Thursday, 27 February 2025

 

Kampeni ya chakula shuleni yapelekea shule 11 bunda tc kufuta daraja 0

27 February 2025, 

Mhe Mbunge wa jimbo la Bunda mjini Mhe Robert Chacha Maboto akiwa katika moja ya shule za sekondari Bunda mjini katika ziara yake ya kuhamasisha chakula shuleni.

Yapo mabadiliko makubwa ya kitaaluma tangu sera ya wanafunzi kupata chakula shuleni ambapo kati shule 17 za sekondari za halmashauri ya mji wa Bunda shule 11 zimefanikiwa kufuta daraja sifuri kwa matokeo kidato cha nne.

Na Adelinus Banenwa

Mbunge wa jimbo la Bunda mjini Mhe Robert Chacha Maboto amewataka wazazi wa wanafunzi katika jimbo la Bunda mjini kufanya kila linalowezekana kuhakikisha wanachanga chakula cha wanafunzi shuleni kama wanahitaji matokeo mazuri kwa watoto wao.

Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 26 Feb 2025 katika siku ya tatu ya ziara yake iliyokuwa inalenga kuhamasisha chakula shuleni huku katika siku hizo tatu Mhe mbunge ametembelea jumla ya shule za sekondari 16.

Mhe Robert Chacha Maboto mbunge wa jimbo la Bunda mjini akisalimiana na moja ya wanafunzi shule ya sekondari Nyiendo alipofika katika ziara yake ya kuhamasisha chakula mashuleni

Mhe Maboto amesema hakuna ambaye hafahamu juu ya ugumu wa maisha lakini suala la chakula shuleni ni jambo la mzazi kuelewa na kuamua endapo anataka matokeo mazuri ya mtoto hasa kitaaluma hivyo kila mzazi anao wajibu wa kitimiza majukumu yake.

Sauti ya Mhe Robert Chacha Maboto mbunge jimbo la Bunda mjini

Afisa lishe halmashauri ya mji wa Bunda Bi Lucy Erasto Mwalwayo amesema yapo madhara mbalimbali ya muda mrefu ambayo yatampata mtoto endapo atakaa muda mrefu bila kupata chakula shuleni ambapo amesema madhara hayo ni pamoja na kuwa na tabia ya kuishiwa damu pindi atakapofikia kipindi cha kuzaa kwa watoto wa kike, upungufu wa nguvu za kiume kwa watoto wa kiume, vidonda sugu vya tumbo pamoja na kupata saratani ya utumbo.

Sauti ya afisa lishe halmashauri ya mji wa Bunda Bi Lucy Erasto Mwalwayo
Mhe Robert Chacha Maboto mbunge wa jimbo la Bunda mjini kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi shule ya sekondari Bunda alipofika kuhamasisha uchangiaji wa chakula mashuleni

Kwa upande wake Sauda Mwakyembe kaimu afisa elimu sekondari kwa upande wa halmashauri ya mji wa Bunda amesema yapo mabadiliko makubwa ya kitaaluma tangu sera ya wanafunzi kupata chakula shuleni ambapo kwa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2024 kwa shule zote 17 za sekondari za halmashauri ya mji wa Bunda shule 11 zimefanikiwa kufuta daraja sifuri kwa matokeo kidato cha nne.

Sauti ya Sauda Mwakyembe kaimu afisa elimu sekondari Bunda TC

Ikumbukwe katika ziara yake ya siku tatu aliyoifanya mbunge wa jimbo la Bunda mjini kwa jumla ya shule 16 za sekondari za Bunda mjini ametoa jumla ya magunia 65 ya mahindi na kilo 800 za maharage ikiwa ni kuunga mkono juhudi za wazazi kuchangia chakula cha wanafunzi shuleni ili kuongeza kiwango cha taaluma.

