Sunday, 17 September 2017

Baa, Migahawa na Vilabu vya Pombe Vyafungwa kwa Ugonjwa wa Kipindupindu

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Mh. Reuben Mfune ameagiza bar zote, migahawa, vilabu vya pombe na grocery kufungwa kwa siku zisizojulikana kutokana na ugonjwa wa kipindupindu kuzidi kusambaa wilayani humo.

Mkuu wa wilaya ametoa taarifa hiyo kupitia Afisa habari wa wilaya hiyo Daudi Nyingo na kuwataka wananchi kuwa makini na matumizi ya maji ya mito na mifereji kwani yameathiriwa na vijidudu vya kipindupindu.

"Wananchi wote wa wilaya ya Mbarali mnatangaziwa kuwa hali ya ugonjwa wa Kipindupindu bado ni mbaya sana wilaya hapa, hivyo basi biashara zote za migahawa, vyakula vyote vinavyotembezwa, minada, vilabu vya pombe, bar, grocery zote, pamoja na mikusanyiko yote inayohusiana na sherehe, vyote vimefungwa hadi hapo mtakapotangaziwa tena"

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali amesema kuwa mtu yoyote ambaye atakiuka maagizo hayo atachukuliwa hatua kali za kisheria

"Aidha mashine zote zitakazobainika kusaga vimea au unga wa pombe za kienyeji hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao Vilevile mnakumbushwa kwamba, maji yote ya mito pamoja na mifereji yameathiriwa na vijidudu vya Kipindupindu, hivyo basi wananchi wote mnaagizwa kuchemsha maji au kutumia vidonge vya 'water guard' pamoja na kufanya matumizi sahihi ya vyoo" alisema Mfune

Hadi kufia Septemba 15, 2017 jumla ya wagonjwa 628 wamepatikana huku jumla ya watu nane wamefariki kutokana na ugonjwa wa Kipindupindu wilayani Mbarali jijini Mbeya.

Mabasi yakamatwa usiku wa manane kwa mwendokasi

Mabasi saba ya abiria yamekamatwa  na kutozwa faini kwa kosa la mwendokasi na kutofuata sheria za usalama barabarani huku wakihatarisha maisha ya abiria.

Kamatakamata hiyo  ambayo imesimamiwa na Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani   Fotunatus  Muslim akiwa na timu ya viongozi na askari  mkoa wa Morogoro imefanyika usiku wa kuamkia leo.

Zoezi la ukamataji mabasi hayo limefanyika eneo la Dumila Wilaya ya Kilosa mkoani hapa, zoezi lilichukua takribani masaa mawili ambapo mabasi hayo yamezuiwa kuondoka mpaka asubuhi huku yakitozwa faini.

Kamanda Muslim amesema jeshi hilo halitakubali kuona maisha ya watanzania yakipotea  kutokana na uzembe wa baadhi ya madereva.

Amesema  kikosi hicho cha usalama barabarani kimeahidi kupambana na madereva wa mabasi ya abiria hasa nyakati za usiku kwani ndio wamekuwa wakiendesha kwa mwendokasi huku wakidai  serikali muda huo inakuwa imelala.

Mabasi ya abiria zaidi ya saba yanayofanya safari kati ya mkoa wa Mara (Musoma) Dar es salaam, na Mwanza- Dar es salaam yamekaguliwa na kutozwa faini.

Muslim amesema  madereva wengi wamekuwa wakifuata sheria za barabarani nyakati za mchana kwa kuhofia kukamatwa kutokana na tochi zilizopo na inapofika nyakati za usiku madereva hao wamekuwa wakitumia mwanya wa kuendesha kwa mwendo kasi.

 Akizungumzia dhamira ya Polisi  Muslim amesema ni kuwalinda raia na mali zao na kuwataka askari wa usalama barabarani kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Amesema doria ni endelevu na sasa itakuwa kwa nchi nzima kwa usiku na mchana huku akiwataka madereva hao kuacha kudanganyika kwa madai kuwa tochi usiku hazifanyi kazi usiku na kwamba tochi sasa zitakamata mpaka usiku.

