Thursday, 18 May 2023

Changamoto ya kukosa huduma ya Afya yawaibua wakazi wa mtaa wa Mine kata ya Kabasa-Bunda.

 

Zahanati inayojengwa mtaa wa Mine kata ya Kabasa-Bunda kwa nguvu za Wananchi

Wananchi wa mtaa wa Mine Kata ya Kabasa Halmashauri ya Mji wa Bunda Mkoani Mara wameungana pamoja katika shughuli ya maendeleo kwa kujenga Zahati ili kuondokana na changamoto ya huduma ya afya katika eneo hilo.




Mafundi wakiwa 'site' kazi ya ujenzi wa Zahanati inaendelea


Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa zahanati hiyo, Samson Machibya amesema ni wiki ya pili hadi sasa tangu waanze ujenzi na wamefikia hatua ya 'lenta' ambapo katika hatua hiyo wananchi wamekuwa wakichangia fedha na kuleta mahitaji mbalimbali kama mawe, mchanga, kokoto na maji.

Samson Machibya, Mwenyekiti kamati ya Ujenzi wa Zahanati mtaa wa Mine 


Mhasibu wa kamati ya Ujenzi wa Zahanati, Lucas Budigila amesema katika hatua ya kujenga msingi wananchi walikubaliana kuchanga shilingi 13,500 na hatua za kuinua jengo walikubaliana kuchanga shilingi 32,000 kwa kila kaya ambazo zinauwezo wa kuchangia hii ni baada ya vikao na mapitio kwa kaya zenye uwezo na zisizo na uwezo.

Mhasibu wa kamati ya Ujenzi wa Zahanati mtaa wa Mine, Lucas Budigila 



Mwenyekiti wa Mtaa wa Mine, Shabani Juma Nkomba akiwa katika eneo la mradi kuhakikisha kazi ya wananchi inasimamiwa na nia ya kupata Zahanati inatimia.







Songoma Ramadhani Omari ambaye ni mkazi wa mtaa huo amesema "mimi ni mwenyekiti wa Chadema lakini baada ya Uchaguzi maisha yanaendelea siwezi kupinga maendeleo wakina mama walivyokuwa wanahangaika, watu walikuwa wanafia njiani kwa ajili ya kupelekwa katika huduma za kujifungua ..."


Nao baadhi ya wanawake na akina mama wa mtaa huo wameupongeza mpango huo na kusema utawaondolea changamoto ya kutembea mwendo mrefu na watoto katika huduma ambazo zinaweza kupatikana pindi Zahanati itakapo kamilika.









Wednesday, 17 May 2023

CCM Bunda hakuna mwenyekiti kurudisha muhuri.

 

Chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Bunda kimesema hakuna mwenyekiti wa mtaa hata mmoja halmashauri ya Bunda mjini kurudisha muhuri huku kikitoa siku 14 kwa viongozi wa halmashauri ya mji wa Bunda kukutana na wenyeviti wa mitaa 88 kusikiliza kero zao.

Maelekezo hayo ya chama yametolewa na mwenyekiti wa ccm wilaya ya Bunda Ndugu Mayaya Abraham Magese may 15 alipokutana na wenyeviti wa mitaa 88 ya halmashauri ya mji wa Bunda kufuatia sintofahamu ya maandamano ya wenyeviti hao siku ya ijumaa tarehe 12 may 2023 kuelekea ofisi za CCM wilaya ya Bunda wakitishia kujiuzulu nyadhifa zao endapo hawatasikilizwa.

Ndugu Mayaya amesema amekaa na wenyeviti hao na kuwasikiliza ambapo amesema madai yao ni Posho ya kujikimu kutokana na kazi wanazozifanya pia suala la ushirikishwaji katika miradi mbambali inayotekelezwa katika maeneo yao na kimsingi madai yao yana mashiko lakini mwenye majibu siyo chama bali  ni serikali.