Wednesday, 26 February 2025

 

Wazazi Sazira na Sizaki Sec wapewa tano kwa wanafunzi wote kupata chakula shuleni

26 February 2025, 

Katika picha akionekana Mhe Robert Chacha Maboto mbunge jimbo la Bunda mjini katika shule tofauti alizozitembelea.

Mbunge wa jimbo la Bunda mjini Mhe Robert Chacha Maboto amewapongeza wazazi na waleza wa shule za sekondari za Sazira na Sizaki kwa kuchanga chakula cha wanafunzi shuleni.

Na Adelinus Banenwa

Mbunge wa jimbo la Bunda mjini Mhe Robert Chacha Maboto amewapongeza wazazi na waleza wa shule za sekondari za Sazira na Sizaki kwa kuchanga chakula cha wanafunzi shuleni na kufanya wanafunzi wote kupata chakula.

Mhe Mbunge ametoa shukra hizo katika ziara yake ikiwa ni siku ya pili ya ziara hiyo yenye lengo la kuhamasisha uchangiaji wa chakula cha wanafunzi mashuleni ili kuongeza ufaulu.

Wanafunzi shule ya sekondari Sizaki wakionesha furaha baada ya kupokea chakula kutoka kwa Mbunge jimbo la Bunda mjini Mhe Robert Chacha Maboto

Mhe Maboto amesema ili mwanafunzi aweze kupata ufaulu mzuri ni lazima mzazi na serikali pamoja na walimu kila mmoja kutimiza wajibu wake ambapo kazi kubwa ya mzazi ni kununua vifaa vya shule na kuchangia chakula shuleni tu.

Amewataka wazazi wa maeneo mengine ndani ya jimbo la Bunda mjini kuiga mifano na mbinu wanazozitumia wazazi wa sazira na sizaki ili kuhakikisha watoto wote wanapata chakula.

Naye mkuu washule ya sekondari ya Sizaki mwalimu Maeda amesema mbinu pekee wanayoitumia kuhamasisha wazazi ni kuwaeleza umuhimu wa chakula kwa wanafunzi pia upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi wote umewezesha kupata ufaulu kati ya daraja la 1 ha 4 na kufuta daraja 0

Nao wanafunzi katika shule alizozitembelea Mhe mbunge wamemshukuru huku wakiahidi kuendelea kuwahimiza wazazi waendelee kuchangia chakula muda wote.

Katika siku ya pili ya ziara yake Mhe mbunge Robert Maboto amezitembelea shule za sekondari za Bunda stoo, Migungani, Rubana, Kunzugu, Paul Jones, sizaki na shule ya Sekondari ya Sazira

Saturday, 22 February 2025

 

Pamba yavaliwa njuga Bunda, matarajio makubwa ya uzalishaji

22 February 2025,

katibu tawala wilaya ya Bunda Salumu Mtelela

Imeelezwa kuwa Serikali kupitia bodi ya pamba Tanzania imedhamilia wakulima wa zao hilo kulima kwa tija badala ya kulima mashamba makubwa lakini mavuno kidogo.

Hayo yamesemwa na mkaguzi wa zao la pamba wilayani Bunda Ndugu Hemedi Kabea mbele ya katibu tawala wa wilaya hiyo Ndugu Salumu Mtelela wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya kilimo cha zao la pamba wilayani Bunda na kujionea hali ya huduma zinazotolewa na bodi ya pamba kwa wakulima wa zao hilo.

Mkaguzi wa zao la pamba wilayani Bunda Ndugu Hemedi Kabea

Kabea amesema jitihada mbalimbali zimefanywa na serikali kupitia bodi ya pamba ili kuongeza tija katika uzalishaji wa zao hilo ambapo serikali imeleta mbegu za kutosha, dawa kwa maana ya viuadudu, vinyunyizi, matrekta, pamoja na Droni.