"Nimekuja na slogani ya Kamata hii ni kwa wale madereva wasiotii na kufuata sheria na tutapambana nao kila wakati na nyakati zote na hiyo itasaidia abiria kusafiri salama na matumizi ya barabarani kuwa bora," amesema kamanda Muslim

Mmoja wa abiria aliyejitambulisha kwa jina la Leon Mwete aliyekuwa katika moja ya basi yaliyokamatwa eneo hilo la Dumila amesema zoezi hilo ni zuri na linafaa kuendelea.

Amesema hii itapunguza ajali za barabarani na kwamba kwa sasa uendeshaji wa madereva wengi ni mzuri ukilinganisha na zamani.

Naye kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Morogoro Boniface Mbao ameeleza kuwa yeye akiwa msimamizi mkuu ataendelea kusimamia na kufanya oparesheni za usiku na mchana kama maelekezo yaliyotolewa.

Friday, 15 September 2017

Wanafunzi wa shule za msingi kupigwa marufuku kuzukuka mtaani kuomba msaada wa kufanikisha mahafali



Tabia ya baadhi ya wanafunzi wa kike wa shule mbali mbali za msingi na sekondari wilayani bunda,mkoani mara,ya kuzunguka mitaani na kuwaomba wananchi wawachangie fedha  kwa ajili ya kufanikisha mahafali yao kumaliza elimu ya msingi na sekondari, imekuwa kero kwa baadhi ya wazazi na kuwaomba walimu wakuu wa shule hizo kukomesha tabia hiyo.

Hayo yamesemwa na baadhi ya wazazi walipozungumza na redio mazingira fm, na kuwaomba walimu wakuu wa shule hizo kuwaita wazazi wa wanafunzi wanaohitimu katika shule hizo ili kutafuta njia nzuri  ya kufanikisha mahafali hayo ili kuwaepusha watoto wa kike kukumbwa na vitendo vya ubakaji kutoka kwa watu wenye nia mbaya.

Baadhi ya wanafunzi wa kike ambao wamezungumza na na redio mazingira fm,wamekiri kupata majaribu mengi toka kwa baadhi ya watu wanaowafikia kwa ajili ya kuwaomba kuwachangia fedha kwa ajili ya mahafali yao,badala yake watu hao huwashawishi kufanya nao mapenzi na kuwaahidi kuwapatia fedha nyingi endapo watawakubalia tendo hilo.

Wakati serikali ikipambana vikali na kukemea baadhi ya watu wanaowarubuni wanafunzi wa kike nakuwapatia mimba,baadhi ya watu wanaoendekeza tamaa zao za mwili bado wanaendelea na tabia hiyo na kujikuta wana waharibia masomo na kukatiza ndoto za maisha yao ya baadae.


Thursday, 14 September 2017

Serikali Yaunda Kikosi Maalumu Kudhibiti Mashambilizi Ya Risasi Nchini

Wiki moja baada ya kujeruhiwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu Serikali imeunda kikosi kazi kushughulikia uvunjifu wa amani nchini.

Kikosi hicho kinachoshirikisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama pia kinashughulika na kukusanya silaha za kivita ambazo zimekuwa zikitumika.

Lissu alijeruhiwa kwa risasi Alhamisi Septemba 7 nyumbani kwake Area D mjini Dodoma na sasa anaendelea na matibabu jijini Nairobi, Kenya.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi amesema hayo bungeni leo Alhamisi akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Chambani (CUF), Yusuf Salim Hussein.

Mbunge huyo amesema hana wasiwasi na uimara, uwezo na weledi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kusimamia majukumu yake ndiyo maana nje ya mipaka ya nchi ni salama lakini ana wasi wasi kuhusiana na hali ya usalama nchini.

