Monday, 9 June 2025

Wazee 2 hadi 3 kati ya 10 hufanyiwa ukatili Bunda

 

Afisa ustawi wa jamii halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara Waryoba Juma

Baadhi ya wazee wameitaka serikali iwatambue wazee kwamba wapo, pia iwahudumie hasa katika sera ya matibabu bure kwa wazee maana wakati mwingine hukosa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya

Na Adelinus Banenwa

Imeelezwa kuwa wazee wawili (2)hadi watatu (3) kati ya wazee kumi (10) halmashauri ya mji wa Bunda hufanyiwa ukatili mbalimbali katika jamii na familia.

Hayo yamesemwa leo na afisa ustawi wa jamii halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara Waryoba Juma ambapo amesema takwimu hizo siyo nzuri lakini pia siyo mbaya ukilinganisha na maeneo mengine nchini.

Waryoba amesema ukatili wanaokutana nao wazee ni pamoja na kubaguliwa, kunyanyaswa, kutosikilizwa na wakati mwingine wazee wanapigwa  matukio ambayo matukio haya yanagawanyika katika makundi mawili ya unyanyasaji ambayo ni kimwili na kisaikolojia.

Waryoba ameyasema hayo katika kikao kilichowakutanisha wazee kutoka mitaa ya kata ya Sazira walipokuta na viongozi wa baraza la ushauri la wazee halmashauri ya mji wa Bunda.

Sauti ya Waryoba Juma

Kwa upande wao baadhi ya wazee wameitaka serikali iwatambue wazee na kwamba wapo pia iwahudumie hasa katika sera ya matibabu bure kwa wazee maana wakati mwingine hukosa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya pia watoto wao kushindwa kuwalea na badala yake huwarundikia wajukuu nyumbani bila utaratibu.

Baadhi ya wazee waliohudhulia kikao cha wazee Sazira
Sauti ya baadhi ya wazee

Naye Machael Kweka ambaye ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda na diwani wa kata ya Sazira  ameiomba serikali  kuleta mpango wa kulipa pensheni kwa wazee wa Tanzania bara kama inavyofanyika huko Zanzibar na lingine watoto wenye kazi kuhakikisha wanawakatia bima za matibabu wazee wao.

Sauti ya Michael Kweka

Sunday, 8 June 2025

Auawa na tembo akilinda shamba la Nyanya Bunda

 

Alikuwa analinda mazao yake yasiliwe na tembo na ndiyo kawaida yetu maana bila kulinda huwezi kuvuna chochote.

Na Adelinus Banenwa

Kijana mmoja aliyetambulika kwa jina la Kinyunyi Nyakile mkazi wa mtaa wa Ichamu kata ya Kunzugu Halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara amepteza maisha baada ya kushambuliwa na tembo wakati akilinda bustani yake ya nyanya.

Tukio hilo linatajwa kutokea usiku wa kuamkia Juni 8, 2025 ambapo inaelezwa kundi la tembo zaidi ya watano walifika karibu na mashamba ya wakulima hapo Kunzugu ndipo wakulima walianza kuwafukuza lakini tembo mmoja aligeuka na kuanza kuwakimbiza hadi alipomshika Kinyunyi na kumkanyaga vibaya hali iliyopelekea kupoteza maisha.

Mwenyekiti wa mtaa wa Ichamu James Magwayega Haruna ameiambia mazingira fm kuwa tukio hilo limewasikitisha kutokana na kupoteza nguvu kazi ya mtaa na imekuwa kawaida kwa wakazi wa mtaa wake ili wavune mazao yao ya shambani ni lazima kulinda.

Sauti ya Mwenyekiti wa mtaa wa Ichamu James Magwayega Haruna

Kwa upande wake Magambo Magambo ambaye ni baba mdogo wa marehemu Kinyunyi amesema kama familia wamepoteza mtu muhimu sana hasa ukizingatia alikuwa bado mdogo na alikuwa hajawa na familia Aidha ameiomba serikali kujenga uzio kuzuia wanyama hao ili kunusuru maisha ya wananchi na mazao.

Sauti ya Magambo Magambo ambaye ni baba mdogo wa marehemu

Naye diwani wa kata ya Kunzugu Mhe Pasaka Samson amesema taarifa za mwananchi wake alizipata usiku ambapo alichukua hatua ya kwenda hadi eneo la tukio kisha aliwasiliana na mamlaka mbalimbali ikiwemo watu wa Kikosi dhidi ya ujangiri KDU, Jeshi la polisi pamoja na ofisi ya mkuu wa wilaya.