Sauti ya mkaguzi wa zao la pamba wilayani Bunda Ndugu Hemedi Kabea

Naye katibu tawala wilaya ya Bunda Salumu Mtelela ameishukuru bodi ya pamba kwa kuendelea kusimamia zao la pamba ambalo ni miongoni mazao mkakati kwa wilaya ya Bunda

Katibu tawala akizungumza na wananchi katika maeneo ya mashamba amesema wilaya ya Bunda kwa msimu huu wa kilimo inatakiwa kuzalisha tani elfu 20 sawa anasilimia 67% ya pamba yote inayotakiwa kuzalishwa katika mkoa wote wa Mara hali hiyo inaifanya wilaya ya Bunda kuwa wilaya kinara katika uzalishaji wa zao la Pamba kimkoa.

katibu tawala wilaya ya Bunda Salumu Mtelela

Mtelela amewapongeza wataalamu wa kilimo kwa kuendelea kubuni njia mbalimbali za kudhibiti wadudu kwenye mashamba zikiwemo njia za asili kama vile matumiszi ya mimea ya alizeti pamoja na tenolojia ya morasisi lakini amesema serikali pia imeleta droni tano wilayani Bunda ambazo zitasaidia katika kunyunyiza dawa kwenye mashamba ya wakulima kwa haraka na kwa muda mfupi

Mtelela ameendelea kuwarai viongozi wote pamoja na wananchi kujiepusha na hujuma zozote zile zinazosababisha hasara kwa serikali na zao lenyewe ikiwemo wizi wa viuadudu pamoja na uzembe katika kupulizia viuatilifu kwenye mashamba.

Sauti ya katibu tawala wilaya ya Bunda Salumu Mtelela
Baadhi ya viongozi na wananchi katika ziara ya pamba Bunda

Kwa upande wao wakulima wameipongeza serikali kwa kuendelea kuweka mkazo katika zao la pamba hasa katika usimamizi lakini wameitaka serikali kuwaletea viuadudu kwa wakati pia wametaja changamoto ya Mabadiliko ya tabia ya nchi kama kikwazo ikiwemo mvua kubwa na wakati mwingine ukame .

Thursday, 20 February 2025

 

Madiwani Bunda DC wakubali kupitisha bajeti ya Tsh, 36,5 bilion

20 February 2025, 

Makamu mwenyekiti wa halmashauriya Bunda DC Mhe Keremba Irobi

Baraza la Madiwani halmashauri ya wilaya ya Bunda limepitisha makadilio ya bajeti ya shilingi Bilion 36.5 kwa mwaka wa fedha 2025 na 2026

Na Adelinus Banenwa

Baraza la Madiwani halmashauri ya wilaya ya Bunda limepitisha makadilio ya bajeti ya shilingi Bilion 36.5 kwa mwaka wa fedha 2025 na 2026 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, mishahara ya watumishi, kulipa madeni, pamoja na matumizi mengine.

Bajeti hiyo imepitishwa leo tarehe 20 Feb 2025 katika baraza hilo liliketi kujadili ambapo pamoja na mambo mengine baraza hilo lilipitia mapendekezo ya kamati mbalimbali za halmashauri.

Kikao hicho kimeongozwa na makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo mhe Keremba Irobi.

Sauti ya makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo mhe Keremba Irobi
Viongozi wa halmashauri wakiongozwa na mwenyekiti wa halmashauri hiyo Mhe Magafu Manumbu katikati, mkurugenzi wa halmashauri stanley Mbilinyi kulia na makamu mwenyekiti wa halmashauri Mhe Keremba Irobi

Katika ushauri wao madiwani hao wameshauri mkurugenzi pamoja na wataalamu kuzingatia maoni ya kamati katka utekelezaji wa miradi ikiwa ni pamoja na kupeleka huduma mahala ambapo hazipo kama katika  sekta za  Elimu na Afya.

Sauti za maoni ya baadhi ya madiwani kuhusu bajeti
Katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela

Kwa upande wake katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela ameipongeza halmashauri hiyo kwa ukusanyaji mzuri wa mapato ambapo amesema kwa mwaka wa fedha 2023 na 2024 halmashauri hiyo ilikusanya zaidi ya malengo.