“Lakini ndani ya nchi yetu hali si salama na mifano miwili ya juzi ya mbunge (Lissu) na Meja Jenerali mstaafu Vincent Mritaba inadhihirisha kwamba ndani ya nchi yetu tuna matatizo, je ni kwa nini Jeshi la Wananchi lisishiriki kikamilifu kuondosha matumizi ya silaha na mauaji ya raia wasio na hatia ndani ya nchi yetu?” alihoji mbunge huyo.

Amesema anavyoona yeye silaha za kivita zinamilikiwa na JWTZ na matumizi yake yanatakiwa yawe ya chombo hicho.

Mbunge huyo alihoji ni kwa nini wasitumike askari maalumu kuhakikisha silaha za kivita zinazotumika vibaya kuua raia zinakamatwa.

Waziri Mwinyi akijibu swali hilo amesema ni dhahiri kwamba kazi ya JWTZ ni ulinzi wa mipaka lakini pale linapohitajika au kuombwa kusaidia mamlaka zingine za kiraia au vyombo vingine vya ulinzi na usalama huwa tayari kufanya hivyo.

“Tunavyozungumza ni kwamba, mamlaka hizo ambazo ni vyombo vingine vya ulinzi na usalama vikihitaji msaada wa jeshi mara zote tunakuwa tayari kutoa msaada huo, kwa hali ilivyo sasa imeundwa task force (kikosi kazi) inayojumuisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama ili kulifanyia kazi tatizo hili la uvunjivu wa amani ndani ya nchi,” amesema.

Amesema hana shaka na kazi hiyo imeanza, hivyo kuwahakikishia wananchi kuwa jukumu hilo litafanywa vyema ili hali ya usalama iwepo ndani ya nchi.

Dk Mwinyi amesema ni kweli silaha za kivita zinadhibitiwa na JWTZ na kwa kutumia kikosi kazi hicho, watakusanya silaha hizo kutoka kwa raia au watu wengine wote ambao wanamiliki silaha hizo ambazo kwa kawaida, utaratibu na kisheria hawapaswi kuwa nazo.

Amesema zitakapopatikana silaha hizo zitarudishwa katika mamlaka zinazohusika.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Mkoani (CUF), Twahir Awesu Mohamed alihoji Serikali imejipangaje kuimarisha amani nchini.

Waziri Mwinyi amesema JWTZ imejipanga kikamilifu kuhakikisha mipaka ya nchi inalindwa muda wote dhidi ya adui yeyote atakayejitokeza kuivamia.

“Jeshi letu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, limeimarisha ulinzi katika maeneo ya mipaka yenye wakimbizi ,” amesema.

Amesema hatua hiyo imesaidia kuzuia na kukabiliana na vitendo vya kihalifu vinavyowezwa kusababishwa na wakimbizi katika mipaka na katika makambi.

Spika Job Ndugai Amtolea UVIVU Godbless Lema

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai, amejibu tuhuma za mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, na kumtaka asipotoshe wananchi, bali apeleke malalamiko yake kwenye kamati.

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akiendesha bunge, na kusema kwamba bunge lina utaratibu wake kwenye kila jambo linalohusika bungeni hapo.

"Lema asipotoshe wananchi aende hadharani kwenye kamati kuzungumzia hayo, bunge haliwezi kusimama kwa shambulio la Lissu bali kanuni zinasema mbunge akifariki bunge linasimama kwa siku moja. Na iwapo Spika akiletewa jambo la maadili linapelekwa kamati ya maadili, suala la jinai linapelekwa polisi", amesema Spika Ndugai

Pia Spika Ndugai amesema suala la Tundu Lissu kuchangiwa fedha za matibabu na wabunge wakati yeye alitibiwa nje ya nchi ni kwamba matibabu ya Tundu Lissu yameenda kinyume na utaratibu wa bunge.

"Wabunge wanaopelekwa nje (India) wanapewa rufaa kutoka hospital ya Muhimbili lakini si kama alivyopelekwa Lissu", amesema Spika Ndugai.

