Thursday, 19 April 2018

Beki wa Chelsea afungiwa


Chama cha soka England FA leo kimetangaza maamuzi mazito kwa beki wa kimataifa wa Hispania anayeichezea Chelsea ya England Marcos  Alonso baada ya kukutwa na hatia ya kosa la kumchezea faulo ya makusudi mchezaji wa Southampton Shane Long.

FA leo wametangaza kuamua kumfungia mechi tatu Marcos Alonso baada ya kumkuta na hatia na kugundua kuwa Marcos alifanya kwa makusudi kumkanyaga Shane Long na kukusudia kumuumiza, kabla ya adhabu hiyo kutolewa Marcos alipewa muda hadi jana Jumatano ya  April 18 saa 20:00 ajitetee kwa nini asiadhibiwe.

Beki wa Chelsea Marcos Alonso aliingia matatizoni Jumamosi ya April 14 2018 katika mchezo kati ya Chelsea dhidi ya Southamton uliyomalizika kwa Chelsea kupata ushindi wa magoli 3-2, baada ya kumchezea faulo  Shane Long.

Wachezaji hawa uwenda wakaondoka Man United mwisho wa msimu huu


Mtandao wa Squawka.com moja kati ya stori kubwa walioiripoti leo Alhamisi ya April 19 2018 ni pamoja na hii ya wachezaji wa Man United ambao wanatazamiwa kuwa wataondoka mwisho wa msimu kwa sababu mbalimbali ikiwemo kukosa nafasi ya kucheza.

1- Anthony Martial ametajwa kuwa ataondoka Man United baada ya kugoma kusaini mkataba mpya wa miaka mitano kutokana na kocha Jose Mourinho kutomchezesha mara kwa mara, hivyo vilabu vya Juventus na Inter Milan vimekuwa vikihusishwa nae kwa karibu, Martial ameanza katika game 16 tu za Man United msimu huu na nafasi yake amekuwa akipewa Rashford.

2- Paul Pogba pamoja na kuwa amenunuliwa kwa pesa nyingi kutoka Juventus na kujiunga na Man United na amefanikiwa kutoa assist nyingi zaidi ya mchezaji yoyote wa Man United katika EPL lakini amekuwa anafanya vizuri kiasi chini ya Jose Mourinho na kuna wakati watu walihoji namna ya Mourinho anavyomtumia kiungo huyo.

3- Marouane Fellaini huyu alikuwa moja kati ya wachezaji wanaopendwa sana na Jose Mourinho msimu uliyoisha lakini maisha yake Man United yanadaiwa kama kukaribia mwisho baada ya kufanikiwa kucheza katika game 19 pekee za mashindano yote msimu huu huku akianza katika game tano pekee na amecheza kwa jumla ya dakika 694.

4- Ander Herrera baada ya ujio wa Nemanja Matic ndani ya Man United Herrera ameonekana kuanza kukosa nafasi ya kucheza na amepata kuanza katika game 10 za Man United, hivyo uwepo wa wachezaji wanatajwa kumzidi uwezo kunaweza kumfanya akakimbia Man United na kwenda timu ambayo atapata nafasi ya kucheza.

5- Luke Shaw anatajwa kuwa yeye mwenyewe ameanza kuhisi kuwa hana nafasi tena ndani ya kikosi cha Man United kutokana na nafasi  yake kuwa kuna kiungo kama Ashley Young wameanza kucheza hiyo inatokana na jeraha lake la muda mrefu alilolipata msimu uliyopita hivyo anakosa nafasi pia kutokana na kukosa fitness.

Achunwa ngozi ya uume..wachunaji waondoka nayo kahama- shinyanga


Mkazi mmoja wa kijiji na kata ya Kinaga, Kahama mkoani Shinyanga amechunwa ngozi ya sehemu za siri baada ya kuleweshwa kwa pombe.

Watu waliomchuna mkazi huyo anayejulikana kwa jina la Paschal Misana, wametoweka na hadi sasa hawajajulikana.

Diwani wa kata hiyo, Mary Manyambo alisema tukio hilo lilitokea Aprili 16, baada ya Misana kupigiwa simu na mtu aliyekuwa akimdai Sh200,000.

“Lakini kwa maelezo ya muathirika ni kuwa baada ya kufika nyumbani kwa mtu huyo alinyweshwa pombe hadi akapoteza fahamu na alizinduka asubuhi ya siku iliyofuata, akajikuta amechunwa uume wake kuanzia kwenye korodani,” alisema Manyambo.

Mganga wa zamu katika Hospitali ya Mji wa Kahama, Dk Abdallah Simba alisema jana kuwa mtu huyo alifikishwa hapo juzi mchana akiwa na hali mbaya.

“Aliletwa hapa sehemu yake ya uume ilikuwa imekatwa kwa kuzunguka na kisha kunyofolewa ngozi yote ya sehemu hizo hali iliyosababisha kuvuja damu nyingi,” alisema.

“Wachunaji hao walimkata kitaalamu kwani hawakufika kwenye mishipa ya sehemu za siri na hivyo tayari ameshonwa na kurudishiwa alipokuwa amekatwa wakati wa kuchunwa.

“Sehemu zake za siri zinaweza kuendelea kufanya kazi kama kawaida kwa sababu sehemu za mishipa hazikukatwa.”