Mtelela amewahimiza watumishi wa halmashauri hiyo wakiongozwa na mkurugenzi kuendelea kukusanya mapato pia kumaliza miradi ambayo inaendelea kutekelezwa katika halmashauri hiyo.

Sauti ya katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela
Baadhi ya madiwani katika baraza la Bunda DC

Wakati huo huo baraza hilo la madiwani halmashauri ya wilaya ya Bunda limepitisha mapendekezo ya Bajeti ya Wakala wa  barabara za mijini na vijijini TARURA ya shilingi bilion 7.6 ikijumuisha fedha za upanuzi wa barabara milioni 800 fedha za mfuko wa jimbo bilion 1 na Fedha za tozo ya mafuta bilion 2.

Sauti ya makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo mhe Keremba Irobi

Akizungumza katika baraza hilo kaimu meneja TARURA Bunda  Muhandisi Hamad Munisi amesema endapo  fedha hizo zikipitishwa  zinakwenda kutekeleza hatua mbalimbali ikiwemo ujenzi wa makarvati, ufunguaji wa barabara mpya, ujenzi wa barabara za lami na ujenzi wa mitaro.

kaimu meneja TARURA Bunda  Muhandisi Hamad Munisi

 

NHIF yaja na vifurushi vipya kuongeza wigo wa matibabu kwa wateja

20 February 2025, 

Afisa Wanachama Mwandamizi NHIF mkoa wa Mara, Felister Renatus,(picha na Edward Lucas)

Jamii yatakiwa kuwa na utamaduni wa kukata bima ya afya kabla ya kuugua ili kuepuka changamoto mbalimbali za kupata huduma

By Edward Lucas,

NHIF yaja na kifurushi cha NGORONGORO AFYA na SERENGETI AFYA ili kuongeza wigo wa matibabu kwa wateja na kutoa punguzo la asilimia 10 ya mchango wa wategemezi kwa kujiunga na familia

Akizungumzia mpango huo kupitia Radio Mazingira Fm, Afisa Wanachama Mwandamizi NHIF mkoa wa Mara, Felister Renatus amesema kwa vifurushi vilivyokuwepo awali vilikuwa na kikomo cha matibabu lakini kwa vifurushi hivi vipya vimeongeza wigo zaidi wa matibabu nchi nzima katika vituo vya matibabu zaidi ya elfu 10 walivyovisajili kwa ngazi ya zahanati hadi taifa

Sauti ya Felister Renatus, Afisa Wanachama Mwandamizi NHIF mkoa wa Mara

Akitoa mfano wa huduma zilizoongezwa katika vifurushi vipya ni pamoja na huduma za kuchuja damu, huduma za saratani, kuboresha zaidi huduma za upasuaji mkubwa na mdogo, maboresho ya huduma za vipimo kama CT Scan na MRI pamoja na huduma za uzazi

Felister Renatus, Afisa NHIF Mara akitaja huduma
Felister Renatus, Afisa Wanachama Mwandamizi NHIF mkoa wa Mara (picha na Edward Lucas)

Aidha Bi, Felister amesema NHIF imezindua na kurejesha huduma ya Toto Afya Kadi ambayo ilizuiliwa kwa muda ili kufanya maboresho ambapo baada ya maboresho huduma hiyo imerejea rasmi hivyo amewaasa wazazi kukata huduma hiyo kwa ajili ya watoto wao

Felister Renatus

Kwa upande wake Mhasibu Mwandamizi NHIF Mkoa wa Mara, Vistus Tilusasila ameiasa jamii kuwa na utamaduni wa kukata bima ya afya kabla ya kuugua ili kuepuka changamoto mbalimbali za kupata huduma

Vistus Tilusasila, Mhasibu Mwandamizi NHIF mkoa wa Mara (Picha na Elia Martine)
Vistus Tilusasila

Sunday, 16 February 2025

 

Wagonjwa 1,520 wahudumiwa bure katika kambi ya macho Bunda

16 February 2025, 

rais wa Chama cha Lions Clubs International, Mahamoud Rajuan,

Zaidi ya Wagonjwa 1,520 Wahudumiwa Bure Katika Kambi ya Matibabu ya Macho Bunda Manyamanyama.

