Tuesday, 26 September 2023

WWF yashirikiana na wadau kupima maji mto Tigite- Tarime

 

mtaalam kutoka shirika la WWF akiwa katika hatua ya kupimaubora wa maji. Picha na Thomas Masalu

Shirika la WWF kwa kushirikiana na bonde la ziwa Victoria wamefanya zoezi la kupima maji ya mto Tigite uliopo Kijiji cha Matongo Kata ya Matongo wilaya ya Tarime ili kubaini afya ya mto huo katika vigezo vya asili na vya kisayansi.

Na Thomas Masalu

Shirika la WWF kwa kushirikiana na bonde la ziwa Victoria wamefanya zoezi la kupima maji ya mto Tigite uliopo Kijiji cha Matongo Kata ya Matongo wilaya ya Tarime ili kubaini afya ya mto huo katika vigezo vya asili na vya kisayansi.

Zoezi hilo limefanyika leo 26 Sept 2023 ambapo limeshirikisha wadau mbalimbali kama vile vikundi vya watumia maji, wapimaji wa afya ya mto ngazi ya jamii, wanafunzi wa shule ya secondary Matongo na baadhi ya walimu wa shule hiyo.

wadau wakiwa katiaka hatua za upimaji wa maji, Picha na Thomas Masalu

Zoezi lilianza kwa wadau kupewa elimu katika kutambua umuhimu wa upimaji wa maji ya mto, afya ya mto na vifaa vinayotumika kupimia maji ya mto.

Pamoja na hayo wadau walionyeshwa hatua ya kwanza ya upimaji hadi hatua ya mwisho ya upimaji hali iliyo onyesha kufurahiwa na wadau kutokana na kupata maarifa mapya katika utuzanji wa vyanzo vya maji.

Thursday, 14 September 2023

Maadhimisho ya 12 ya Mto Mara yazinduliwa rasmi leo


Mkuu wa mkoa wa Mara, Said Mtanda (wa kwanza kulia) akiwa ametembelea Banda la WWF katika viwanja vya Sokoine Maadhimisho ya Siku ya Mto Mara

Mamlaka za serikali na wadau wengine wa Mazingira wametakiwa kudhibiti matumizi ya maji yasiyoendelevu na kudhibiti vyanzo vya maji ili kuulinda Mto Mara


Na Edward Lucas

Maadhimisho ya 12 ya siku ya Mto Mara yamezinduliwa rasmi leo katika Viwanja vya Sokoine mjini Mugumu Wilaya ya Serengeti mkoani Mara huku wananchi wakitakiwa kuendelea kuutunza Mto Mara kwa kizazi endelevu.


Akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho hayo, Mkuu wa mkoa wa Mara, Said Mtanda ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi amesema maadhimisho hayo yanafanyika kufuatia uamuzi wa Baraza la Mawaziri kutoka Serikali ya Tanzania na Kenya yaliyopitishwa mwaka 2012 ili kuwa na siku maalumu kila mwaka kwa lengo la kuelimisha na kuhamasisha wananchi wa nchi zote mbili kuhifadhi Mto Mara.

Said Mtanda, Mkuu wa Mkoa wa Mara

Katika Maadhimisho haya yenye kauli mbiu isemayo “Hifadhi Mto Mara kwa Ustawi wa Viumbe Hai na Uchumi Endelevu” yanakuwa ni ya 6 kufanyika upande wa Tanzania kati ya 12 huku eneo la Mugumu yakiwa yanafanyika kwa mara ya 3 sasa.


Mtanda amesema pamoja na fursa nyingi zilizopo katika bonde la Mto Mara pia limekuwa likikutana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchafuzi na uharibifu wa vyanzo vya maji kutokana na shughuli za kilimo na ufugaji katika maeneo ya mto.


Amewataka wananchi kuacha vitendo hivyo vinavyoharibu vyanzo vya maji huku akiziagiza mamlaka za serikali na wadau wengine wa Uhifadhi wa Mazingira kusimamia sheria na taratibu zingine zilizoanzishwa ili kuulinda Mto Mara.

