa Jimbo la Bunda Mhe. Boniphace Mwita Getere leo amefanikisha ahadi yake ya kuwakutanisha wananchi wa vijiji vinavyopakana na mbuga ya Serengeti, taasisi za uhifadhi  na viongozi wa serikali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda ili kujadili na kuweka mikakati ya kusaidia kilio cha wananchi dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu.


Katika mkutano huo uliofanyika katika viwanja vya Shule ya msingi Stephen Wasira kijiji cha Sarakwa kata ya Hunyari ulitoa nafasi kwa wananchi kueleza changamoto mbalimbali, mapendekezo na ushauri huku viongozi wakitumia nafasi hiyo kufafanua baadhi ya hoja na kuelezea mikakati ya kukabiriana na changamoto hizo.




Wananchi wa kijiji cha Sarakwa wakiwasilisha hoja zao kuhusu changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu

Miongoni mwa hoja za wananchi kuhusu adha ni tembo kuingia katika mashamba na kuharibu mazao yao jambo linalopelekea kukosa uhakika wa chakula na kuwasababishia njaa huku wengine wakipoteza mifugo yao kutokana na uvamizi wa simba, chui na fisi na kubainisha kuwa fedha ya kifuta jasho au machozi haifiki kwa wakati na haitoshi ikilinganishwa na hasara inayosababishwa.


Katika mkutano huo wananchi wameomba kuwekewa kituo karibu cha kukabiliana na wanyama, kuwekewa uzio ili kutenga maeneo ya wananchi na hifadhi huku wakilia na mpango wa kuona gari moja tu ndilo likihudumu katika maeneo mengi ya wilaya ya Bunda jambo linalopelekea kutofika kwa wakati katika matukio.

David Mwakipesile, Meneja wa Idara ya Mawasiliano Grumeti Fund

"Ni kweli kituo cha Hunyari gari ni moja na ndilo tulilonalo kwa sasa...haya mengine nitayaacha kwa mbunge pamoja na watu wa serikali waangalie kama kutakuwa na uwezekano wa kuongeza gari waongeze lakini sisi kwa uwezo wetu tunalo hilo gari moja ambalo tunamudu kuliendesha" Mwakipesile

Kamishna Msaidizi kutoka TAWA, Said Kabanda

Akizungumzia mkakati huo, Kamishna Msaidizi TAWA, Said Kabanda amesema jambo la kukabiliana na wanyama waharibifu linahitaji ushirikiano wa wadau wote wakiwemo wananchi na taasisi zingine ili kufanikisha zoezi 

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dr Vicent Naano Anney

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dr Vicent Naano Anney amesema kuhusu changamoto ya upungufu wa gari inaichukua kwenda kuifanyia kazi kwa kuwashirikisha viongozi na wadau wengine ili kuhakikisha yanapatikana magari mengine mawili ili kuondoa kilio hicho kwa wananchi.

Aidha amewatahadharisha wananchi dhidi ya vitendo mbalimbali vinavyoweza kuhatarisha usalama wao hususani vitendo vya kuingia ndani ya hifadhi pasipo utaratibu maalumu.



Tuesday, 18 July 2023

Bulaya awashika mkono kituo cha kulea watoto yatima St. Francis-Bunda

 

Mbunge Viti Maalumu Mh. Ester Bulaya akisalimiana na watoto kituo St. Francis kilichopo Balili-Bunda. Picha na. Edward Lucas

Bulaya atembelea kituo cha watoto yatima na mazingira magumu St. Francis na kusaidia mahitaji mbalimbali kama sukari, mchele, unga na mafuta

Na Edward Lucas

Mbunge wa Viti Maalumu na ambaye pia amewahi kuwa Mbunge wa Bunda Mjini, Mh Ester Amos Bulaya leo ametembelea kituo cha kulelea watoto yatima St. Francis kilichopo mtaa wa Rubana kata ya Balili wilaya ya Bunda Mkoani Mara na kutoa mahitaji mbalimbali kwa ajili ya watoto.

Akizungumza baada ya zoezi hilo la kukabidhi Mchele, Unga, Sukari, Mafuta na mahitaji mengine Mh Ester amesema watoto hao wanahitaji upendo, ushirikiano na kutembelewa ili wapate moyo wa kuona kupoteza wazazi na kuwa katika changamoto ya mazingira magumu sio sababu ya kutotimiza ndoto zao.

Sauti ya Mbunge Ester Bulaya baada ya kukabidhi mahitaji kituo cha St. Francis

Katika ziara hiyo ambayo ilitoa nafasi ya watoto kuimba na kuuliza maswali mbalimbali kwa lengo la kupata motisha katika makuzi yao iliwapa nafasi pia watoto kutaka kujua kazi za mbunge na vipaumbele vyake katika kusimamia shughuli za maendeleo.

Sauti ya Ester Bulaya kuhusu maswali aliyokutana nayo kwa watoto

Kwa upande wake Kiongozi wa Kituo hicho, Sr Arta Lleshaj ameshukuru kwa kupokea mahitaji hayo na kuiomba jamii kuendelea kuwa karibu na watoto hao kwani bado wanamahitaji mengi.

Watoto wa kituo cha St. Francis wakiwa na Sr. Arta wakimsikiliza mgeni wao Mh Ester bulaya
Sauti ya Sr Arta akitoa neno la shukurani na kubainisha watoto wanaolelewa katika kituo hicho