Mayaya ameongeza kuwa kutokana na umuhimu wa kikao hicho pia aliwaalika mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Bunda na makamu wake kuja kujibu baadhi ya hoja ambazo zimeibuliwa na wenyeviti hao na baadhi yake zimejibiwa na zilizobaki ametoa siku 14 kwa halmashauri kukutana na wenyeviti hao kuzitatua kero hizo.

Aidha kuhusu viongozi hao kutaka kurudisha mihuri ya ofisi na kutaka kujiuzulu mwenyekiti Mayaya amesema hilo halitatokea hakuna mwenyekiti atayerudisha muhuri wala  kujiuzulu badala yake wawe na subra wakati serikali ikifanyia kazi malalamiko yao.

Naye mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Bunda Michael Kweka amesema kupitia kikao hicho wamewasikiliza wenyeviti na si dhamira ya halmashauri kutowapa stahiki zao wenyeviti bali ni kutokana na ufinyu wa mapato ya halmashauri lakini ameyachukua na kupitia baraza la madiwani watapata muafaka wa pamoja maana wanatambua kazi  nzuri inayofanywa na wenyeviti hao.

Kwa upande wake katibu wa umoja wa wenyeviti wa mitaa halmashauri ya mji wa Bunda Ritha Ikandiro amesema wao kama wenyeviti wanakishukuru chama kwa kuwasikiliza na kuwakutanisha na mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa bunda na wanasubili utekelezaji wa maelekezo ya chama kwa halmashauri ndandi ya siku hizo 14 yasipotekelezwa msimamo wao uko pale pale wa kujiuzulu.


TANAPA: Upigaji faini Mifugo inayoingia Hifadhini bado sio ‘mwarobaini’ kwa Wafugaji.

 

Albert Mziray

Upigaji wa faini kwa mifugo inayoingia katika maeneo ya hifadhi bado sio mwarobaini wa  kukomesha vitendo vya wafugaji kuingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi hususani katika kipindi cha kiangazi.

Hayo yamesemwa na Kamishina Msaidizi wa Tanapa Kanda ya Magharibi, Albert Mziray wakati akizungumza na Radio Mazingira Fm ofisini kwake jana tarehe 16 May 2023 kufuatia malalamiko ya baadhi ya wafugaji kukamatiwa mifugo yao inayoingia hifadhi na kupigwa mnada.

Mziray amesema utaratibu uliokuwepo ni kutoza faini ya shilingi laki moja (100,000) kwa kila mfugo lakini utaratibu huo bado haujafanikiwa kukomesha vitendo hivyo kwani adhabu inaonekana ni ndogo kwa wafugaji na kufanya vitendo hivyo kuendelea hususani katika kipindi cha kiangazi na wakati mwingine inaipa hifadhi kazi kubwa ya kuitunza mifugo baada ya wafugaji kukimbia.

Amesema kwasasa yapo maelekezo ya serikali kwamba mifugo hiyo inapokamatwa ndani ya hifadhi inataifaishwa na kupelekwa mahakamani kisha inapigwa mnada.

Albert Mziray

Mziray amesema zipo changamoto za mifugo kuingia kwenye maeneo ya hifadhi na kusababisha athari mbalimbali ikiwa ni pamoja na ushindani wa kupata malisho kwa wanyamapori na magonjwa kutokana na muingiliano wa wanyama wa kufugwa na wanyama pori hivyo

Albert Mziray

Friday, 12 May 2023

Rais Samia Amlilia Membe

 


Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesikitishwa na taarifa za kifo cha mwanasiasa na  waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa kimataifa Bernard Membe kilichotokea leo.

Rais ameandika kwenye ukurasa wake wa Instagram: Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Ndugu Bernard Membe. Kwa zaidi ya miaka 40 Ndugu Membe alikuwa mtumishi mahiri wa umma, mwanadiplomasia, Mbinge na Waziri aliyetumikia nchi yetu kwa weledi.

Pole kwa familia, ndugu, jamaa&marafiki. Mungu amweke mahali pema. Amina.

