Kamati za maafa za Mikoa na Wilaya
kufanya tathimini ya kujua miundombinu iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea
kunyesha hapa nchini ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mhe.
Hussein Nassor juu ya mpango wa serikali kurejesha miundombinu
iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea nchini.
“Kipindi hiki tumeendelea kupata
mvua nyingi nchini, ambazo zimesababisha maafa, Nawapa pole wale waliopoteza
ndugu zao na kuharibiwa na miundombinu kutokana na mvua hizo,” alisema Waziri
Mkuu.
Amesema, Serikali inaendelea
kujipanga kuhakikisha miundombinu yote iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea
inarejeshwa katika hali yake kupitia kamati za maafa za mikoa na wilaya kwa
kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na Wakala wa
Barabara Mijini na Vijijini (TARURA).
Hata hivyo, amewataka wakulima
kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kwa kulima mazao ya chakula na biashara
kwani Serikali imejipanga vyema kushirikiana na wakulima kutafuta masoko ya
mazao hayo ndani na nje ya nchi.
Aidha Waziri Mkuu, ametoa wito kwa
wananchi wanaoishi mabondeni kuhama kwani mvua zinazoendelea kunyesha zinaweza
kuleta madhara makubwa zaidi ikiwa ni pamoja na kupoteza maisha.
Vile vile Mhe. Majaliwa amesema,
Serikali imetoa shilingi Bilioni 160 kwa ajili ya kujenga na kuimarisha
vituo vya afya ngazi za wilaya nchi nzima ikiwa ni sehemu ya mikakati ya
Serikali kuimarisha huduma za afya hapa nchini.
Ameendelea kwa kusema, lengo la
Serikali ni kuhakikisha vituo hivyo vya afya vinakuwa na chumba cha maabara,
chumba cha upasuaji pamoja na chumba kwa ajili ya huduma ya mama na mtoto.
Amesema, ujenzi huo wa vituo vya
afya unaenda sambamba na ujenzi wa nyumba ya mganga mkuu katika kila kituo.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania limeweka utaratibu wa wabunge wa bunge hilo kumuuliza maswali ya papo
kwa papo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa
kila siku ya Alhamisi katika mikutano yote ya Bunge.
No comments:
Post a Comment