Mhe Pasaka amesisitiza kuwa serikali ione umuhimu wa kuongeza gari la doria kwa kuwa lililopo halitoshi kuanzia Balili hadi Tungirima ambao ni ukanda wote wa hifadhi ya taifa ya Serengeti.

Sauti ya diwani wa kata ya Kunzugu Mhe Pasaka Samson

Friday, 6 June 2025

Wafugaji kufanya kongamano kubwa June, 15 na 16

 

Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Ndugu Mrida Mshota

Watu zaidi ya laki moja wakitalajiwa kuudhulia katika kongamano hilo

Na Thomas Masalu

Chama cha Wafugaji Tanzania kimetangaza kufanyika kwa kongamano maalum la siku mbili litakalofanyika tarehe 15 na 16 Juni mwaka huu, katika viwanja vya nane nane , Nyakabindi mkoani Simiyu huku watu zaidi ya laki moja wakitalajiwa kuudhulia katika kongamano hilo linalolenga uzinduzi wa chanjo ya mifugo na utambuzi pamoja na kujadili changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya ufugaji nchini.

Akizungumza na Redio Mazingira FM, leo tarehe 6/6/2025 kupitia kipindi cha Duru za Habari, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Ndugu Mrida Mshota, amesema kuwa maandalizi ya kongamano hilo yanaendelea vizuri.

Aidha mwenyekiti huyo wa chama cha wafugaji Tanzania Mrida Mshota ameeleza kuwa Mgeni Rasmi katika Kongamano hilo maaalum la siku mbili, anatarajiwa kuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Daktari Samia Suluhu Hassan,

Sauti ya Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Ndugu Mrida Mshota

Huku akiongeza kuwa kongamano hilo linalotarajiwa kuwahusisha wafugaji kutoka mikoa mbalimbali nchini, huku likitarajia kutoa afua ya masuala ya sera za ufugaji, teknolojia mpya, masoko ya bidhaa za mifugo, pamoja na umuhimu wa uhifadhi wa mazingira katika shughuli za ufugaji.

kwa Kuwa ni mara ya ya kwanza kwa Tanzania kuwa na kongamano la kitaifa la utoaji chanjo na utambuzi kwa mifugo jambo ambalo limefanyika katika uongozi wa awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Sauti ya Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Ndugu Mrida Mshota

Wednesday, 4 June 2025

Vikundi vya ulinzi shirikishi hupunguza uhalifu kwenye jamii

 

Mkaguzi wa polisi Jonas Kaijage ambaye ni mratibu wa polisi jamii wilayani Bunda

Bunda kuna jumla ya vikundi 31 vya ulinzi shirikishi ambavyo vipo hai na katika maeneo hayo matukio ya uharifu yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Na Adelinus Banenwa

Imeelezwa kuwa sehemu zenye vikundi vya ulinzi shirikishi yaani polisi jamii wilayani Bunda matukio ya kiharifu yamepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na maeneo ambayo hakuna kabisa vikundi hivyo.

Hayo yamesemwa na mkaguzi wa polisi Jonas Kaijage ambaye ni mratibu wa polisi jamii wilayani Bunda kupitia kipindi cha Asubuhi leo kinachorushwa Radio Mazingira fm ambapo amesema kwa wilaya ya Bunda kuna jumla ya vikundi 31 vya ulinzi shirikishi ambavyo vipo hai na katika maeneo hayo matukio ya uharifu yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Kaijage ameongeza kuwa sheria ya kuwepo kwa ulinzi shirikishi una lengo la kuishirikisha jamii katika masuala ya ulinzi na usalama katika maeneo yao ndiyo maana kama jeshi la polisi wanahusika kutoa elimu na maelekezo kwa vikundi vinavyoanzishwa.

Kaijage ametoa wito kwa jamii kuhakikisha kupitia kwa wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji wanaanzisha vikundi hivyo ili kuweka usalama kwenye maeneo yao kwa kuwa sasa jeshi la polisi limesogeza karibu kabisa huduma na vikundi hivyo ikiwa nipamoja na kila kata kuwepo kwa polisi kata ambaye anasaidia kutoa elimu kwa vikundi hivyo.

Sauti ya Jonas Kaijage ambaye ni mratibu wa polisi jamii wilayani Bunda

Kwa upande mwingine Insp Kaijage amewataka wafanyabiashara wanaotoa huduma za kifedha kwa maana ya huduma pesa kuwa waangalifu kutokana na changamoto za wizi na utapeli ambao unaonekana kushamili kwa siku za hivi karibuni.

Sauti ya Jonas Kaijage ambaye ni mratibu wa polisi jamii wilayani Bunda