Ahukumiwa Jela Maisha kwa kosa la kumbaka mtoto wa Miaka 7

 



Mahakani wilayani Bunda imemuhukumu kifungo Cha Maisha Jela Melkiadi Mgaya,umri 22years, mkulima,mkazi wa mtaa wa Balili Bunda kwa kosa la kumbaka mtoto wa Miaka 7 kwa nyakati tofauti.


Kesi hiyo namba 238/2022 ya Kubaka, imetolewa hukumu May 10, 2023


Inaelezwa hakamani hapo na mwendesha Mashtaka wa polisi Tryphone Makosa Jacob kwamba mtuhumiwa amekuwa akimbaka mtoto wa kike umri 07 years, jina limehifadhiwa toka mwaka 2020 hadi tarehe 22/12/2022 alikutwa na Babu wa mhanga akiwa amempakata huku akimbaka.


Kesi ilifikishwa mahakamani 29/12/2022 mbele ya Mheshimiwa Mulokozi Paschal Kamuntu hakimu mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa mahakama ya wilaya na kusomewa mashitaka ambapo mshitakiwa alikana na ushahidi ulitolewa.


Tarehe 10/05/2023 amehukumiwa kwenda jela maisha baada ya mahakani kujilidhisha pasi na shaka kwamba mtuhumiwa alitenda kosa hilo angalia akijua ni kinyume na Sheria Kifungu 130 (1),(2) (e) na 131 (3) Kanuni ya adhabu sura 16 marejeo 2022


Awali Mwendesha mashitaka wa Polisi mkaguzi msaidizi wa polisi Tryphone Makosa Jacob amesema katika kesi hiyo Mashahidi 05 waliletwa upande wa mashtaka hivyo aliiomba mahakama kumpa adhabu kali kwa Mujibu wa kifungu cha sheria aliyoshtakiwa nayo Ili liwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo.


Naye mshtakiwa katika utetezi wake aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwani ni mkosaji wa mara ya kwanza na kwamba yeye ni mlemavu na hana wazazi

Thursday, 11 May 2023

Bei ya PAMBA msimu wa 2022/2023 hadharani

 

Wakulima wa zao la pamba watauza pamba yao kwa bei ya ukomo isiyopungua 1060 kwa msimu wa mwaka 2022 na 2023.

Hayo yamesema wa makaguzi wa zao la pamba wilayani Bunda Hemedi Kabea alipozungumza na Mazingira Fm iliyofika ofisini kwake kwalengo la kujua iwapo msimu wa pamba umefunguliwa ama la!.

Kabea amesema msimu wa zao la pamba tayari umefunguliwa kitaifa tangu tarehe 2 mwezi may mkoani Kigoma katika wilaya ya Kasuru ambapo bei ya kianzio ni 1060 kwa kilo lakini kampuni itakayopewa kipaumbele ni ile itakayokuwa na bei nzuri.

HEMEDI KABEA

Aidha amesema mkulima hatokatwa fedha ya pembejeo alizokopeshwa na bodi ya pamba badala yake atapokea fedha yake kama ilivyo .

HEMED KABEA

Kabea ameongeza kuwa kwa wilaya ya Bunda msimu bado haujafunguliwa kwa kuwa wanasubili miongozo itakayotumika katika msimu huu lakini maandalizi yote tayari yamefanyika ikiwemo ukaguzi wa mizani, uandaaji wa maghala ya kuhifadhia pamba miongoni mwa mengine.

Wednesday, 10 May 2023

CCM Bunda yawanoa makatibu wa uenezi kata

 

Chama cha mapinduzi CCM wiayani Bunda kimewataka makatibu wa siasa na uenezi kuzingatia itifaki katika Kutekeleza majukumu yao

hayo yamebainishwa vkatika semina elekezi ya kuwajengea uwezo makatibu hao wa siasa na uenezi ngazi ya kata kutoka kata 33 za wilaya ya bunda.


akizungumza na mazingira fm katibu wa siasa na uenezi ccm wilaya ya bunda ndugu gasper petro charles ambaye ndiye aliyeandaa semina hiyo amesema lengo kuu ni kuwajengea uwezo viongozi hao hasa ikizingatiwa uchaguzi umefanyika mwaka jana hivyo wengi wao wanakumbushwa majukumu yao

