Friday, 21 March 2025

Diwani wa Ketare ambaye ni Mkurugenzi Radio Mazingira na atunukiwa hati ya Pongezi

 

Diwani wa kata ya Ketare Mhe Mramba Simba Nyamkinda akipokea hati ya pongezi kutoka kwa mwenyekiti wa CCM Bunda

viongozi hao wameonesha umoja na ushirikishanaji wa taarifa za miradi pindi inapopelekwa kwenye maeneo yao.

Na Adelinus Banenwa

Halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Bunda imewapongeza baadhi viongozi wilayani Bunda kwa utekelezaji na usimamizi wa miradi ya serikali kwenye maeneo yao.

Akizungumza katika kikao cha halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Bunda Mwenyekiti wa CCM wilaya, Abraham Mayaya Magese amesema viongozi hao wameonesha umoja na ushirikishanaji wa taarifa za miradi pindi inapopelekwa kwenye maeneo yao.

Wajumbe wa halmashauri ya wilaya kuu CCM wilaya ya Bunda

Akizungumzia mradi wa shule ya sekondari ya Nyaburundu iliyopo kata ya Ketare, Mayaya amesema kamati ya siasa baada ya kufika katika mradi huo ilikuta kuanzia viongozi wa kata mpaka wananchi wanataarifa zinazofanana kuhusu mradi huo.

Sauti ya Mwenyekiti wa CCM wilaya, Abraham Mayaya Magese

Miongoni mwa waliotunukiwa hati hizo za pongezi ni pamoja an Mhe Diwani wa Kata ya Ketare Mramba Simba Nyamkinda, mkuu wa shule ya msingi Nyaburundu, Mwenyekiti wa CCM kata ya Ketare, Diwani wa kata ya Nyasura Magigi Samweli Kiboko, miongoni mwa viongozi wengine.

Diwani wa kata ya Nyasura Magigi Samweli Kiboko akipokea hati ya pongezi kutoka kwa mwenyekiti wa CCM Bunda

Wakizungumza Mara baada ya kupokea hati hizo Diwani wa kata ya Ketare Mhe Mramba Simba Nyamkinda na diwani wa kata ya Nyasura Magigi Samweli Kiboko wamesema

Sauti za madiwani waliotunukiwa hati za pongezi

Wednesday, 19 March 2025

Wananchi watakiwa kuzingatia usafi kuepuka magonjwa ya mlipuko

 

Wananchi watakiwa kuzingatia usafi kuepuka magonjwa ya mlipuko

19 March 2025, 

Maafisa afya kutoka halmashauri ya mji wa Bunda

Kazi kubwa ya wataalamu ni kutoa elimu kwa jamii ili kudhibiti magonjwa ya milipuko kama vile kipindupindu, kichocho, miongoni mwa magonjwa mengine.

Na Adelinus Banenwa

Wito umetolewa kwa jamii kuzingatia usafi wa mazingira na vyakula ili kuepukana na magonjwa ya mlipuko ambayo ni hatari kwa afya za wananchi,

Hayo yamesemwa na maafisa afya kutoka halmashauri ya mji wa Bunda wakati wakizungumza kupitia kipindi cha Asubuhi leo kinachorushwa na radio Mazingira Fm.

Mohamed  Mlanza mratibu wa utoaji elimu ya afya kwa jamii kutoka halmashauri ya mji wa Bunda

Mohamed  Mlanza mratibu wa utoaji elimu ya afya kwa jamii kutoka halmashauri ya mji wa Bunda amesema kazi yao kubwa kama wataalamu ni kutoa elimu kwa jamii ili kudhibiti magonjwa ya milipuko kama vile kipindupindu, kichocho, miongoni mwa magonjwa mengine,

Akizungumzia ugonjwa wa homa ya nyani (M-POX) Mlanza amesema ugonjwa huo umeshatangazwa na serikali kwamba upo hivyo ni jukumu la wananchi kuchukua tahadhari endapo wataona dalili za ugonjwa huo ambazo ni pamoja na vipere sehemu za usoni, miguuni, mikononi , homa , maumivu ya kichwa miongoni mwa dalili zingine.