Na Adelinus Banenwa

Zaidi ya wagonjwa 1,520 wa macho wamehudumiwa ndani ya siku mbili kati ya tatu katika kambi maalumu ya matibabu ya macho iliyofanyika katika Hospitali ya Bunda Manyamanyama.

Akizungumza katika kambi hiyo, rais wa Chama cha Lions Clubs International, Mahamoud Rajuan, amesema kati ya wagonjwa hao, 150 wamefanyiwa upasuaji wa macho kutokana na changamoto mbalimbali walizokuwa nazo, ikiwa ni pamoja na mtoto wa jicho.

Baadhi ya wagonjwa waliopata huduma katika kambi ya macho ikiwemo kufanyiwa upasuaji

Mahamoud amewashukuru wananchi kwa kujitokeza na pia kuwashukuru wafadhili waliowezesha kufanyika kwa kambi hiyo, ambapo huduma zilikuwa bure.

Sauti ya rais wa Chama cha Lions Clubs International, Mahamoud Rajuan,
Dr. Majey Majey, mganga anayehusika na huduma za matibabu ya macho

Naye, Dr. Majey Majey, mganga anayehusika na huduma za matibabu ya macho na vipimo, amesema kwa siku hizo mbili wamewahudumia wagonjwa 1,520 na wanashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kupata matibabu.

Dr. Majey ameeleza kuwa matatizo ya macho yanaweza kusababishwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo aleji, mtoto wa jicho, presha ya macho, vumbi, moshi, na mengine, na hivyo wanatoa ushauri kulingana na chanzo cha ugonjwa wa kila mgonjwa.

Sauti ya Dr. Majey Majey, mganga anayehusika na huduma za matibabu ya macho
Baadhi ya wagonjwa waliopata huduma katika kambi ya macho ikiwemo kufanyiwa upasuaji

Kwa upande wao, baadhi ya wagonjwa waliopata huduma katika kambi ya siku tatu wamewashukuru kwa huduma walizopata, kwani hawakudaiwa fedha yoyote kuanzia kwenye vipimo hadi upasuaji.

Kambi hiyo ya matibabu ya macho katika Hospitali ya Bunda Manyamanyama ilianza tarehe 14 Februari na kumalizika leo, tarehe 16 Februari 2025, huku matibabu yaliyotolewa ikiwa ni pamoja na huduma za vipimo, ugawaji wa miwani ya jua na kusomea, pamoja na upasuaji, yote hayo yakitolewa bure.

Saturday, 15 February 2025

 

Wavamia mtaa wa Zanzibar kufuatia kugunduliwa kwa dhahabu, serikali yatia mguu

15 February 2025, 

Baadhi ya wananchi waliojikusanya kwenye eneo ilipoibuka rashi ya dhahabu

Serikali ya mtaa inachukua hatua muhimu katika kusimamia usalama na ustawi wa jamii katika kipindi hiki cha shughuli za uchimbaji.

Na Adelinus Banenwa

Makumi kwa mamia ya vijana  kutoka maeneo mbalimbali wameshukudiwa katika viunga vya mtaa wa Zanzibar , kata ya Nyasura, halmashauri ya mji wa  Bunda, kutokana na kuibuka kwa rashi ya madini ya dhahabu katika eneo hilo kwa lengo la kuanza shughuli za uchimbaji.