Gasper Charles

kwa upande wao baadhi ya washiriki wamepongeza hatua hiyo ya kupewa semina maana zipo changamoto zilizokuwa zinawakabili kama upande wa itifaki lakini pia nani anapaswa kupeperurusha bendera ya chama

Waenezi

naye magoti emanuel magoti miongoni mwa wakufunzi waseminishaji amesema chama cha mapinduzi kinaongozwa kwa kanuni hivyo semina ya leo itawasaidia viongozi hao kujua namna ya kufanya kazi zao ikiwemo kujua masuala ya itifaki katika chama


Wanufaika TASAF Bunda walia ucheleweshwaji fedha zao


Wito umetolewa kwa walengwa wa TASAF wilaya ya Bunda kuudhulia warsha za mafunzo ilikuwa na uelewa kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu malipo kwa familia hizo

hayo yamesemwa na afisa ufuatiliaji TASAF wilayani Bunda Alex Kumwalu alipokuwa akizungumza na wanufaika wa TASAF kata ya Bunda Stoo  katika kujibu changamoto mbalimbali zilizoelezwa na wanufaika hao.

ALEX KUMWALU AKIWASIKILIZA WANUFIKA WA TASAF BUNSA STOO

Kumwalu amesema tatizo kubwa kwa wanufaika pindi wanapokwenda kwenye warsha hizo hawafuatilii yale mafundisho na elimu wanayopewa badala yake wanawaza kupata fedha na kuondoka jambo linaloleta ugumu kwa waratibu maana katika mpango wa kuzinusuru kaya maskini kuna ruzuku tofauti kulingana na kaya yenyewe

kwa upande wao walengwa wa TASAF wamesema tatizo kubwa ni ucheleweshwaji wa fedha hizo maana mara ya mwisho ililipwa ile ya mwezi  Nov na Dec mwaka jana ambayo waliipata mwezi wa pili mwaka huu mpaka sasa hawajapta fedha yao sasa yapata mwezi wa tano

aidha changamoto nyingine iliyobainishwa ni upungufu wa vifaa vya kazi katika mpango wa ajira za muda mfano kama gunboot, groves, majembe miongoni mwa vifaa vingine

Flavian Chacha – Diwani

Naye diwani wa kata ya Bunda stoo Mhe Flavian Chacha amesema mara kadhaa amepokea malalamiko kutoka kwa wananchi wake hao ambao ni walengwa juu ya kucheleweshewa malipo yao jambo lililomsukuma kuitisha kikao hicho ili kuwakutanisha walengwa na waratibu wa TASAF ili kupata majibu ya changamoto zao

Hata hivyo ameshukuru mpango wa ajira za muda za TASAF maana zimeleta mabadiriko katika barabara zilizofunguliwa na wanufaika hao.

Kesi 104 za ukeketaji wilayani Tarime hazikufika mwisho kwa kukosa ushahidi

 

Timu ya waandishi wa habari wa kupinga Ukeketaji

imeelezwa kuwa ukeketaji unaovuka mipaka bado ni changamoto hasa katika jamii zinazoishi mipakani kati ya nchi na nchi.

hayo yamebainishwa katika ufunguzi wa warsha ya mafunzo kwa Waandishi wa habari za kupinga masuala ya ukeketaji unaovuka mipaka inayofanyika wilayani tarime mkoani Mara.

akizungumza katika warsha hiyo afisa utawi wa jamii kutoka wilayani tarime Antony Nyange amesema suala la ukeketaji unaovuka mipaka ni tatizo kubwa katika maeneo yanayopakana kati ya taifa moja na lingine kwa kuwa jamii kutoka pande zote katika mipaka ni za aina moja.

“tumekumbana na changamoto kubwa kupambana katika suala hili unakuta kiongozi anaishi upande mmoja wa nchi lakini anawaongoza wa hata wale kutoka upande wa pili wa nchi wajamii ile ile”.