Sauti ya Mohamed  Mlanza mratibu wa utoaji elimu ya afya kwa jamii kutoka halmashauri ya mji wa Bunda
Amani Mashauri Jumbula, afisa afya halmashauri ya mji wa Bunda

Kwa upande wake Amani Mashauri Jumbula, afisa afya halmashauri ya mji wa Bunda amesema mbali na elimu inayotolewa lakini jukumu kubwa lipo kwa wananchi kuzingatia usafi hasa katika magonjwa kama kipindupindu chanzo chake ni uchafu hasa pale mtu anapokula chakula chenye vimelea vya wadudu wa kipindupindu ambao msingi wake ni kinyesi .

Ametoa wito kwa jamii kuzingatia kanuni zote za afya ikiwemo kunawa mokono, kuwa na vyoo bora , kuepuka kula vyakula ambavyo nivyabaridi miongoni mwa tahadhari zingine.

Sauti ya Amani Mashauri Jumbula, afisa afya halmashauri ya mji wa Bunda

Saturday, 15 March 2025

 

Bunda kuadhimisha miaka minne ya Rais Samia Machi 17

15 March 2025, 5:46 pm

Katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela

Miongoni mwa maeneo yatakayoangaziwa ni pamoja na sekta mbalimbali za serikali ikiwemo Maji, Umeme, Afya, Barabara pamoja na Elimu.

Na Adelinus Banenwa

Serikali wilayani Bunda imewaomba wananchi wote kuudhuria maadhimisho ya miaka minne ya serikali ya awamu ya sita chini ya rais Samia Suluhu Hassan yanatarajiwa kufanyika Tarehe 17 March 2025.

Akizungumza na radio mazingira fm ofisini kwake katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela amesema wananchi wote wanaalikwa siku hiyo ya jumatatu ambapo watapata nafasi ya kusikiliza kile serikali ya awamu ya sita imefanya ambapo mgeni rasmi atakuwa ni mkuu wa wilaya ya Bunda Mhe Aswege Enock Kamnyoge.

Sauti ya Katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela

Aidha Mtelela amesema ratiba ya maadhimisho hayo inatarajiwa kuanza na zoezi la upandaji miti katika eneo la Kunzugu kisha kwenye viwanja vya ukumbi wa Maika na miongoni mwa maeneo yatakayoangaziwa ni pamoja na sekta mbalimbali za serikali ikiwemo Maji, Umeme, Afya, Barabara pamoja na Elimu.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka minne ya rais Samia wilaya ya Bunda imepokea kiasi cha fedha za miradi zaidi ya Bilion 247 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Sauti ya Katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela

Ikumbukwe Rais Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania mnamo March 19, 2021 baada ya kifo cha mtangulizi wake Hayati Dr John Pombe Magufuli Rais awamu ya tano.

Sunday, 9 March 2025

 

Mbunge Ghati ahimiza ushirikiano kwa wanawake

Mbunge viti maalumu mkoa wa Mara kutia kundi la wanawake Mhe Ghati Chomete

Mbali na kuwataka wanawake kuwa na mshikamano pia amesema ni lazima zisemwe kazi nzuri zilizofanywa na serikali awamu ya sita chini ya rais Samia Suluhu Hassan

Na Adelinus Banenwa

Wito umetolewa kwa wanawake wote kuwa na ushirikiano na kujenga tabia ya kupendana ili kutimiza adhma ya nafasi ya mwanamke katika jamii.

Hayo yamesemwa leo tarehe 7 March 2025 na mbunge viti maalumu mkoa wa Mara kupitia kundi la wanawake Mhe Ghati Chomete katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambapo kwa wilaya ya Bunda yamefanyika leo katika viwanja vya CCM wilaya ya Bunda.

Mbunge viti maalumu mkoa wa Mara kutia kundi la wanawake Mhe Ghati Chomete, Akiwa na mwenyekiti wa kamati ndogo ya fedha na uchumi CCM Bunda Ndugu Kambarage Wasira

Mbunge Chomete kama mgeni rasmi katika maadhimisho hayo wilayani Bunda mbali na kuwataka wanawake kuwa na mshikamano pia amesema ni lazima zisemwe kazi nzuri zilizofanywa na serikali awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kama vile miundombinu ya maji barabara, umeme elimu miongoni mwa kazi zingine.

