Chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Bunda kimesema hakuna mwenyekiti wa mtaa hata mmoja halmashauri ya Bunda mjini kurudisha muhuri huku kikitoa siku 14 kwa viongozi wa halmashauri ya mji wa Bunda kukutana na wenyeviti wa mitaa 88 kusikiliza kero zao.
Maelekezo hayo ya chama yametolewa na mwenyekiti wa ccm wilaya ya Bunda Ndugu Mayaya Abraham Magese may 15 alipokutana na wenyeviti wa mitaa 88 ya halmashauri ya mji wa Bunda kufuatia sintofahamu ya maandamano ya wenyeviti hao siku ya ijumaa tarehe 12 may 2023 kuelekea ofisi za CCM wilaya ya Bunda wakitishia kujiuzulu nyadhifa zao endapo hawatasikilizwa.
Ndugu Mayaya amesema amekaa na wenyeviti hao na kuwasikiliza ambapo amesema madai yao ni Posho ya kujikimu kutokana na kazi wanazozifanya pia suala la ushirikishwaji katika miradi mbambali inayotekelezwa katika maeneo yao na kimsingi madai yao yana mashiko lakini mwenye majibu siyo chama bali ni serikali.
Mayaya ameongeza kuwa kutokana na umuhimu wa kikao hicho pia aliwaalika mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Bunda na makamu wake kuja kujibu baadhi ya hoja ambazo zimeibuliwa na wenyeviti hao na baadhi yake zimejibiwa na zilizobaki ametoa siku 14 kwa halmashauri kukutana na wenyeviti hao kuzitatua kero hizo.
Aidha kuhusu viongozi hao kutaka kurudisha mihuri ya ofisi na kutaka kujiuzulu mwenyekiti Mayaya amesema hilo halitatokea hakuna mwenyekiti atayerudisha muhuri wala kujiuzulu badala yake wawe na subra wakati serikali ikifanyia kazi malalamiko yao.
Naye mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Bunda Michael Kweka amesema kupitia kikao hicho wamewasikiliza wenyeviti na si dhamira ya halmashauri kutowapa stahiki zao wenyeviti bali ni kutokana na ufinyu wa mapato ya halmashauri lakini ameyachukua na kupitia baraza la madiwani watapata muafaka wa pamoja maana wanatambua kazi nzuri inayofanywa na wenyeviti hao.
Kwa upande wake katibu wa umoja wa wenyeviti wa mitaa halmashauri ya mji wa Bunda Ritha Ikandiro amesema wao kama wenyeviti wanakishukuru chama kwa kuwasikiliza na kuwakutanisha na mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa bunda na wanasubili utekelezaji wa maelekezo ya chama kwa halmashauri ndandi ya siku hizo 14 yasipotekelezwa msimamo wao uko pale pale wa kujiuzulu.
No comments:
Post a Comment