“unakuta upande wa mama ni Kenya ila upande wa baba ni Tanzania hivyo ugumu unakuja pale ambapo unakutana na mtoto mpakani unadhani anavuka kwenda kukeketwa ia ukimkamata anakwambia anakwenda kwa mjomba au shangazi hivyo inakuawa ngumu kuendelea kuwashikilia” amesema Antony .

kwa upande wake Valeriani Mgani ambaye meneja miradi wa kituo cha AT-FGM MASANGA kilichopo tarime mkoani Mara amesema katika mataifa matano katika ukanda wa afrika mashariki walipitisha makubaliano 9 mnamo 17 /4/2019 ambayo yanatekelezwa katika mataifa yote matano.

Valeriani ameongeza kuwa mataifa hayo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia pamoja na Somalia ambapo amesema kwa mwaka 2021 hadi 2022 kesi 104 za ukeketaji zilizoripotiwa wilayani Tarime na kufikishwa mahakamani ila hakuna kesi hata moja iliyofika mwisho na kutolewa hukumu kutokana na kukosa ushahidi.

Pia kwa miaka mitatu iliyopita yaani 2019 hadi 2022 zaidi watoto 287 wamekimbilia Tanzania wakitokea kenya kukwepa ukeketaji.

Naye Michael Marwa ambaye ni kutoka shirika la C-SEMA amesema wameandaa warsha hii ikiwa lengo ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari kupaza sauti katika vita hii ya ukeketaji unaovuka mipaka .

Uwepo wa Sheria mahususi ya Ukeketaji itamaliza Ukatili huo Nchini.

 

Uwepo wa Sheria Mahususi inayopinga vitendo vya Ukeketaji Nchini Tanzania itasaidia kutokomoza Ukatili huu kwenye Jamii zilizoathirika na huo utamaduni3

Hayo yamesemwa na wadau wa kupinga Ukeketaji Nchini Tanzania katika mafunzo kwa waandishi wa habari ambapo lengo kuu la Mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo kuhakikisha Ukeketaji unaisha Nchini Tanzania

Claudi Mtweve

Akizungumza katika kikao hicho mkaguzi msaidizi wa Polisi Cloud Mtweve ambaye ni mratibu wa mradi wa kupinga Ukeketaji unaovuka Mipaka amesema Tanzania hatuna Sheria Mahususi inayopinga vitendo vya Ukeketaji japokuwa tunavyo vifungu Vya Sheria vinavyopinga masuala ya Ukatili wa kijinsia akitolea mfano Sheria ya kanuni ya Adhabu sura ya 16 kifungu na 169 A kifungu kidogo Cha (1) na (2) malejeo ya mwaka 2022, pia Sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009, kwa pamoja zinakataza kumfanyia mtoto huo Ukatili.

Aidha Mtweve ameeleza kuwa changamoto inayowakumba ni suala la ushahidi ambapo amesema kwa upande wao kama jeshi la polisi Ili kesi iweze kusikilizwa mahakani na kutolewa hukumu ni lazima awepo mlalamikaji na shahidi pili Ili mahakama iweze kutoa hukumu inatakiwa ijiridhishe pasipo kuacha shaka.

Amesema mara nyingi kesi za ukeketaji zinashindwa kufika mwisho kutokana na ugumu wa kupata walalamikaji pia mashahidi hivyo ingekuwepo Sheria ya kuwabana hata wazee wa kimila, mangariba, wazazi na walezi, wanaohusika wote kwenye sherehe hizo, marufuku ya ahadi ya zawadi ingeweza kusaidia.

Michael Marwa

Kupitia kwa Michael Marwa Mkuu wa Miradi kutoka Shirika lisilokuwa la kiserikali la C – SEMA kwa kishirikina na UNFPA ambao ndiyo wadhamini wa mafunzo haya amesema mafunzo haya yamewalenga waandishi wa habari kwa lengo la kwenda kuhihamasisha Jamii na kuishawishi mamlaka ili Kwa juhudi za pamoja suala la Ukeketaji hasa unaovuka mipaka (Cross Border FGM) unakwisha ifikapo 2030 kwa Mujibu wa mkakati uliyowekwa na mataifa matano ukanda wa Afrika ya Mashariki.