Sauti ya mbunge viti maalumu mkoa wa Mara kutia kundi la wanawake Mhe Ghati Chomete
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bunda Ndugu Abraham Mayaya Magese

Naye mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bunda Ndugu Abraham Mayaya Magese amewapongeza wanawake kwa kuadhimisha siku yao huku akisema chama cha mapinduzi kinatambua mchango mkubwa unafanywa na wanawake viongozi wa chama cha mapinduzi na serikali huku akiwata viongozi hao kutatua kero za wananchi kila mmoja kwa eneo alilopo iwe ni ngazi ya mtaa au kijiji, Kata, mpaka wilaya.

Sauti ya mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bunda Ndugu Abraham Mayaya Magese

Aidha viongozi hao wasemema kazi kubwa ya CCM ni kuangalia na kutatua kero za wananchi wakitolea mfano utatuzi wa migogoro baada ya tamko la hivi karibuni kuhusu mabasi kusitisha kushusha abiria katika vituo vya Nyasura na Bunda DDH ambapo kupitia viongozi hao wameeleza kuwa tayari malalamiko ya bodaboda na wajasiliamali yamefanyiwa kazi na mabasi yataendelea kushusha abiria katika vituo hivyo.

Sauti ya mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bunda Ndugu Abraham Mayaya Magese

Miongoni mwa viongozi waliokuwepo kwenye Maadhimisho hayo ya siku ya wanawake Duniani ni pamoja na Mwenyekiti wa kamati ya fedha, mipango na uchumi chama cha mapinduzi wilaya ya Bunda Eng Kambarage Masatu Wasira ambaye amesema kuna kila sababu ya kuwapongeza wanawake kwa hatua kubwa ya kimaendeleo walizopiga

Kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani hufanyika March 8, ambapo kwa mwaka huu kitaifa yanatarajiwa kufanyika mkoani Arusha ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan

Thursday, 6 March 2025

 

Anusurika kifo baada ya kushambuliwa na mamba akioga

6 March 2025, 5:29 pm

Anusurika kifo baada ya kushambuliwa na Mamba alipokwenda ziwani asubuhi, rafiki apanda juu ya mamba kunusuru ndugu yake.

Na Adelinus Banenwa

Kijana mmoja aliyetambulika kwa jina la Baraka Jumanne Maseke mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya sekondari Neruma kata ya Neruma halmashauri ya wilaya ya Bunda amenusurika kifo baada ya kushambuliwa na Mamba alipokwenda ziwani asubuhi.

Akizungumza na Mazingira fm mjomba wa kijana huyo aitwaye Exavely Palapala amesema tukio hilo limetokea asubuhi ya tarehe 5 March 2025 majira ya saa kumi na mbili asubuhi ambapo Baraka akiwa ameambatana na rafiki yake aitwaye Dotto Maingu Elias walikwenda ziwani kuoga ili kwenda shule.

Palapala ameongeza kuwa kwa mujibu wa maelezo yao baada kufika ziwani Baraka alikuwa wa kwanza kuingia kwenye maji ndipo alipo dakwa na mamba muda mfupi tu baada ya kuanza kuoga.

Sauti ya Exavely Palapala Mjomba wa Baraka,

Kwa upande wake Dotto Maingu aliyekuwa ameambatana na Baraka ameiambia Mazingira fm kuwa baada tu ya kufika ziwani Baraka alitangulia kuingia majini na yeye alibaki akiwa amekaa ufukweni.

Anasema baada ya muda mfupi tu alisikia kelele za rafiki yake akiwa kwenye maji akiomba msaada ndipo alipovua ngua haraka na kujitosa kwenye maji ili aone namna ya kumsaidia.

Sauti ya Dotto Maingu rafiki yake Baraka

Naye mwenyekiti wa kikiji cha Kasaunga ndugu Benard James Nyamwega amesema ni kweli taarifa za tukio hilo anazo na kuwa tukio hilo lilitokea jana lakini vijana hao hawakwenda kuoga bali kuangali mitego yao ya samaki ndipo mmojawapo akashambuliwa na mamba.

Sauti ya mwenyekiti wa kikiji cha Kasaunga ndugu Benard James Nyamwega

Baraka kwa sasa a anapatiwa matibabu katika Hospitali ya mkoa ya mwal Nyerere ya mkoani maarufu hospitali ya Kwangwa.

Tuesday, 4 March 2025

 

Mtoto Angel aliyezama kwenye rambo apatikana akiwa amefariki

4 March 2025, 

Kaimu kamanda wa zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara Agostino Magere

Mwili wa mtoto huyo umeopolewa na askari wa zimamoto na uokoaji walikuwa eneo la tukio tangu March 2, 2025 walipopata taarifa za tukio hilo.