Pamoja na hayo Spika Ndugai amesema anamsamehe Godbless Lema na kuwataka watu kumsamehe kwani hajui alitendalo.

Hapo jana mbunge wa Arusha Godbless Lema alimlaumu Spika Ndugai kuwa anashindwa kutetea kiti chake, kwa kuzidi kuwakandamiza wabunge wa upinzani hususan suala la kupigwa risasi kwa Tundu Lissu.

Mabomu ya Machozi yatumika kuwatawanya madiwani Geita

Polisi wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi na madiwani waliofunga  barabara ya kuingia kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).

Katika tukio hilo leo Alhamisi asubuhi, madiwani wawili na baadhi ya wananchi wamekamatwa na polisi.

Kabla ya kutumia mabomu, polisi walitoa onyo wakiwataka wananchi na madiwani hao kutawanyika kwa amani lakini waligoma.

Madiwani wa  halmashauri mbili za Wilaya ya Geita jana Jumatano walitanga mgogoro na GGM wakishinikiza kulipwa Dola 12 milioni za Marekani zinazotokana na ushuru wa huduma kuanzia mwaka 2004 hadi 2013.

Walitangaza kuzuia magari ya mgodi kwa    kufunga barabara  na pia kufunga maji yanayoingia mgodini kutoka Ziwa Victoria.

GGM iliwatangazia wafanyakazi wake jana kutofika kazini leo kutokana na mgogoro huo.

Polisi hivi sasa wameimarisha ulinzi kwenye maeneo ya Nungwe uliko mradi wa kusambaza maji mgodini, eneo la uwanja wa ndege na geti la kuingia mgodini.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi na mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma wameingia mgodini baada ya madiwani na wananchi kutawanywa

Vijana katika Halmashauri ya Mji wa Bunda Mkoani Mara wameombwa kutambua kuwa wao ni nguvu kazi ya taifa siku zote.

Vijana katika Halmashauri ya Mji wa Bunda Mkoani Mara wameombwa kutambua kuwa wao ni nguvu kazi ya taifa siku zote, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa bidii bila kubagua kazi, ili kuweza kuleta maendeleo katika jamii na taifa kwa ujumla.

Ushauri huo umetolewa baadhi ya vijana wa mtaa wa wa bank wakati wakizungumza na redio mazingira hii leo
Juma Hamis na Debora Joram  wamesema vijana wasipojituma kufanya kazi kwa bidii kauli ya kusema  vijana ni nguvu kazi ya taifa itabaki midomoni mwa watu bila vitendo vyovyote, hivyo ni wakati wakujituma ili kauli hiyo iwe kwa vitendo.

Katika hatua nyingine vijana hao wameiomba halmashauri ya mji wa Bunda, kuwajali vijana katika upande wa asilimia iliyotengwa na serikali ili kuweza kusaidia katika majukumu yao ya kujituma.  




vijana wa mgambo 166 wachukuliwa na Suma jkt wilayani Bunda

Mkuu wa wilaya ya Bunda Mkoani Mara mwl.Lydia Bupilipili amewapongeza wale wote waliojitokeza miaka ya nyuma kushiriki mafunzo ya mgambo, kwani wamekuwa msaada mkubwa ndani ya jamii katika utekelezaji wa majukumu ya ujenzi wa taifa.

Bulipili ametoa Pongezi hizo siku chache baada ya wanamgambo 166 kuchukuliwa na Suma jkt, kwajili ya kwenda kulinda katika makampuni  mbalimbali hapa nchini.

Aidha Bulipili amesema kuwa, vijana waendelee kujitokeza kwa wingi kushiriki mgambo kwani serikali ya wilayani Bunda imedhamilia kumaliza kero mbalimbali likiwemo suala la ajira.