Waandishi wa habari za kupinga Ukeketaji

Mtoto wa mwaka Mmoja na Nusu apoteza maisha kwa kutumbukia kisimani

 

Kisima alipotumbukia mtoto

Mtoto mmoja Slavic anayekadiriwa kuwa na umri wa mwaka Mmoja na Nusu Mkazi wa Mtaa wa idara ya Maji kata ya Bunda stoo amepoteza maisha kwa kutumbukia kwenye kisima Cha Maji nyumban kwao.

kisima

Tukio hilo limetokea leo asubuhi 2 May 2023 ambopo inaelezwa mtoto huyo alitumbukia kisimani wakati akicheza karibu na hizo kisima jambo lililopelekea kutitia na kusababisha mtoto huyo kutumbukia.

Noela Richard, Shuhuda

Wakizungumza na Mazingira Fm mashuhuda wa tukio hilo Noela Richard amesema kisima hicho kimewekewa mfuniko lakini ndani hakijajengewa hivyo kutokana na mvua inayoendelea kunyesha kimesababisha udongo kuporomoka na kusababisha mtoto huyo kutumbukia.

“Mtoto huyo alikuwa anacheza pembezoni mwa kisima wakati mimi naosha vyombo hapa jirani na mama yake huyo mtoto alikuwa anaosha vyombo nikamwambia kuwa makini na huyo mtoto visima sasa hivi haviaminiki gafla nikaona mama yake Anapiga kelele nami nikashtuka namuuliza nini anasema mtoto katumbukia kwenye kisima huku na yeye akipiga piga miguu akitaka kutumbukia nikaenda haraka nikamvuta kumrudisha nyuma.” Alisema Noela.

Aidha Noela ameongeza kuwa baada kumtoa mama wa mtoto karibu na kisima aliwaita majirani na wapita njia ili kutoa msaada pia aliwapigia viongozi akiwepo Mwenyekiti wa Mtaa pamoja na Diwani Ili kuwapa taarifa juu ya tukio hilo huku jitihada za kumtoa mtoto huyo zikiendelea.

Naye Diwani wa kata ya Bunda stoo Mhe Flavian Chacha amesema kupitia tukio hilo anawasihi wazazi na walezi kuangalia usalama wa watoto hasa kutocheza karibu na maeneo hatarishi hasa visimani na maeneo mengine kama hayo.

Aidha amewaagiza wenyeviti wa mitaa, na watendaji kuhakikisha wanapita kwenye maeneo yao yote kuona ubora wa visima na mashimo ya vyoo na kuona namna ya kuwasaidia wananchi hao.

Friday, 5 May 2023

AHADI YA KAMBARAGE IMEANZA KUTEKELEZWA KUPAUA OFISI YA CCM MCHARO-BUNDA

Zoezi la upauaji jengo la ofisi ya CCM kata ya Mcharo lililopo mtaa wa Changuge-Bunda

Ikiwa ni wiki moja tangu Mwenyekiti wa kamati ndogo ya Fedha, Uchumi na Mipango CCM Wilaya ya Bunda, Kambarage Wasira afike kata ya Mcharo kuunga mkono juhudi za ujenzi wa ofisi ya CCM tayari kazi ya upauaji imeanza leo tarehe 5 May 2023.


Akizungumza na Radio Mazingira FM wakati wa zoezi la upauaji wa jengo hilo Mwenyekiti wa CCM kata ya Mcharo, Phinias Kasoga Budeba amesema baada ya kupokea mabati kutoka kwa Kambarage Wasira siku ya jumatano tarehe 3 May 2023 alipokea mbao na vifaa vingine vilivyokuwa vimeahidiwa hivyo kwa sasa wanaendelea na kazi.