Akizungumzia tukio hilo akiwa hospitalini hapo anapoendelea na matibabu, Misana alisema baada ya kupigiwa simu hiyo alikwenda kwa lengo la kulipwa fedha alizokuwa amemkopesha mtu huyo.

“Nilimkopesha ng’ombe mmoja kwa thamani ya Sh200,000 na nilipofika baiskeli yangu iliingizwa chumbani na kisha nikakaribishwa ndani,” alisema.

Misana alisema baada ya kukaa, aliwaona wageni watatu waliokuwa chumbani, wawili wakiwa wanawake.

Alisema baadaye alitengewa ugali ambao alikula na wenyeji na baada ya kumaliza alipewa pombe aina ya shujaa waliyokuwa wakipewa pia wageni wengine.

Majeruhi huyo alisema baada ya kunywa pombe hiyo alipoteza fahamu mpaka asubuhi alipozinduliwa na mke wa mtuhumiwa.

Hata hivyo, alisema alishangazwa na kitendo cha kuwa peke yake akiwa uchi, huku akitokwa damu na sehemu zake za siri zikiuma.

“Sikujua chochote, baada ya watu kujaa wasamaria wema na kuanza kunipa huduma ya kwanza, walinieleza kuwa sehemu zangu za siri zilikuwa zimekatwa, hali iliyonishtua na baadaye polisi walifika wakanichukua na kunipeleka hospitalini,” alisema.

Kamanda wa polisi wa mkoa, Simon Haule alisema tayari wanamshikilia mtuhumiwa kwa ajili ya mahojiano.

Baada ya kuhojiwa, mtuhumiwa huyo alisema wageni wake watatu walihusika kumchuna ngozi Misana na kutoweka nayo na mpaka alipokamatwa hajui walielekea wapi.

Polisi wanaendelea kuwasaka wageni hao huku mtuhumiwa akiendelea kusaidia upelelezi.

Kamati za Maafa za Mikoa na Wilaya Kufanya Tathimini ya Maafa ya Mvua Nchini


Kamati za maafa za Mikoa na Wilaya kufanya tathimini ya kujua miundombinu iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha hapa nchini  ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mhe. Hussein Nassor juu ya mpango wa serikali  kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea nchini.

“Kipindi hiki tumeendelea kupata mvua nyingi nchini, ambazo zimesababisha maafa, Nawapa pole wale waliopoteza ndugu zao na kuharibiwa na miundombinu kutokana na mvua hizo,” alisema Waziri Mkuu.

Amesema, Serikali inaendelea kujipanga kuhakikisha miundombinu yote iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea inarejeshwa katika hali yake kupitia kamati za maafa za mikoa na wilaya kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA).

Hata hivyo, amewataka wakulima kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kwa kulima mazao ya chakula na biashara kwani Serikali imejipanga vyema kushirikiana na wakulima kutafuta masoko ya mazao hayo ndani na nje ya nchi.

Aidha Waziri Mkuu, ametoa wito kwa wananchi wanaoishi mabondeni kuhama kwani mvua zinazoendelea kunyesha zinaweza kuleta madhara  makubwa zaidi ikiwa ni pamoja na kupoteza maisha.

Vile vile Mhe. Majaliwa amesema, Serikali  imetoa shilingi Bilioni 160 kwa ajili ya kujenga na kuimarisha vituo vya afya ngazi za wilaya nchi nzima ikiwa ni sehemu ya mikakati ya Serikali kuimarisha huduma za afya hapa nchini.

Ameendelea kwa kusema, lengo la Serikali ni kuhakikisha vituo hivyo vya afya vinakuwa na chumba cha maabara, chumba cha upasuaji pamoja na chumba kwa ajili ya huduma ya mama na mtoto.

Amesema, ujenzi huo wa vituo vya afya unaenda sambamba na ujenzi wa nyumba ya mganga mkuu katika kila kituo.

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeweka utaratibu wa wabunge wa bunge hilo kumuuliza maswali ya papo kwa papo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kila siku ya Alhamisi katika mikutano yote ya Bunge.

Watu Watatu wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji -Bunda Mara


Jeshi la polisi wilaya ya Bunda Mkoani Mara linawashikilia Watu watatu kwa tuhuma za mauwaji ya mwanamkea mmoja aliyetambuliwa  kwa jina la  Bhoke mke wa matasu mwenye umri wa miaka 64 mkazi wa kijiji cha kyandege kata ya mgeta.

Tukio la kuuwawa kwa mwanamke huyo limetokea alfajiri ya tarehe 16 mwezi huu wakati mwanamke huyo akitoka chooni kujisaidia ndipo alipigwa na wauwaji hao na kitu chenye ncha kali sehemu za mgongoni na shingoni.

Baada ya  kutekeleza mauaji hayo watu hao hawakuchukuwa kitu chochote kutoka kwa marehemu licha ya marehemu kuwa na fedha kiasi cha shilingi laki moja ambapo imeelezwa kuwa chanzo cha mauji hayo ni imani za kishirikina.

Hata hivyo Jeshi la polisi wilaya ya bunda limetoa wito kwa wananchi kutoa taarifa mapema pindi wanapoona hali kama hiyo ndani ya jamii.