Hata hivyo Bupilipili  amesema mngambo ni kitu muhimu sana na sio cha kubezwa hata mara moja hivyo vijana wasione aibu kushiriki kwa asilimia mia moja.


tabia ya kuanzisha masoko kiholela pasipo mpangilio yapigwa marufuku Bunda

Mkuu wa wilaya ya Bunda mwl. Lydia Bhupilipili amekemea tabia ya uwanzishwaji wa masoko kiholela pasipo mpangilio kwani hali hiyo  inapelekea kukosesha mapato ndani halmashauri na serikali kiujumla.
Bhupilipili ameyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake ambapo amekemea tabia hiyo na kuwataka wataalamu wa mipango miji kuhakikisha wanafanya kazi yao ipasavyo. 

Aidha Bhupilipili amemtaka mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa bunda Janeth Mayanja kuhakikisha ana wasimamia wahusika wote wa mipango miji ili waweze boresha na kusitisha uwanzishwaji wa masoko kila sehemu bila utaratibu hali inayopelekea uchafudhi wa mazingira katika maeneo hayo.


Katika hatua nyingine Bhupilipili amesema kuwa kwa sasa stendi mpya ya Mabasi kumekuwa na mbanano wa magari na kushauri kwamba utengenezwe utaratibu wa baadhi ya magari mfano yanayo kwenda nyamuswa yawe yanatokea Manjebe ili kupunguza msongamano uliopo kwa sasa katika stedi hiyo.

ng’ombe 7485 katika kata ya bunda stoo katika halmashauri ya mji wa bunda kuwekewa chapa

Jumla ya ng’ombe 7485 katika kata ya bunda stoo katika halmashauri ya mji wa bunda  inatarajiwa kusajiliwa ikiwa ni sambamba na uwekaji  chapa zoezi litakalochukua siku 10 kukamilika.

Zoezi hilo la uwekaji chapa kwa mifugo limeanza tarehe saba mwazi huu katika kijiji cha butakale na linatarajiwa kukamilika tarehe 17  Mwezi wa tisa mwaka huu.
Akisoma taarifa fupi ya mifugo mbela ya mkuu wa wilaya ya bunda, mtendaji wa kata hiyo bwana  Raymond Bukombe amesema kuwa kata hiyo inajumla ya mifugo 27485 na yote inatarajiwa kusajiliwa.


Hata hivyo mkuu wa wilaya ya bunda Mwalimu Lydia Bupilipili amewapongeza wafugaji wa kata ya bunda stoo kwa kuhamasika kepeleka mifugo yao kuwekewa chapa na kusajiliwa kwa kuwa zoezi hilo ni la kitaifa na ni muhimu kwani inapunguza baadhi ya changamoto ikiwemo wizi wa mifugo

wazazi na walezi watakiwa kuendelea kulea vizuri watoto wao waliohitimu dara la saba mwaka huu

Baada ya wanafunzi wa darasa la saba kumaliza mtihani wa kumaliza elimu ya msingi nchini  mnamo septemba 7  mwaka huu, wazazi na walezi wa watoto hao wametakiwa kuendelea na ushirikiano ule ule wa kuwalea watoto hao katika maadili mema.

Hayo yamesemwa na  baadhi ya wakazi wa kata ya kabarimu  halmashauri ya mji wa bunda kwa nyakati tofauti ambapo wamesema kuwa wapo baadhi ya wazazi hujisahau kuwapa malezi mazuri watoto hao na kuwaacha wakifanya mambo yasiyo yakimaadili kama kujihusisha na vitendo vya ngono.

Mmoja wa wakazi hao bwana Thomas Ezekil amesema kuwa wazazi wanapaswa kutambua kwamba watoto hao bado ni wanafunzi na wanasubiri matokeo yao ili waendelee na masoma yao.