Na Adelinus Banenwa

Mtoto Angel Wilson 8 mwanafunzi wa darasa la pili shule ya msingi Kataryo B halmashauri ya Musoma Vijijini mkoani Mara aliyedaiwa kuzama kwenye bwana la maji amepatikana akiwa amefariki.

Kaimu kamanda wa zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara Agostino Magere amesema mwili wa mtoto huyo umeopolewa leo na askari wa zimamoto na uokoaji walikuwa eneo la tukio tangu March 2, 2025 walipopata taarifa za tukio hilo.

Magere amesema chanzo cha tukio hilo ni kukosekana kwa umakini ambapo mtoto Angel Wilson akiwa na dada yake wa kidato cha tatu walikwenda kuchota maji ambapo maeneo hayo ni hatari kwa usalama hali iliyopelekea mtoto huyo kutereza na kuzama.

Sauti ya Kaimu kamanda wa zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara Agostino Magere

Magere ametoa rai kwa wananchi kujenga tabia ya kulitaarifu jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara mapema pindi kunapohitajika maokozi ama ya moto au watu kuzama majini.

Monday, 3 March 2025

 

Nyamuswa yetu kwanza yadhamiria kurudisha tabasamu kijijini

3 March 2025, 

viongozi wa serikali na baadhi ya wanachama wa kikundi cha Nyamuswa yetu kwanza

Kikundi hicho kilianzishwa tangu mwaka 2021 na kilianza katika dhima ya kusaidia watu misibani na kusaidia batibabu kwa wale wanaougua lakini hawana uwezo wa kwenda hospitali.

Na Adelinus Banenwa

Kiasi cha pesa taslimu shilingi milioni moja laki sita na elfu therathini na ahadi shilingi milioni nane Mifuko ya saruji 338 pamoja na mabati 108 vimepatikana kwenye harambee ya kuboresha miundombinu ya shule ya msingi Nyansirori.

Mikinyemi Sepeku kwa niaba ya katibu tawala mkoa wa Mara akichukua ndoo kwa ajili ya uzinduzi wa harambee ya upatikanaji wa fedha za kujenga vyumba viwili vya madarasa

Harambee hiyo imeandaliwa na kikundi cha vijana cha Nyamuswa Yetu kwanza ambacho kinapatikana katika kitongoji cha Nyamuswa, kijiji cha Mekomariro, kata ya Mihingo halmashauri ya wilaya ya Bunda.

Wanachama wa kikundi cha nyamuswa yetu kwanza wakikabidhi photocopy mashine ikiwa ni sehemu ya mchango wao kwa shule ya msingi Nyansirori

Akizungumza katika harambee hiyo Mikinyemi Sepeku kwa niaba ya katibu tawala mkoa wa Mara ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema shule hiyo ni miongoni mwa shule ambazo zinahitaji maboresho makubwa kutokana na miundombinu yake kuchakaa Amewapongeza kikundi kilichoandaa harambee hiyo ili kusaidia kuboresha shule hiyo.

Mikinyemi Sepeku kwa niaba ya katibu tawala mkoa wa Mara

Kwa upande wake mwalimu Jafari ambaye ni miongoni mwa walimu kutoka shule ya msingi Nyansirori akisoma taarifa ya shule amebainisha changamoto mbalimbali ambazo zinaikabili shule hiyo kuwa ni pamoja na upungufu wa madarasa, nyoo, madawati, nyumba za walimu miongoni mwa mahitaji mengine.

Sauti ya walimu Jafari ambaye ni miongoni mwa walimu kutoka shule ya msingi Nyansirori

Naye mwenyekiti wa kikundi cha Nyamuswa yetu kwanza ndugu Innocent Joseph amesema kikundi hicho kilianzishwa tangu mwaka 2021 na kilianza katika dhima ya kusaidia watu misibani na kusaidia batibabu kwa wale wanaougua lakini hawana uwezo wa kwenda hospitali.

Innocent ameongeza kuwa baadaye kikundi hicho kiliona ni vema pia kikajikita kwenye maendeleo hivyo wameamua kuanza na shule ya msingi Nyansirori ambapo hadi sasa wameshajichangisha kiasi cha shilingi milioni 13.4 na leo wameamua kuhitisha harambee ili wadau waweze kuwaunga mkono.