"Baada ya jana kukutana tulipata taarifa kutoka kwa katibu kwamba tayari sasa kesho mafundi wanafika na shughuli ikaanzishwa, mpaka sasa kweli tuko hapa mafundi wako juu shughuli inaendelea kuchapwa kikamilifu sana" amesema Phinias Kasoga.

Mwenyekiti wa CCM kata ya Mcharo, Phinias Kasoga Budeba akiendelea kushuhudia hatua ya upauaji wa ofisi inayojengwa mtaa wa Changuge-Bunda


Naye Katibu wa CCM kata ya Mcharo, Samwel Makindi amesema  jengo hilo lina jumla ya vyumba vitatu(3) vya ofisi kwa ajili ya viongozi mbalimbali na ukumbi wa mikutano. Hivyo amewashukuru wadau wote waliotoa michango yao katika kufanikisha ujenzi wa jengo hilo na kutoa wito kwa wadau wengine kuendelea kuchangia ili kukamilisha ujenzi wa ofisi hiyo kwani bado litahitajika kuwa na madirisha, milango, rangi na vitu vingine.

Katibu wa CCM kata ya Mcharo-Bunda, Samwel Makindi akiwa katika viwanja vya jengo la ofisi ya CCM mtaa wa Changuge akishuhudia kazi inavyoendelea.



Jengo la ofisi ya CCM kata ya Mcharo lenye vyumba vitatu vya ofisi na ukumbi wa mikutano  likiendelea kuezekwa leo tarehe 5 May 2023










MITARO YA MAJI KUONGEZA ULINZI WA BARABARA NYASURA-BUNDA.

Barabara ya Mabanzini maeneo ya maduka 7 Nyasura baada ya kujengwa mtaro upande mmoja wa barabara kupunguza uharibifu wa barabara.


Wakaazi wa kata ya Nyasura Halmashauri ya Mji wa Bunda Mkoani Mara wametakiwa kulinda miundombinu ya barabara kwa kuhakikisha mitaro iko safi ili maji yaendelea kupita vizuri pasipo kuharibu barabara.


Wito huo umetolewa na Diwani wa Kata hiyo, Mh Magigi Samweli Kiboko wakati akifanya mahojiano na Radio Mazingira Fm jana tarehe 3 May 2023 kuhusu ufanisi wa mitaro katika kuendelea kulinda miundombinu ya barabara hususani katika kipindi hiki mvua zikiendelea kunyesha.


Mh Kiboko amesema hali ya sasa ni afadhali kuliko mwanzoni kwani barabara zilikuwa zikiwekewa changarawe lakini zinaharibika baada ya muda mfupi lakini kwasasa barabara zilizowekewa mitaro zimeendelea kuwa imara licha ya mvua kuendelea kunyesha.


Moja kati ya barabara ambazo zimejengewa mtaro kata ya Nyasura -maduka 7 zikionesha ahueni licha ya kuzongwa na tope wakati wa mvua kubwa.

"Kwa sasa hivi tangu tumejenga mitaro hii, barabara zile ambazo tumejenga mitaro na kuweka moramu kwa kweli zinapitika kipindi chote wakati mvua inanyesha" alisema Mh Kiboko.


Akitolea mfano wa barabara ya Nyasana, Dr Nchimbi na barabara ya Mabanzini maduka 7 amesema zilikuwa hazipitiki kiurahisi katika kipindi cha mvua kwani maji yalikuwa yakipita juu lakini kwasasa tangu zijengewe mitaro na kuwekewa moramu zinapitika kwa muda wote.


Kwa upande wao baadhi ya wakaazi wa kata ya Nyasura wamethibitisha kuwepo na mabadiliko makubwa katika upitikaji wa barabara hizo kwasasa tofauti na ilivyokuwa mwanzoni licha ya kutaja kasoro ndogo ndogo ikiwa ni pamoja na baadhi ya mitaro kuwa mifupi na kuruhusu maji kupita juu ya barabara  na kukosekana kwa moramu katika barabara jambo linalosababisha tope kuwa nyingi wakati wa mvua.