“sisi wazazi tunapaswa kutambua kwamba watoto hao ni bado ni wetu “

HOSPITALI YA WATOTO YA HUNAN YAWAFUNDA MADAKTARI NA WAUGUZI WA ZANZIBAR

Makamu wa Raiswa Hospitali ya watoto ya Hunan Chini China Zhu Lihui ameahidi kuwa Hospitali hiyo itaendelea kushirikiana na Hospitali ya Mnazimmoja ya Zanzibar kuwajengea uwezo wafanyakazi na kuimarisha Utawala wa Hospitali.
Zhu ameeleza hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku kumi yanayowashirikisha madaktari na wauguzi 25 wanaoshughulikia watoto kutoka Hospitali ya Mnazimmoja, Kivunge na Makunduchi.
Amesema Hospitali ya watoto ya Hunan imewahi kutoa mafunzo kwa wafanyakazi 26 katika vipindi tofauti nchini China imeamua kufanya mafunzo Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Afya iliwafanya kazi wengi waweze kufaidika.
Ameeleza matarajio yake kuwa wafanyakazi waliopata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo wataenda kuwaelimisha wafanyakazi wenzao ambao hawakubahatika kushiriki.
Aidha amesema kuja kwamadaktari bingwa kutoka jimbo la Hunan kutoa mafunzo hapa Zanzibar kutaongeza  mashirikiano kati ya Hospitali ya Mnazimmoja na kubadilishana uzoefu katika kuimarisha afya za wananchi na kuimarisha masuala ya utawala.
Balozi mdogo wa China aliepo Zanzibar Xie Xiawu amesema ushirikiano baina ya China na Zanzibar niwamuda mrefu na nchi yake itaendelea kusaidia Zanzibar katika kuimarisha na kukuza maendeleo ya wananchi.
Alisema mafunzo yatakayotolewa na wataalamu kutoka Hospitaliya watoto ya Hunan yatawajengea uwezo watendaji wa wodi za watoto na kuimarisha afya ya mama baada ya kujifungua na watoto wanaozaliwa. 
Akifungua mafunzo hayo yanayofanyika Hospitali mpya ya wazazi ya Mnazimmoja, Naibu Waziri wa Afya Harusi Saidi Suleiman aliishukuru Hospitali ya watoto ya Hunan kwa kusaidia kuwaongezea ujuzi wafanyakazi wanaoshughulikia matatizo ya watoto na kuimarisha utawalawa Hospitali.
Aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa wasikivu na kufuatilia kwa karibu masomo watakayo someshwa ili nao kuja kuwa walimu kwa wengine baada ya kumaliza na kuwawezesha wataalamu wa China kusomesha kada nyengine za afya.

Tundu Lissu bado Yupo ICU

Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema ambaye sasa yupo Kenya amefunguka na kueleza kuwa hali ya Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu sasa ina afadhali ukilinganisha na hali aliyokuwa nayo siku mbili zilizopita ila amedai mpaka sasa bado yupo ICU.

Lema amesema hayo alipokuwa akifanyiwa mahojiano na BBC Swahili  na kudai kuwa hali ya kiongozi huyo inazidi kuimarika ukilinganisha na siku za awali ambazo alikuwa amefanyiwa shambulio hilo.

"Mgonjwa anapokuwa yupo hospitali tena kwenye chumba cha wagonjwa mahututi huwezi kusema hali ya mgonjwa ni nzuri lakini kwa kadri ambavyo tumekuwa hapa Nairobi kwa siku zote mimi na wenzangu akiwepo Mchungaji Msigwa, mke wa Lissu na Mwenyekiti wetu Freeman Mbowe tunaweza kusema kuna mabadiliko lakini bado Tundu Lissu yupo ICU na ni wito wetu kwamba Watanzania wote wenye mapenzi mema waendelee kumuombea Tundu Lissu " alisema Godbless Lema

Aidha Lema anasema kuwa jaribio la kutaka kumuuwa Lissu ni mpango na watu waliofanya hivyo siyo majambazi bali walifanya hivyo kwa lengo la kutaka kutuma ujumbe kuwa wanaweza kufanya lolote na wasifanywe jambo lolote.

Mbunge Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 akiwa mjini Dodoma na baadaye kupelekwa nchini Kenya kupatiwa matibabu.