Mwenyekiti wa mtaa wa Zanzibar, Nyabatuli Ndege, amesema kuwa serikali ya mtaa inachukua hatua muhimu katika kusimamia usalama na ustawi wa jamii katika kipindi hiki cha shughuli za uchimbaji.

Baadhi ya wananchi waliojikusanya kwenye eneo ilipoibuka rashi ya dhahabu

Nyabatuli amesema kuwa wanahakikisha kuwa kuna usafi, maeneo ya chakula yamewekwa mbali na maeneo ya uchimbaji, na uchimbaji wa vyoo umeanzishwa ili kudumisha afya na usalama kutokana na  wingi wa watu wanaokusanyika.

Sauti ya Mwenyekiti wa mtaa wa Zanzibar, Nyabatuli Ndege

Naye mtendaji wa mtaa wa Zanzibar, Bi. Grece Mwita, ameeleza kuwa halmashauri tayari imeanza kukusanya mapato kutoka kwa wachimbaji, ambapo kila kiroba cha mchanga kinachopakiwa kinatozwa shilingi 1000.

Baadhi ya wananchi waliojikusanya kwenye eneo ilipoibuka rashi ya dhahabu

Grece amesisitiza kuwa ni muhimu kwa wachimbaji kufuata utaratibu wa kisheria na kulipa mapato kwa mujibu wa sheria.

Sauti ya mtendaji wa mtaa wa Zanzibar, Bi. Grece Mwita

Aidha, Maiga James Majanjala, mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wa madini wi, ametoa wito kwa vijana wote kuwa watulivu na kuzingatia sheria za uchimbaji.  Huku akiwahakikishia kuwa viongozi wa wachimbaji wako mstari wa mbele kuhakikisha utaratibu unafuatwa ili kuepuka migogoro na madhara yoyote.

Sauti ya

Awali akizungumza na Mazingira fm moja ya vijana wa mwanzo kugundua uwepo wa dhahabu katika eneo hilo la Zanzibar amesema eneo hilo kwa kawaida walikuwa wanalitumia kuchimba kokoto na molamu lakini siku ya ijumaa jioni ndipo walipoona mawe yenye chembechembe za madini ya dhahabu na walipokwenda kuyasaga alipata gram 3.5 ndipo alianza kuwapa taarifa wengine

Sauti ya Mangaro Stima moja ya vijana wa mwanzo kugundua uwepo wa dhahabu

Friday, 14 February 2025

 

Radio Mazingira FM yapongezwa kwa utendaji kazi mzuri

14 February 2025, 

Mkuu wa wilaya ya Musoma Juma Chikoka alipokuwa akizungumzia siku ya radio,(picha na Shomari)

Mkuu huyo wa wilaya ya Musoma amekipongeza kituo cha redio cha Mazingira Fm cha mjini Bunda kwa kazi nzuri za kuendelea kuwafikishia wananchi taarifa mbalimbali.

Na.Shomari Binda

Katika kuadhimisha siku ya radio duniani jamii imetakiwa kufatilia matangazo yake ili kuweza kupata taarifa mbalimbali zikiwemo za utekelezaji wa miradi ya serikali.

Kauli hiyo imetolewa februari 13,2025 na mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka alipokuwa akiizungumzia siku hiyo.

Amesema redio ni chombo muhimu na kinachopaswa kufatiliwa hivyo wananchi wanakumbushwa kufatilia matangazo yanayotolewa

Chikoko amesema ipo miradi inayotekelezwa na serikali katika Wilaya ya Musoma na maeneo mengine ya nchi na moja ya vyanzo vya kupata taarifa ni kupitia redio

Mkuu huyo wa Wilaya ya Musoma amekipongeza kituo cha redio cha Mazingira Fm cha mjini Bunda kwa kazi nzuri za kuendelea kuwafikishia wananchi taarifa mbalimbali.

Chikoka kupitia siku hii ya redio duniani amewapongeza watangazaji wa Mazingira Fm kwa kazi wanayoifanya ya kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata taarifa