Mamlaka za serikali na wadau wengine wa Mazingira wametakiwa kudhibiti matumizi ya maji yasiyoendelevu na kudhibiti vyanzo vya maji ili kuulinda Mto Mara
Na Edward Lucas
Maadhimisho ya 12 ya siku ya Mto Mara yamezinduliwa rasmi leo katika Viwanja vya Sokoine mjini Mugumu Wilaya ya Serengeti mkoani Mara huku wananchi wakitakiwa kuendelea kuutunza Mto Mara kwa kizazi endelevu.
Akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho hayo, Mkuu wa mkoa wa Mara, Said Mtanda ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi amesema maadhimisho hayo yanafanyika kufuatia uamuzi wa Baraza la Mawaziri kutoka Serikali ya Tanzania na Kenya yaliyopitishwa mwaka 2012 ili kuwa na siku maalumu kila mwaka kwa lengo la kuelimisha na kuhamasisha wananchi wa nchi zote mbili kuhifadhi Mto Mara.
Katika Maadhimisho haya yenye kauli mbiu isemayo “Hifadhi Mto Mara kwa Ustawi wa Viumbe Hai na Uchumi Endelevu” yanakuwa ni ya 6 kufanyika upande wa Tanzania kati ya 12 huku eneo la Mugumu yakiwa yanafanyika kwa mara ya 3 sasa.
Mtanda amesema pamoja na fursa nyingi zilizopo katika bonde la Mto Mara pia limekuwa likikutana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchafuzi na uharibifu wa vyanzo vya maji kutokana na shughuli za kilimo na ufugaji katika maeneo ya mto.
Amewataka wananchi kuacha vitendo hivyo vinavyoharibu vyanzo vya maji huku akiziagiza mamlaka za serikali na wadau wengine wa Uhifadhi wa Mazingira kusimamia sheria na taratibu zingine zilizoanzishwa ili kuulinda Mto Mara.
Kilele Cha Maadhimisho ya 12 kitakuwa ni tarehe 15 Septemba 2023 ambapo wadau mbalimbali kutoka Tanzania na Kenya wanashiriki kuonesha huduma na bidhaa mbalimbali katika viwanja vya Sokoine Wilaya ya Serengeti
No comments:
Post a Comment