Waziri Mkuu: asema Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayejaribu kuvuruga amani yetu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania ipo salama na imara na kwamba mtu yeyote atakayejaribu kutaka kuvuruga amani atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Ametoa kauli hiyo jana (Jumatano, Septemba 13, 2017) alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Iran nchini Tanzania, Bw. Mousa Farhang jijini Dar es Salaam.

“Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote kutoka popote atakayejaribu kuvuruga amani yetu. Nawaomba wananchi muwe makini na muendelee kuidumisha amani yetu.”

Amesema kwa sasa Serikali ipo katika mapambano dhidi ya vitendo vya ufisadi, rushwa, biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na wahujumu uchumi.

Waziri Mkuu amesema licha ya Tanzania kuwa ni nchi ya amani na yenye utulivu wa kisiasa, wameendelea kuwahamasisha wananchi wake kudumisha mshikamano.

Amesema mbali ya kuimarisha amani nchini, pia Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji jambo ambalo litawawezesha watakaokuja kuwekeza nchini kupata tija.

Hivyo ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini Iran ili waje kuwekeza kwenye viwanda mbalimbali vikiwemo  vya kuchakata mazao ya  kilimo.

Pia amewakaribisha raia wa Iran kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyoko nchini Tanzania kama mlima wa Kilimanjaro, fukwe, mali kale na mbuga za wanyama.

Kwa upande wake, Balozi Farhang  ameipongeza Serikali kwa kuwa na dhamira ya dhati ya kuimarisha uchumi na kupambana na dawa za kulevya na ufisadi.

Balozi huyo amesema Serikali ya Irani ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi pamoja na vitendo vingine vya kihalifu.

Balozi Farhang ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali ya Tanzania ifungue Ofisi ya Ubalozi nchini Iran ili kuimarisha uhusiano huo, ambapo Waziri Mkuu amekubali.

Pia Bw. Farhang amesema aliwahi kutembelea mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro na kusema kwamba ni maeneo mazuri ambayo hajawahi kuyaona tangu azaliwe.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Wednesday, 13 September 2017

Mlinzi wa Meja Jenerali aliyejeruhiwa kwa risasi Dar akamatwa

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu wawili akiwemo mlinzi wa Suma JKT na mhudumu wa benki ya NBC tawi la Tangibovu ambao wanatuhumiwa katika tukio la kujeruhiwa kwa risasi Meja Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ), Vincent  Mritaba.

Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema leo Jumatano kuwa Septemba 11 mwaka huu saa 11 jioni maeneo ya Tegeta Masaiti jeshi hilo lilipata taarifa ya Mritaba kuvamiwa na watu wawili wasiojulikana ambao walimjeruhi na kumpiga risasi ya begani, tumnoni na kwenye paja la mkono wa kulia huku wakimpora kiasi cha Sh5 milioni.

Amesema tukio hilo lilitokea baada ya mstaafu huyo kutoka kuchukua fedha hizo katika benki ya NBC tawi la Tangibovu akiwa kwenye gari lake ya Volkswagen Amarok.

Mambosasa amesema alipofika nyumbani kwake alipiga honi na kufunguliwa geti na mlinzi wake Godfrey Gasper.

Amesema geti lilipofunguliwa pikipiki ilisimama hapo getini na watu wawili waliokuwa wamevaa helment walishuka na kulifuata gari huku wakiwa na silaha aina ya bastola ndipo walishambulia upande wa kulia wa dereva na katika kioo cha mbele.

"Huku wakimwamuru ashuke ambapo risasi zilimjeruhi maeneo ya begani, tumboni na kwenye paja la mkono wa kulia na kutokomea kusikojulikana kwa kutumia pikipiki waliokuja nayo," amesema Mambosasa.

Mambosasa amesema cha kushangaza wakati mlinzi huyo anaenda kufungua geti silaha yake aina ya shotgun yenye namba TZCAR9644 aliiacha kwenye kibanda cha ulinzi huku ikiwa chini ya kitanda.

