Saturday, 26 April 2025

Kiwango cha malaria mkoa wa Mara asilimia 15

 

Wito umetolewa kwa wananchi kuzingatia usafi wa mazingira na matumizi sahihi ya vyandarua ili kuepuka maambukizi ya malaria

Hayo yamesemwa leo na Dr Henry Lukamisa ambaye ni mratibu wa Malaria mkoa wa Mara wakati akizungumza kupitia Radio Mazingira fm ndani ya kipindi cha Asubuhi leo

Amesema hadi sasa kwa mkoa wa Mara kiwango cha ugonjwa wa malaria ni asilimia 15.

Dr Henry Lukamisa ambaye ni mratibu wa Malaria mkoa wa Mara

Dr Henry amesema ugonjwa wa malaria umeua watoto takribani 62 kwa mkoa wa Mara kwa mwaka 2024 kwa vifo vilivyorekodiwa hivyo ni vema wananchi wakachukua tahadhari

Dr Henry Lukamisa

Naye Mohamed Mlanza ambaye ni mratibu wa malaria halmashauri ya mji wa Bunda ambapo amesema kwa halmashauri hiyo wanajitahidi kutekeleza afua mbalimbali za kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria ikiwa ni pamoja na kugawa vyandarua kwa mama wajawazito na kwa akina mama wenye watoto wachanga.

Mohamed Mlanza ambaye ni mratibu wa malaria

Aidha Mlanza ameongeza kuwa mbali na kutoa vyandarua pia idara hiyo inatoa elimu kwa jamii juu ya namna unavyoenezwa na kusambaa pamoja na madhara ugonjwa huo.

Mohamed Mlanza

Ikumbukwe kuwa kila tarehe 25 April kila mwaka Dunia huadhimisha siku ya malaria ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu ni ” Malaria inatokomezwa na sisi, wekeza chukua hatua, ziro malaria inaanza na mimi”

Wednesday, 23 April 2025

Mwalimu jela miaka 30 kwa ubakaji, ulawiti

 

Mbali na kifungo cha miaka 30 pia mahakama imeamuru kulipa fidia ya shilingi milioni 2 kwa muhanga kwa mujibu wa sheria ya uendeshaji wa makosa ya jinai 348 (1) sura ya 20 marejeo ya mwaka 2022.

Na Adelinus Banenwa

Mahakama ya wilaya ya Bunda imemuhukumu kifungo cha miaka 30 jela na fidia ya shilingi milioni 2 Vicent Joseph Nkunguu (39) aliyekuwa mwalimu mkuu wa shule msingi masaunga wilayani Bunda kwa kosa la ubakaji na ulawiti wa mwanafunzi (16) wa darasa la sita ambaye jina lake limehifadhiwa.

Hukumu hiyo ya kesi ya jinai namba 7623 ya mwaka 2024 imetolewa leo tarehe 23 April 2025 na hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Bunda mhe Betron Sokanya

Akisoma hukumu hiyo Mhe Sokanya amesema mahakama imejiridhisha bila kuacha shaka kuwa mtuhumiwa Vicent Joseph Nkungu alitenda kosa hilo baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili ambapo upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi watano (5) na kielelezo kimoja huku upande wa utetezi ukiwasilisha mashahidi wawili (2) bila kielelezo chochote.

Mhe Sokanya amesema katika kosa la kwanza la ubakaji mahakama imemtia hatiani kutokana na mshitakiwa huyo kutenda kosa angali akijua ni kinyume na kifungu cha 130 (1) (2)( e) na kifungu cha 131 (1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura 16 marejeo ya mwaka 2022

Aidha katika kosa la pili la kulawiti Mhe Sokanya amesema mahakama imemkuta mshitakiwa na hatia kinyume na kifungu cha cha 154 (1) (a) cha kanuni ya adhabu sura 16 marejeo ya mwaka 2022.

Mbali na kifungo cha miaka 30 pia mahakama imeamuru mshitakiwa Vicent kulipa fidia ya shilingi milioni 2 kwa muhanga kwa mujibu wa sheria ya uendeshaji wa makosa ya jinai 348 (1) sura ya 20 marejeo ya mwaka 2022.

Awali Mwendesha mashtaka wa serikali Isiaka Ibrahim Mohamed alisema matukio hayo yalitendeka tarehe 9 March 2024 nyumbani kwa mshitakiwa huku mwendesha mashtaka akiiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili liwe fundisho kwake na kwa wengine wenye tabia kama zake

Katika utetezi wake mshitakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ni mara yake ya kwanza kukutwa na hatia pia ana mke na watoto wanaomtegemea.