Sauti ya mwenyekiti wa kikundi cha Nyamuswa yetu kwanza ndugu Innocent Joseph

Katika harambee hiyo baadhi ya viongozi waliochangia kwa ahadi ni pamoja na ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Bunda kwa kushirikiana na ofisi ya mbunge wa jimbo la Bunda kutoa bati 108, mbunge wa jimbo la Bunda ameahidi kujenga madarasa mawili kwa thamani ya milioni 50 na mtatiro Nyamuhanga Kitinkwi pamoja na marafiki zake wakiahidi kutoa shilingi milioni 6

 

Mtoto wa miaka 8 azama maji kwenye rambo wakati akichota maji

3 March 2025, 

Angel Wilson ( 8) mwanafunzi wa darasa la pili shule ya msingi Kataryo B halmashauri ya Musoma Vijijini anatajwa kuzama kwenye rambo wakati akiteka maji.

Na Adelinus Banenwa

Mtoto mmoja aliyetambulika kwa jina la Angel Wilson ( 8) mwanafunzi wa darasa la pili shule ya msingi Kataryo B halmashauri ya Musoma Vijijini mkoani Mara anatajwa kuzama kwenye rambo wakati akiteka maji.

Akizungumza na Mazingira fm baba mzazi wa mtoto huyo Wilson Wilson amesema alipata taarifa za mtoto wake kudumbikia kwenye mashimo hayo ambayo ni mabaki sehemu yaliyokuwa machimbo ya dhahabu.

Wilson amesema alifanya jitihada za kuwasiliana na viongozi akiwemo afisa madini, jeshi la polisi pamoja na jeshi la zimamoto na uokoaji.

Amesema changamoto kubwa katika eneo hilo ni kwamba mashimo hayo ambayo yalikuwa machimbo ambyo kwa sasa yamejaa maji yapo kwenye makazi ya watu lichaya kuwa kuna walinzi lakini wananchi huenda pale na kuchota maji na kunywesha mifugo.

Sauti ya baba mzazi wa mtoto huyo Wilson Wilson

Kaimu kaimu kamanda wa zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara Agostino Magere amesema taarifa za mtoto huyo kuzama kwenye bwana hilo walizipata siku ya tarehe 2 March na baada ya kufika eneo la tukio taratibu za maokozi zilianza na kutokana na changamoto ya giza pamoja kina kirefu walilazimika kusitisha zoezi mpaka March 3, 2025.

Sauti ya Kaimu kaimu kamanda wa zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara Agostino Magere

Aidha kamanda Magere ametoa wito kwa wananchi hasa wazazi na walezi kuhakikisha wanawachunga watoto hasa katika maeneo hatarishi kama visimani, kwenye madimbwi , au kuchezea vitu vya moto.

Sunday, 2 March 2025

 

Onyo wafanyabiashara watakaopandisha bei bidhaa za chakula Ramadhani na kwaresma

2 March 2025, 

Katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela

Mara nyingi malalamiko ya wananchi yamekuwa ni kwenye bidhaa za mihogo, viazi, tambi sukari miongoni mwa bidhaa zingine.

Na Adelinus Banenwa

Wafanyabiashara wilayani Bunda wametakiwa kujiepusha na upandishaji holela wa bei ya bidhaa za chakula katika kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani na kwaresma.

Akizungumza na radio mazingira fm ofisini kwake katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela amesema serikali inafuatilia kwa ukaribu sana mwenendo wa bidhaa kulingana na bei ya soko ilivyo.

Amesema mara nyingi malalamiko ya wananchi yamekuwa ni kwenye bidhaa za mihogo, viazi, tambi sukari miongoni mwa bidhaa zingine hivyo amewataka wafanyabiashara mbali na kufuata sheria pia wanatakiwa kuwa na utu kwa kuwa kipindi cha mfungo ni ibada.

Mtelela amesema mtu yeyote atakayepata taarifa za mfanyabiashara yeyote anapandisha bei ya bidhaa za chakula katika kipindi hiki bila kufuata utaratibu atoe taarifa kwa wenyeviti au watendaji au ofisi ya mkuu wa wilaya naserikali haitasita kumchulia hatua mtu yeyote atakayekiuka sheria.

Sauti ya katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela