Jeshi la Polisi katika wilaya ya Gomba nchini Uganda linachunguza tukio 
la kuuawa kwa mwanamke mjamzito aliyejulikana kwa jina la Amina 
Nabukeera (19) katika Kijiji cha Bakandula.
Akisimulia tukio hilo mume wa marehemu Bwana Arafat Kabuubi amesema 
tukio hilo limetokea juzi Mei 15, 2018 muda wa saa mbili usiku wakati 
akiwa na mkewe wakielekea kununua mahitaji ya nyumbani
“Mimi na mke wangu tulikuwa tunaenda moja ya maeneo ya biashara muda wa 
saa mbili usiku kununua mahitaji ya nyumbani, nilikua nikitembea mbele 
yake kabla sijasikia purukushani nyuma yangu na nilipogeuka niliona mtu 
akimshambulia mke wangu kwa kumpiga na nyundo kichwani, alimkata sikio 
la upande wa kulia pamoja na taya kwa kutumia panga kabla ya kukimbia. 
niliogopa sana na nilikosa nguvu za kumpigania mke wangu” amesema bwana 
Kabuubi
Bwana Kabuubi aliongeza kuwa alijaribu kupiga kelele za kuomba msaada 
lakini alikua tayari amechelewa kumuokoa mke wake ambae alifariki wakati
 akitafuta usafiri wa kumpeleka katika kituo kidogo cha afya.
Mkuu wa Polisi katika mkoa wa Katonga Kamanda Joseph Musana 
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuomba wananchi kuwa watulivu 
wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wa kumbaini mtuhumiwa.
Hilo ni tukio la pili kwa marehemu kushambuliwa ambapo mwezi Machi mwaka
 huu alishambuliwa akiwa nyumbani kwake lakini alipatiwa matibabu katika
 kituo kidogo cha afya.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Gomba ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa kidaktari.

No comments:
Post a Comment