Mhe hakimu Sokanya amesema rufaa ipo wazi kwa hukumu hiyo.

Tuesday, 22 April 2025

Radio jamii zanolewa kumulika nafasi ya wanawake uchaguzi mkuu 2025

 

Picha ya pamoja washiriki wa mafunzo kwa radio jamii Tanzania yaliyotolewa na TAMWA kwa kushirikiana na TADIO jijiji Dodoma

Licha ya sensa ya watu na makazi ya 2022 kuonesha idadi ya wanawake ni wengi kuliko wanaume, katika nafasi za uongozi kwa ngazi za udiwani na ubunge bado kuna idadi ndogo zaidi ya uwakilishi.

By Edward Lucas

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania TAMWA kwa kushirikiana na TADIO wameendesha mafunzo kwa radio za kijamii Tanzania Bara kuandaa habari na vipindi vitakavyowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu hasa kwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa 2025.

Akizungumzia mafunzo hayo, Meneja Mipango na Mikakati TAMWA, Sylivia Daulinge amesema mafunzo hayo yanayodhaminiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Vyombo vya Habari Finland VIKES yamelenga elimu ya namna bora ya kuandaa vipindi vya usawa na ujumuishi wa masuala ya kijinsia kwa kuhakikisha wanawake hasa vijana na makundi maalumu yanapewa kipaumbele kuelekea uchaguzi mkuu.

Sylivia Daulinge, Meneja Mipango na Mikakati TAMWA
Sylivia Daulinge, Meneja Mipango na Mikakati TAMWA

Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Radio Tadio, Hilali Alexander Ruhundwa amesema kwa kushirikiana na TAMWA wameona wanajukumu la kufanya katika jamii kwa kuwashirikisha waandishi wa habari ili kufikisha elimu kwa jamii kuwafanya wanawake washiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao

Hilali Alexander Ruhundwa, Mkufunzi wa mafunzo kutoka Radio Tadio akieleza kuhusu malengo ya mafunzo kwa radio za jamii kuelekea uchaguzi wa 2025
Sauti ya Hilali Alexander Ruhundwa

Kwa takwimu za uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2020, madiwani wanawake waliochaguliwa kwenye kata ni 260 kati ya 3,953 ambao ni sawa na asilimia 6.58 na kwa upande wa ubunge kati ya majimbo 264 wabunge wanawake waliochaguliwa kwenye majimbo ni 26 tu sawa na asilimia 9.85

Wednesday, 16 April 2025

Nyamo-hanga azikwa leo kwao Bunda

 

Ni aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa TANESCO aliyefariki kwa ajali ya gari eneo la nyatwali Bunda

Na Adelinus Banenwa

Shughuli ya mazishi ya aliyekuwa mkurugenzi wa TANESCO Boniface Gissima Nyamo-hanga inaendelea nyumbani kwake Mtaa wa Migungani kata ya Bunda stoo Bunda mjini mkoani Mara .

Ibada ya Mazishi ikiongozwa na Askofu Mwita Maguge wa kanisa la kiinjiri la kirutheli Tanzania KKKT dayosisi mkoani Mara.

Katika ujumbe wake kwenye ibada hiyo askofu Mguge amesema hakuna mtu anayeweza kukikimbia kifo hata kama una ulinzi wa namna gani kifo kitakufuata.

Viongozi mbalimbali wamefika katika shughuli hizo zinaongozwa na Naibu waziri mkuu na waziri wa Nishati Mhe Dotto Biteko ambapo pia amesema tanesco na na taifa kwa ujumla limempoteza mtu muhimu sana ambaye mara zote alikuwa si mtu wa kulalamika bali akiona tatizo basi anatoa na njia ya kutatua tatizo hilo.

Akisoma wasifu wa marehemu Gissima Nyamo-hanga, Irene Gowele afisa mawasiliano TANESCO amesema Mhandisi Gissima alizaliwa tarehe 10 Sept 1969 mkoani Mara huku akishika nyadhifa mbalimbali za uongozi ikiwemo mkurugenzi mkuu wa REA  kati ya mwaka 2016 hadi 2019, wakala wa ujenzi Tanzania. TBA na baadae kuwa Mkurugenzi mtendaji wa TANESCO Tanzania ambapo hadi umauti alikuwa akitumika katika nafasi hiyo

Mhandisi Boniface Gissima Nyamo-hanga ameacha wajane wawili na watoto 15.

Ikumbukwe Mhandisi Nyamo-hanga alifariki dunia April 13, 2025 katika ajali ya gari eneo la Nyatwali Bunda