Amesema baadaye watuhumiwa walimwambia akimbie katika eneo hilo na yeye alitii amri hiyo na kwenda mbali na tukio hilo jambo ambalo linatia shaka.

"Ninavyojua askari wa Suma JKT anapewa mafunzo ya ukakamavu haiwezekani uache silaha chini ya kitanda unakwenda kufungua geti kitu ambacho sikubaliani nacho,"amesema

Amesema walipofuatilia mawasiliano ya mmoja wa wahudumu wa benki hiyo walibaini kuwa alikuwa anapanga mipango na watu mbalimbali wanaokwenda katika benki hiyo. Hivyo msako mkali unaendelea ili kuwabaini watuhumiwa waliohusika katika tukio la kujeruhi kwa risasi afande huyo.

Pia alizungumzia kuvunjwa kwa ofisi ya wakili ya Prime Attoneys akieleza kuwa wanaendelea na msako mkali ili kuwabaini waliohusika katika tukio hilo na watakapokamatwa watachukuliwa hatua za kisheria.

Mkuu wa Majeshi Atoa ONYO Zito

Mkuu wa majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo amefunguka na kusema kuwa vyombo vya Ulinzi na usalama vinakabiliana na matukio ya uhalifu yanayotokea nchini kadili yanavyojitokeza na kusema kuwa anaimani uhalifu huo utakwisha.

Mabeyo amesema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari na kudai kuwa kwa sasa wanataka kujiridhisha kuwa silaha hizo zinazotumika na hao wahalifu zinatoka wapi na watu hao wasiojulikana ni watu wa aina gani, hivyo amewataka wananchi kuviachia vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi yake.

"Haya matukio tunaendelea kukabiliana nayo kama yale matukio ya Kibiti, kwanini matukio ya Kibiti hayaleti mshtuko mkubwa sana sasa wakati watu waliothirika ni wengi zaidi kuliko matukio ya sasa?

"Mimi sitaki kuingia huko lakini nasema vyombo vya ulinzi na usalama wakati wote vinakabiliana na matukio kadili yanavyojitokeza na ninaamini hali itakuwa shwali na sasa vinashughulika."

"Hoja ya msingi tunataka kujiridhisha silaha hizi zinatoka wapi? Hawa watu ni wa aina gani,sasa vyombo mviachie vifanye kazi yake msitoa majibu haraka" alisisitiza Mabeyo

Katika hatua nyingine,Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF), Jenerali Venance Mabeyo ametoa tahadhari kwa wananchi kwamba kuna matapeli wanaojifanya wanaajiri vijana kujiunga na jeshi.

Amesema watu hao wanadai fedha ili kuwasajili vijana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), jambo ambalo ni kinyume na taratibu za jeshi kuajiri vijana kwa JWTZ na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Mabeyo ameonya kwamba mtu yeyote atakayetapeliwa na watu hao basi naye atahesabika kama mmoja wa watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na kuchukuliwa hatua mara moja.

"Maongezi ya mtu na mtu hatuyatambui, ukitapeliwa nyamaza kimya kwa sababu ukilalamika kwetu na wewe utachukuliwa kama sehemu ya watoa rushwa," amesema Jenerali Mabeyo.

Mkuu huyo wa majeshi amebainisha njia mbalimbali ambazo wanazitumia kuajiri vijana jeshini kuwa ni kuwachukua wale waliopitia mafunzo ya JKT au pale wanapotaka watu wenye taaluma adimu kama vile madaktari, wahandisi au wanasheria.

Amebainisha kwamba jeshi linapokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na wanachukua hatua kila wanapopata taarifa ikiwa ni pamoja na kuwatafuta wahusika na kuwakamata.
 
"Kuna mmoja alikusanya vijana 15 na kila kijana akatakiwa kulipa Sh1 milioni. Aliwapangia chumba sehemu kisha akatoweka," amesema Mabeyo na kusisitiza kuwa wengi wanaofanya vitendo hivyo ni raia, wanajeshi ni wachache na wanachukuliwa hatua za kinidhamu mara moja