Said Mtanda, Mkuu wa mkoa wa Mara

Kilele Cha Maadhimisho ya 12 kitakuwa ni tarehe 15 Septemba 2023 ambapo wadau mbalimbali kutoka Tanzania na Kenya wanashiriki kuonesha huduma na bidhaa mbalimbali katika viwanja vya Sokoine Wilaya ya Serengeti 

Wednesday, 13 September 2023

Mtanda awapongeza WWF kwa Uhifadhi wa Mto Mara


Mkuu wa mkoa wa Mara, Said Mtanda akiendesha zoezi la upandaji miti na uwekaji wa bikoni kando ya bonde la Mto Mara

Na Edward Lucas

Mkuu wa mkoa wa Mara, Said Mtanda amelipongeza Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira WWF na wadau wengine katika juhudi wanazozifanya katika kuulinda Mto Mara

Mtanda ametoa kauli hiyo leo wakati wa zoezi la upandaji wa miti na uwekaji wa bikoni au vigingi kandokando ya mto Mara katika kijiji cha Borenga Wilaya ya Serengeti katika kuadhimisha siku ya Mto Mara.

Sauti ya Mhe. Mtanda akiwapongeza WWF na wadau wengine kwa Uhifadhi wa mto Mara

Katika zoezi hilo linalotekelezwa maeneo mbalimbali kwenye mkondo wa bonde la Mto Mara, WWF kwa ufadhili wa USAID wamekusudia kupanda miche 44,000 na kuweka vigingi 50 ili kuweka alama zitakazosaidia wananchi kutofanya shughuli zao ndani ya mita 60 katika bonde la mto.


Awali akisoma taarifa fupi ya Uhifadhi wa bonde la Mto Mara, Afisa Mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Helga Enock Nkongoki amesema jumla ya miti 5000 imeshapandwa eneo la la Nyasurura na Marenge huku miche 500 iliyotolewa na WWF ikipandwa leo eneo la Borenga Serengeti.

Helga Enock Nkongoki akisoma risala ya utekelezaji wa zoezi la upandaji wa miti na uwekaji wa bikoni
Viongozi na wananchi wakishiriki zoezi la upandaji wa miti 500 eneo la cha Borenga Wilaya ya Serengeti

Zoezi la Upandaji wa Miti katika bonde la Mto Mara linaendelea


Viongozi kutoka idara na taasisi mbalimbali wakishirikiana na wananchi kupanda miche na kuweka bikoni kando ya bonde la Mto Mara

Na Edward Lucas

Viongozi kutoka WWF kwa kushirikiana na taasisi zingine pamoja wananchi wameshirikiana kwa pamoja kupanda miche kandokando ya bonde la Mto Mara eneo la kijiji cha Borenga Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Tuesday, 12 September 2023

WWF: ‘Mto Mara ulindwe na Utunzwe’


Sehemu ya banda la WWF katika viwanja vya Sokoine Wilaya ya Serengeti maadhimisho ya 12 ya Mto Mara

Kupitia Maadhimisho ya 12 ya siku ya Mto Mara, Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira WWF limeeleza mikakati linayoifanya kuulinda Mto Mara.

Na Edward Lucas

Wananchi mkoani Mara wametakiwa kuendelea kutunza rasilimali ya Mto Mara ili kuifanya kuwa endelevu.

Wito huo umetolewa na Mratibu wa Mradi WWF mkoa wa Mara, Damas Mbaga wakati akizungumza na Radio Mazingira Fm katika viwanja vya Sokoine Wilaya ya Serengeti mkoani Mara katika Maadhimisho ya 12 ya Mto Mara ameeleza ni kwa namna gani wanafanya kuulinda Mto Mara.

Mahojiano ya Mazingira Fm na Mratibu wa Mradi WWF katika Maadhimisho ya 12 ya Mto Mara